Habari za Punde

Mbunge wa jimbo la Handeni vijijini aanza na kasi ya ugawaji wa miti kwa wananchi.

Na.Hamida Kamchalla

Mbunge wa jimbo la Handeni vijijini mkoani Tanga John Sallu ameanza zoezi la kugawa miche ya miti milioni moja kwa wananchi ambao wapo tayari kuanza kilimo cha miti, ahadi ambayo aliitoa wakati wa kampeni zake mwaka jana wilayani humo. 

Akizungumza wakati wa kumkabidhi mkulima    wa kwanza aliyejitokeza kuhitaji miche hiyo jana katika kata ya Kiva alisema, lengo la kugawa miche hiyo bure ni kutaka wananchi wapate zao la biashara badala ya kutegemea mahindi lakini pia kutunza mazingira,kwani maeneo mengi kuna uharibifu wa misitu.  

Salu alibainisha kwamba ameandaa vitaru viwili vya miti vyenye miche zaidi ya milioni moja na laki sita,na jana amekabidhi miche 1000 kwa mkulima wa kwanza, hivyo mwananchi yeyote anayehitaji kulima miti afike ofisi ya kata au kijiji atapewa maelekezo ya kuandaa shamba na kupewa mbegu hizo bure,gharama yake itakuwa ni kusafirisha.

"Mche mmoja wa miti hii kwa wafanyabiashara wanauza shilingi 400 mpaka 500,nimeandaa miche 1.6 milioni hii ni sawa na shilingi 800,000 milioni (milioni mia nane) nitawapa wananchi wangu bure,lengo ni kupata zao la biashara lakini pia kutunza mazingira yetu baada ya miaka kadhaa Handeni naamini itabadilika,"  alisema Sallu.

Mkulima Rajabu Mlela wa kijiji cha Kweditiline alisema ameamua kulima miti kwasababu anajua faida yake ni kubwa ikifikia wakati wa kuvuna,kwani zao la Mahindi gharama za kuandaa na faida yake ni ndogo sana ukilinganisha na miti ambayo huchukua muda mrefu ila faida ni kubwa.

Alisema shamba la miti pia moja ya faida zake baada ya mwaka unaweza kuchukua mkopo kwenye taasisi za kifedha na kujiendeleza kimaisha,ila shamba la mahindi uhakika wa kupata mkopo ni mdogo maana hata mavuno yake,huwezi kuyategemea kwa asilimia kubwa.

Kaimu ofisa kilimo wa kata ya Kiva Devid Joachim alisema wakulima wanategemea kufanya kilimo cha miti wahakikishe wanafanya mawasiliano na ofisi yao kwa elimu zaidi,lengo ni kuona wakulima wanafaidika na kilimo cha miti ambayo pia itatunza mazingira.

Alisema kwa hatua za awali lazima miti hiyo ipandwe mita tatu kwa mita tatu,huku kanuni nyingine za kilimo zikifuatwa kuhakikisha miche yote milioni moja itakayotolewa na mbunge kwenda kwa wananchi ipone na kuleta tija kwao.

Ukiacha miti hiyo ambayo inaweza kuvunwa mbao na shughuli nyingine,tayari mbunge huyo ameshaanzisha vitaru vingine kwaajili ya kuandaa miche ya mbegu za Miembe ambayo pia itatolewa kwa wananchi wa Handeni vijijini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.