Habari za Punde

Ndoto ya Kuifanya Zanzibar Kuwa Sehemu ya Kutoa Tiba za Kibingwa Sasa Imeanza. - Dk. Hussein Mwinyi

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Madaktari Bingwa Wazalendo wa Kitengo cha Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu katika Hospital ya Mnazi Mmoja waliupofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kuwapongeza, hafla hiyo imefannyika katika ukumbi wa Ikulu.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba ile ndoto yake ya kuifanya Zanzibar iwe ni sehemu ya kutoa tiba za kibingwa sasa imeanza.   

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo wakati alipowapongeza madaktari wa Kitengo cha upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu cha Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar ambao aliwaaita Ikulu Jijini Zanzibar kwa lengo hilo maalum la kuwapongeza.

Pongezi hizo zimekuja mara baada ya kitengo hicho cha wataalamu hao kumfanyia upasuaji mgonjwa Kelesh Belinda raia kutoka nchini Nigeria ambaye hakuwa na imani ya kutibiwa hapa Zanzibar lakini kutokana na uwezo uliopo wa kitengo hicho cha hapa Zanzibar mgonjwa huyo aliweza kutibiwa na hatimae mara baada ya kupona alianza kuipa sifa Zanzibar na kutoa taarifa katika mitandao ya kijamii.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kuna haja ya kuwapongeza madaktari hao kwa kuanza kutoa huduma hizo za kibingwa ambazo ni ngumu jambo ambalo wameonesha kwamba inawezekana katika kutekeleza ndoto zake.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alikipongeza kitengo hicho cha Hospitali ya Mnazi Mmoja  kwa kazi nzuri wanazozifanya ambazo zimepelekea kuwaita Ikulu kutokana na mafanikio  waliyoyapata ambayo yameijengea sifa kubwa Zanzibar.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kuna haja ya kuwapongeza kutokana na kazi hizo licha ya kutambua kwamba wanafanya kazi hizo katika mazingira magumu kwani nia ya kurekebisha mazingira magumu ipo.

Alisema kwamba kazi inayofanywa na kitengo hicho ni kutoa tiba kwani wagonjwa wengi waliokuwa wakisafirishwa kwenda Dar-es-Salaam ama nje ya nchi hivi sasa wengi wanatibiwa Zanzibar ambayo hayo ni mafanikio makubwa kwani lengo ni kuhakikisha wananchi wanatibiwa hapa ndani na kupunguza gharama pamoja na kujenga uwezo.

Dk. Mwinyi aliongeza kuwa pia, kitengo hicho kinajenga uwezo wa kufundisha madaktari na tayari kitengo hicho kimeshapata ithibati ya kuweza kuwatibu hata wagonjwa kutoka nje ya Zanzibar sambamba na kuwepo vifaa vinavyopelekea kufanya aina kadhaa za upasuaji.

Alisema kuwa ile ndoto yake ya kuifanya Zanzibar iwe ni sehemu ya Zanzibar kutoa tiba  za kibingwa wataalamu hao wameonesha mfano kwa kuanza na tiba za kibingwa ambazo ni ngumu.

Alisema kuwa waataalamu hao wameonesha kwamba hilo linawezekana na tayari katika Hospitali ya Mnazimmoja wameshajenga uwezo wa miundombinu kwa maana ya majengo, vyumba vya upasuaji, vifaa na kuanza kutoa elimu.

Alisema kuwa hayo yote ni mafanikio makubwa ambayo yamepelekea kutekeleza ndoto yake huku akieleza kwa kutoa mifano ya Hospitali ya Jakaya Kikwete Dar-es-Salaam, ana uhakika iwapo huduma za tiba ya hiyo itatolewa, tiba ya moyo pamoja na  kansa sehemu kubwa ya watu wanaopelekwa nje watatibiwa hapa hapa Zanzibar.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza jambo ambalo linataka kufanywa na Serikali ya Awamu ya Nane ni kujenga miundombinu kwa jengo jipya la kisasa ili kutoa mazingira bora ya kufanya kazi hizo ili kuhakikisha wataalamu kutoka sehemu mbali mbali waje  kutoa huduma hizo sambamba na kujenga uwezo wa ndani.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa nguvu za serikali zinahitajika katika kuhakikisha mazingira yanakuwa mazuri na kuweza kuwaunga mkono wale wanaotoa msaada wao kwa Zanzibar katika huduma hiyo.

“Leo nimefurahi sana na nakupongezeni kwa kazi nzuri mnayofanya ambayo imekuwa na sifa dunia nzima tunasikia watu mpaka wa nje kwa kazi nzuri mnazofanya”,alisema Dk. Mwinyi.

Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Profesa Jose Piquer Belloch kwa juhudia zake anazozichukua na kusema kuwa mbali ya tiba anayoiotoa pia amekwua akiunga mkono kwa kusaidia vifaa.

Alisema kuwa yeye pamoja na Serikali anayoiongzoa itaendelea kumuunga mkono bingwa huyo kutoka Hispania na kumuhakikishia  kwamba anapata kibali cha kuishi na kumuwezesha kufanya kazi muda wote hapa Zanzibar na kuitaka Idara ya Uhamiaji kuhakikisha inampa kibali hicho.

Aidha, aliwataka kuendelea kuwahudumia Wazanzibari na kusema kwamba lengo ni kuhakikisha huduma hizo zote zinapatikana hapa Zanzibar hasa ikizingatiwa azma ya Serikali ya kujenga Hospitali ya Kisasa huko Binguni.

Nae Mkuu wa  Kitengo cha upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu cha Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar Dk. Said Idrissa Ahmada  alisema kuwa Idara hiyo ilianzishwa  rasmi Novemba, 2014.

Aliongeza kuwa kabla ya kuanzishwa kitengo hizo  Profesa Joe mnamo mwaka 2008 alifanya upasuaji wa kwanza ambapo alimfayia mtoto aliyetokea Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja na kufanikiwa vyema upasuasaji huo licha ya changamoto ya vifaa iliyokuwepo wakati huo na baada ya hapo ndipo harakati hizo zilianza.

Alisema kuwa Idara hiyo tokea kufunguliwa mwaka 2014 hadi hivi sasa imeshafanya kesi zipatazo 1700 za upasuaji ikiwemo upasuaji wa vichwa maji kwa watoto,  migongo wazi kwa watoto, uvimbe katika ubongo, ajali za vichwa,  uvimbe katika mishipa ya fahamu, huduma za uti wa mgongo na nyenginezo,

Aliongeza kuwa hatua hiyo imepelekea  kupunguza asilimia zaidi ya 50 kupeleka wagonjwa nje ya nchi ikiwemo India na kupunguza gharama kwa Serikali huku .

Alifahamisha kuwa wito waliopata Ikulu kwa ajili ya kupongezwa unatokana na tiba waliyoifanya ya raia wa Nigeria Kelesh Belinda waliomfania upasuaji ambapo kabla ya kufanyia huduma hiyo hakuwa tayari kutibiwa kwa kudhani kwamba Hospitali hiyo haina uwezo kwani Hospitali ya Clobal ilishindwa na kuamriwa aende Dar-es-Salaam.

Dk. Said alieleza jinsi hatua za upasuaji huo walivyozifanya na kuweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na hatimae mgonjwa huyo anaendelea na shughuli zake huko kwao Nigeria.

Mbali na mafanikio hayo, Dk. Said alitumia fursa hiyo kueleza changamoto walizonazo katika kitengo chao huku akitumia fursa hiyo kwa kumpongeza Profesa Joe kwa kusaidia vifaa katika kitengo hicho.

Mapema Profesa Jose Piquer Belloch ambaye pia,  ni Rais wa Taasisi ya Maendeleo ya Elimu inayohusiana na upasuaji wa Mishipa ya Fahamu, Uti wa Mgongo na Vichwa, Maji (NED) ambaye ni raia kutoa Hispania alipongeza mashirikiano anayoyapata hapa nchini huku akiahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali katika kutoa huduma hizo.

Daktari Bingwa huyo alitoa pongezi zake kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuwajali madaktari hao na kuwaita Ikulu akiwa na lengo la kuwapongeza kwa kazi zao nzuri wanazozifanya katika kuisaidia jamii.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.