Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi Akijumuika katika Sala na Dua ya Kumuombea Mwanachuoni Mkubwa Afrika Mashariki na Kati Marehemu Sayyid Hussein Badawy Iliofanyika katika Masjid Mushawr Muembeshauri Jijini Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj.Dk. Hussein Ali Mwinyi akijumuika na waumini wa Dini ya Kiislam Zanzibar  katika Sala na Dua maalum ya kumuombea Mwanachuoni Mkubwa Afrika Mashariki na Kati Marehemu Sayyid Hussein Badawy, aliyezikwa jana Lamu Nchini Kenya, Sala na Dua hiyo imefanyika katika Masjid Mushawar Muembeshauri Jijini Zanzibar leo 12-2-2021.    

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyiamejumuika pamoja na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya “Ghaib” ya Marehemu Sayyid Hussein Ahmad Badawy aliyekuwa Mwanachuoni mkubwa Afrika Mashariki na Kati.

Sala hiyo ya “Ghaib” iliyofanyika katika Msikiti wa Mwembeshauri, Jijini Zanzibar ilihudhuriwa na Waumini  mbali mbali wa Zanzibar wakiwemo viongozi wa Serikali na viongozi wa dini kama vile Masheikh, Maulamaapamoja na wananchi.

Alhaj Dk. Mwinyi mapema aliungana na Waumini hao katika msikiti huo kwa ajili ya Sala ya Ijumaa ambapo akisoma hutuba ya Sala hiyo ya Ijumaa katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume alisema kuwa kifo cha Mwanachuoni huyo kimewagusa watu wengi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati pamoja na nyenginezo duniani.

Katika hotuba yake hiyo alisisitiza haja ya mwananadamu kuyafanya maisha yake kuwa historia, na kusema kwamba kifo cha Mwanachuoni huyo ni msiba ambao hauna mfano wake na ni pengo ambalo halizibiki.

Alisema kuwa mtu bora ni yule ambaye anawasomesha wenziwe mambo ya kheri ambapo Mtume Muhammad (S.A.W) amesisitiza kwamba mbora miongoni mwa watu ni yule aliyewafundisha wenziwe Qur-an huku Sayyid Omar akisisitiza kwamba elimu ni bora kuliko mali.

Akisoma historia fupi ya Sharif Sayyid Hussein Badawy, Sayyid Mohammed Omar Al Sheikh Juddah alisema kuwa Mwanachuoni huyo amekutwa na mauti huko Lamu, katika Jamhuri ya Kenya hapo juzi (Februari 10, 2021) akiwa ametimiza umri wa miaka 88.

Alisema kuwa maziko ya Ulamma huyo yalifanyika jana (Februari 11, 2021), kwenye makaburi ya huko huko kwao Lamu.

Kwa maelezo ya Sheikh Mohammed Omar Al Sheikh Juddah, Mwanachuoni huyo alizaliwa Lamu mnamo mwaka 1933 Milaadiya ambaye ni miongonimwa watoto 21 wa familia ya Alhabib Sayyid Ahmad Badawy Bin Swaleh bin Alwy Jamal Leyl.

Alisema kuwa Mwanachuoni huyo alifika Zanzibar  na kuishi kuanzia mwaka mmoja-1963 hadi 1964 ambako alijiunga na Muslim Academy, chuo maarufu cha Kiislamu kwa eneo hili la Afrika Mashariki, kilichokuwepo Forodhani Zanzibar ambako alifungua madrasa na Ali Al Beidh Al habib Omar Bin Abdalla au Mwinyibaraka.

Katika safari yake ya kutafuta elimu na kufundisha  ilimfikisha nchini Uganda akitokea Zanzibar mwaka 1964 baadae alikwenda Zaire, Burundi na Sudan ambapo akiwa Uganda alijenga Masjid Hudaa pamoja na kuanzisha madrasa.

Alieleza kwamba Mwanachuoni huyo alikuwa msomi mzuri wa Qur-an, alikuwa msomi mzuri wa tajwid, amesomesha, msomaji wa samai, alikuwa mtunzi wa mashairi ya Kiarabu na Kiswahili na mtunzi wa Nashid ambapo moja ya Kaswida zake ni “Nyoyo zimefurahika kwa kuzaliwa Nabiya”.

Alifahamisha kwamba Sharif Sayyid Hussein Badawy alifikwa na maradhi yalimuweka ndani  muda wa miaka miwili mpaka mauti yalipomkuta ambapo Marehemu ameacha wake watatu waliomkalia eda huku akiwacha watoto 45 alioruzukiwa na Allah.

Alieleza kuwa kabla ya hapo, mwaka 1951 aliishi Tanganyika akianzia na Dar es Salaam ambako alianzisha Masjid Badawy ulioko karibu na lililoitwa Soko Mjinga la Kisutu ambapo alama nyengine aloiwacha ni madrasa ya mtaa wa Mkunguni na Yambuu Badawy iliyopo Yombo, Dar es Salaam.

Nae Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabih alieleza jinsi alivyomfahamu Mwanachuoni huyo pamoja na nasaba yake huku akisisitiza kwamba Zanzibar imefiwa na ndugu yao huyo kwani alikwua si Mkenya tu bali pia alikuwa ni Mzanzibari.

Nae Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume alitoa salamu za Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi, alisema kuwa kiongozi huyo anatoa mkono wa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki, wanachuoni, Masheikh pamoja na wananchi wote.

Aliongeza kwua Alhaj Ali Hassan Mwinyi alikuwa na ukaribu Mkubwa na Mwanachuoni huyo ambapo katika uhai wake wakati huo Mwanachuoni huyo ambaye ametumia nusu ya uhai wake Tanzania alikuwa akimualika Rais huyo Mstaafu.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi alimtembelea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mstaafu Balozi Seif Ali Iddi huko nyumbani kwake Kama, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.