Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Ametoa Agizo Hadi Mwisho wa Mwezi wa Tatu Barabara ya Uwanja wa Ndege Hadi Mnazi Mmoja iwe imekamilika

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza Wananchi wa Nyerere kwa Mtimwa jeni wakati wa ziara yake kukagua Mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) alipofika katika eneo hili kuagalia mmoja wa Mtaro uliojengwa na Mradi huo wa kupitishia maji machafu na ya mvua.    

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi ametembelea baadhi ya maeneo yamradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) huku akitoa agizo la kuhakikisha hadi mwisho wa mwezi wa tatu sehemu zilizokuwa hazijakamilika katika eneo la barabara ya uwanja wa ndege wa Zanzibar hadi MnaziMmoja ziwe zimekamilika.

Rais Dk. Hussein aliyasema hayo leo wakati wa ziara yake hiyo ambayo alipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali yaliyomo kwenye mradi wa ZUSP katika mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na kukagua Jaa kuu la Kibele huku akiwasikiza changamoto za baadhi ya wananchi aliokutana nao njiani.

Akimalizia ziara yake aliyotembea kwa miguu kutoa uwanja wa ndege wa Abeid Amani karume hadi Mnazi Mmoja, akiwa amefuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mama Mariam Mwinyi, Dk. Mwinyi alieleza kuridhishwa na maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya Disemba 9,2021 licha ya kuwa baadhi ya maeneo hayajakamilika na kutaka hadi mwisho wa mwezi ujao yakamilike.

Alisisitiza kwamba barabara hiyo ya kutoka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume hadi MnaziMmoja ndio iwe kigezo kwa barabara nyengine zote za Mji wa Zanzibar kwani kinachoonekana ni kuwa bado barabara nyingi za mji  ni chafu.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuzipongeza na kutoa shukurani kwa Kampuni zilizounga mkono katika kusaidia kuweka vigae, bustani na matengenezo mengine pembezoni mwa barabara hiyo inayotoka uwanja wa ndege hadi Mnazi Mmoja huku akivisifu Vikosi vya SMZ kwa kuunga mkono matengenezo hayo katika maeneo yao.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisikitishwa na tabia ya maeneo ya hifadhi ya barabara kufanywa sehemu ya biashara na kuagiza kutafutwa taratibu za kuhakikisha kadhia hiyo inaondoshwa.

Pia, alieleza jinsi ya miti iliyopandwa katika barabara za Mjini pamoja na kuwepo baadhi ya taa ambazo haziwaki na kutoa agizo kwa wale wote waliopewa jukumu hilo katika mradi huo wa ZUSP kuhakikisha changamoto hiyo inafanyiwa kazi.

Hivyo, aliutaka uongozi wa Serikali ya Mkoa, Wilaya pamoja na Manispaa katika kuhakikisha suala la usafi na mipango ya Miji linafanyiwa kazi huku akisisitiza umhimu wa kukusanya kodi na kuwataka Wakurugenzi wa Manispaa kuhakikisha wanakusanya kodi.

Aidha, akieleza juu ya vyombo vya usafiri kupita katika maeneo ya Mji Mkongwe, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wananchi waliolalamikia suala la usafiri katika eneo hilo kwamba usafiri wa bodaboda umekatazwa katika eneo hilo kutokana na sababu maalum za uhifdhi wa Mji Mkongwe.

Pia, kwa upande wa wananchi alisema kuwa utaratibu wa kuzuia vyombo hivyo kwa watu binafsi unakwenda kwa awamu hivyo, hairuhusiki kuwazuia wananchi kupita katika sehemu hizo bila ya kuwawekea utaratibu maalum na kuutaka uongozi wa Mkoa na Wilaya kulisimamia hilo.

Rais Dk. Mwinyi, pia aliutaka uongozi wa Mkoa na Manispaa ya Mjini kukaa na wananchi waliotoa wazo la kujengwa mtaro katika eneo la MnaziMmoja ili kuuhami uwanja huo ambao umekuwa ukituama maji wakati wa mvua pamoja na pembezoni mwa Hospitali ya Mnazi Mmoja katika eneo la Dodoma.

Katika ziara hiyo, Rais Dk. Mwinyi aliitaka Wizara ya Mawasiliano kupitia Wakala wa barabara kuhakikisha inalitengeneza vizuri eneo la barabara iliyokaa muda mrefu bila ya kutiwa lami na kuleta usumbufu kwa wapita njia.

Akiwa katika eneo la Kilimani baada ya kupokea na kusikiliza malalamiko ya mwananchi mkaazi wa nyumba za maendeleo za Kilimani, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya wananchi kulipa kodi za makaazi katika nyumba hizo ili pesa zinazopatikana ziweze kufanyia ukarabati wa nyumba hizo

Aidha, aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kuangalia sheria zinasemaje kwa wale wenye baa kuweko na utaratibu maalum wa kuhakikisha hawawabughudhi wananchi wanaoishi karibu ya baa hizo kwa kupiga miziki masaa yote.

Rais Dk.Mwinyi alitoa agizo hilo baada ya kupata masikitiko kutoka kwa Hamida Ali Mwinyigogo aliyeeleza kwamba wamekuwa wakipata kadhia kubwa ya kupigiwa miziki masaa yote.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana alitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar kwa ziara yake hiyo pamoja na kuzishukuru Kampuni zote zilizojitolea pamoja na vikosi vya SMZ katika kutengeneza maeneo ya pembezoni mwa barabara kutoka uwaja wa ndege hadi MnaziMmoja.

Baada ya kuondoka hapo Rais Dk. Mwinyi alielekea Maruhubi katika kituo cha  kukusanya taka na kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na uongozi wa ZUSP ambapo Rais alisisitiza kwamba bado kituo hicho hakijafanya kazi yake ipasavyo.

Hivyo, aliziagiza taasisi husika kuhakikisha inazitoa taka katika eneo la mji wa Zanzibar pamoja na kuhakikisha wanazifanyia ukarabati gari zao ili kurahisisha zoezi hilo huku akiwataka kuacha urasimu.

Akiwa katika eneo la Kwamtumwa Jeni, Rais Dk. Mwinyi alisikiliza malalamiko ya wananchi juu ya kutuama kwa maji katika eneo hilo la makaazi yao licha ya kujengwa mtaro katika mradi wa ZUSP na kuagiza kampuni ya CRJEya China, kuhakikisha inarudi tena kurekebisha tatizo hilo kabla ya kupewa fedha zao.

Rais Dk. Mwinyi pia, alifika katika kituo cha kukusanya taka Kwa Binti Hamrani, huko Mpendae Mjini Unguja na kupewa maelezo juu ya huduma zitakazotolewa katika kituo hicho.

Akiwa katika eneo la Kwarara, Wilaya ya Magharibi B, Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua zitakazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kituo cha Polisi kinakuwepo katika eneo hilo pamoja na kutatua changamoto ya barabara kituo cha afya pamoja na maji safi na salama kwa wananchi wa eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana alieleza jitihada zilizochukuliwa katika kuzuia uchimbaji mchanga katika eneo hilo pamoja na utupaji taka ovyo kwa kushirikiana na ulinzi shirikishi ambapo wamezikamata gari 6 za ng’ombe na ng’ombe 8 huku akilitaka Shirika la Umeme Zanzibar ZECO kusimami ulinzi katika nguzo lizopita umeme mkubwa katika eneo hilo.

Baada ya hapo, Rais alifikaeneo la  Jaa la Kibele, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, na kueleza haja ya kuwa na orodha ya gari zote zinazotoa huduma za maji machafu ili iwe rahisi kuweza kuondoa changamoto ya kumwanga maji katika maeneo yasiyoruhusika badala ya kumwaga katika eneo hilo na zile zitakazokaidi zifutiwe leseni.

Aidha,  Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja,Rashid Hadidu Rashid alimueleza Rais changamoto ya ukosefu wa maji taka yanayotakiwa katika eneo hilo kwa ajili ya mradi huo katika eneo hilo la Kibele.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alizitaka Manispaa za Mkoa wa Mjini Mgharibi kukusanya taka na kupeleka katika eneo hilo na wasione mzigo kwani taka ni mali kwa ajili ya kupata umeme sambamba na kujua kiasi cha taka wanazozalisha.

Akizungumza na wananchi waliokwenda kutoa malalamiko yao juu ya fidia katika eneo hilo la Kibele, Rais Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Wizara ya Nchi (OR) Fedha na Mipango kuhakikisha unafanya uhakiki na kuhakikisha zoezi la fidia linafanyika kwa uadilifu kwani kuna baadhi ya wafanyakazi katika ofisi hiyo si waadilifu.

Sambamba na hayo, aliwataka wananchi hao kwa upande wao kuridhika na kile wanachopewa badala ya kufuatwa utaratibu uliowekwa kwani kila mtu atapewa fidia kwa vigezo vilivyowekwa.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.