Baadhi ya Wasanii kutoka Bara na Zanzibar waliohudhuria Uzinduzi wa Filam ya Ndonga Ukumbi wa Sanaa Raha leo Mjini Zanzibar.
Picha Na Bahati Habibu - Maelezo Zanzibar
MARYAM KIDIKO MAELEZO ZANZIBAR 13/ 2/2021
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana , Utamadni na Michezo Fatma Hamad Rajab amewataka wasanii nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia mila, tamaduni na desturi za Kitanzania ili ziweze kudumu na kurithisha vizazi vijavyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa Filamu ya Ndonga ilioandaliwa na kikundi cha Allan Culture kutoka Dar es Salaam huko ukumbi wa Sanaa Rahaleo amesema utamaduni ni lulu ambayo inahitaji kuenziwa, hivyo Sanaa zitumike vizuri katika kuutangaza utamaduni wa Mtanzania ndani na nje ya nchi.
Amesema watu wengi wamepata maendeleo kupitia Sanaa hivyo amewataka vijana kujifunza Sanaa ili waweze kuzalisha Sanaa yenye viwango inayokubalika na jamii hatua ambayo itaibuwa fursa nyingi za ajira na kuwaingizia kipato.
Akizungumzia kuhusiana na Filamu ya Ndonga bi. Fatma ameeleza kuwa filamu hiyo iliyobeba maudhui ya kuielimisha jamii juu ya kulinda mazingira ya bahari na madhara yatokanayo na uvuvi haramu, itasadia kuipa mwanga jamii katika kufikia azma ya serikali ya kufikia maendeleo ya uchumi wa buluu.
Aidha amewasisitiza wasanii kujisajili katika vyombo husika ili waweze kutambulika na kupata haki zao za msingi kupitia kazi zao.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Khamis Abdallah Said amesema filamu ya Ndonga itumike kutoa elimu kwa jamii ili mazingira ya bahari yawe salama na kuweza kuliingizia mapato taifa.
Kwaupande wake Mkurugenzi wa kikundi cha Allan Culture Mwahija Mungi amesema Sanaa ni kazi kama kazi nyengine hivyo ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo kuionesha filamu ya donga kupitia vyombo vya habari vilivyopo Zanzibar ili maudhui ya filamu hiyo ifike katika jamii ya wazanzibari kwa haraka.
No comments:
Post a Comment