Habari za Punde

Wafanyakazi wa mradi wa Viungo Zanzibar waendelea na mafunzo

Wafanyakazi wa  mradi wa Viungo Zanzibar wenye lengo la kuwawezesha wakulima wa matunda mboga mboga na viungo (Spice) wakiendelea na mafunzo ya siku moja yenye lengo la kuwajengea uwezo katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku.
Afisa kutoka taasisi ya People Development Forume (PDF) John Malanilo akitoa ufafanuzi kwa wafanyakazi wa mradi wa Viungo katika ofisi za mradi huo zilizopo Mwanakwerekwe mjini Unguja.

 Mkurugenzi mtendaji wa People Development Forume (PDF) Jorua Kizito akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

Na Muhammed Khamis

Kwa lengo la kuongeza ufanisi wa majukumu wafanyakazi wa mradi wa Viungo Zanzibar  wamepatiwa mafunzo ya kiutendaji ambayo yanalenga kuongeza ufanisi katika majukumu yao ya kila siku kupitia shughuli za kilimo cha mboga mboga matunda na viungo katika shehia 50 za Unguja na Pemba.

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika ofisi za mradi huo zilizopo Mwanakwerekwe mjini Unguja na kuongozwa na watendaji kutoka taasisi ya People development Forume (PDF) ya Dar es Salama ambayo ni moja miongoni mwa taasisi shiriki katika utekelezaji wa mradi huo wa miaka minne.

Akifungua mafunzo hayo Meneja mradi Amina Ussi Khamis alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wafanyakazi katika majukumu yao ya kila siku.

Alisema kwa kuwa mradi huo unakwenda kuwasaidia wananchi kupitia shughuli mbali mbali za kilimo cha matunda na mboga mboga kuna haja wafanyakazi kufahamu vyema wajibu wa majukumu yao ya kila siku kwa lengo la kupunguza usumbufu katika shughuli za kiutendaji.

Aliwataka wafanyakazi hao kuyachukua na kuyafanyia kazi mafunzo hayo wakiamini kuwa matarajio ya wananchi wengi wa Unguja Pemba ni kupitia mradi huo wa kilimo.

‘’Mradi huu unakwenda kuwasaidia wananchi 21,000 Unguja na Pemba hivyo hata Serikali yetu ina matumaini makubwa na mradi huu’’aliongezea.

Awali akiwasilisha mada katika mafunzo hayo afisa kutoka taasisi ya People Development Forume ya Dar es Salam John Malaniko alisema kila mfanyakazi kupitia mradi huo ana wajibu wa kutambua na kufahamu vyema majukumu yake ya kazi.

Alisema  kikawaida wafanyakazi wanapofahamu wajibu wao hutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa na kuepusha usumbufu wa hapa na pale.

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha utafiti na ufuatiliaji kupitia mradi huo Ali Abdalla Mbarouk kutoka taasisi ya Community Forest in Pemba (CFP) aliwataka wafanayakazi hao kuhakikisha wanaandika taarifa za utekelezaji wa kila shughuli ya mradi huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa shirika la People Development Forum (PDF) Jorua Kizito amewataka wafanayakazi hao kufanya kazi kwa bidii muda wote.

Alisema mashirikiano ya pamoja kwa watendaji ndio kupitia mradi huo ndio njia pekee itakayofanya utekelezaji wa mradi huo kufikia malengo.

Mradi huo wa viungo unatekelezwa kwa miaka minne na taasisi ya People Development Forume (PDF),Community Forest in Pemba (CFP) pamoja na Tanzania Media Womena Association TAMWA-Zanzibar chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.