Habari za Punde

Dk Hussein Mwinyi aikumbusha Wizara ya Fedha: Jukumu lenu ni kutafuta fedha za miradi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar,katika mkutano wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa wakati wa kuwaapisha Mawaziri na Makatibu Wakuu, mkutano huo ulimefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.  wakati 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Wizara ya Nchi, Ofis ya Rais, Fedha na Mipango kuendelea na jukumu la kutafuta fedha za miradi na kuziachia Wizara na taasisi kuingia katika mikataba.

Dk. Mwinyi ametoa ufafanuzi huo Ikulu Jijini hapa katika mkutano uliojadili Utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wakati alipowaapisha.

Amesema kazi ya hazina ni kutafuta fedha, hivyo akaitaka Wizara hiyo kuondokana na utamaduni uliozoeleka wa kutafuta fedha za miradi  na kuingia mikataba, jambo ambalo linapswa kufanywa na Wizara au taasisi husika.

“Kuanzia sasa Hazina iwe na kazi ya kutafuta fedha, mikataba iingiwe na sekta husika”, alisema.

Akitoa mfano wa mradi wa ZUSP, Dk. Mwinyi alisema Wizara hiyo iliingia mkataba bila kuzishirikisha sekta zinazohusika, hivyo kuwepo na usimamizi dhaifu wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Akigusia changamoto ya upungufu wa wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Dk. Mwinyi alisema IT ni taaluma maalum, hivyo watumishi wanaopaswa kuajiriwa ni lazima wafanyiwe usaili na wataalamu wa fani hiyo, jambo linalohitaji kuangalia na Tume ya Ajira.

Alieleza pia kuna umuhimu kuangalia namna ya kuwalipa mishahra mizuri wataalamu hao, kwa kuzingatia kuwepo taasisi mbali mbali zenye mahitaji.

Aidha, alisema bado Wizara  hiyo haijafanisha usimamizi mzuri wa fedha za Serikali, kwa kigezo kuwa kumekuwepo fedha nyingi zinzopotea, akitoa mfano wa tukio la karibuni lililofanywa na baadhi ya watendaji wa Vikosi vya SMZ la kujaribu kuajiri wafanyakazi wapya ili kuziba mianya ya fedha zilizokuwa zikipotea kwa miaka kadhaa.

Alisema nusu ya fedha zinazokusanywa na Serikali zinaelekezwa katika kulipa mishahara ya wafanyakazi , hivyo ni wajibu wa Wizara kuhakikisha wale wanaolipwa ni wafanyakazi halali.

Aidha, alisema Mashirika yote ya Serikali yanapatiwa ruzuku na mishahara kwa ajili ya wafanyakazi wake, huku mengine yakiwa hayana faida.

Rais Dk. Mwinyi, alisema bado kazi za ukaguzi wa ndani hazijafanyika ipasavyo, akibainisha kuwepo upotevu mkubwa wa fedha za Serikali, jambo linalothibitisha utekelezaji duni wa kazi hiyo.

Aliipongeza Wizara hiyo kwa kuanza utaratibu wa kurekebisha mifumo, akibainisha mbali na taasisi za Seriklai kupewa fedha , lakini kwa makusudi baadhi yake zimeacha kutumia mifumo ya Elektronik.

“Fedha za TASAF, pamoja na fedha nyingi ya mikopo ya wanafunzi zinapotea kutokana na kushindwa kutumia mifumo, mbali na taasisi hizo kupewa fedha”, alisema.

Aidha, aliitaka Wizara hiyo kukamilisha kazi ya uhakiki wa fedha za wastaafu, TASAF pamoja na ruzuku za pembejeo kwa wakulima na kutuma taarifa ya uhakiki huo kwake, akibainisha kuwepo upotevu mkubwa wa fedha.

Vile vile, aliwataka wataalamu wa Uchumi kuishauri Serikali namna bora ya kupata fedha kwa ajili ya  kuendesha miradi, pamoja na kuangalia uwezekano wa Benki ya Zanzibar (PBZ) kutoa mikopo ya  kuendesha miradi mbali mbali.

Aidha, aliitaka Wizara hiyo kubadilika na kuondokana na urasimu katika mambo yenye tija pamoja na kuziondoa taasisi za kibiashara katika mifumo ya Serikali, akibainisha mashrika/taasisi zinazofanya biashara ni vyema zikawa na mfumo wake.

Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Jamal Kassim Ali alisema katika utekelezaji wa maagizo ya Rais, Wizara hiyo imefanikiwa kukamilika kwa asilimia 90 ya mfumo wa ufuatiliaji na ukusanyaji wa kodi kwa wakati, jambo litakalopunguza ukusanyaji wa mapato kwa fedha taslimu na kuondoa utoaji wa risiti za karatasi, mfumo utakaoanza kutumika  April mosi, mwaka 2021.

Alisema Wizara hiyo ilikutana na kuzungumza na Benki za Biashara, ikiwemo CRDB ili kuangalia maeneo ya Uwekezaji yatakayoweza kushirikiana na Serikali.

Aidha, Wizara ilifanikiwa kukutana na wadau wa kodi ili kutambua changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa kutimiza taratibu za ulipaji kodi.

Akigusia changamoto, Waziri Jamal alisema Wizara inakabiliwa na uhaba wa wataalamu wabobezi wa TEHAMA katika maeneo ya ukaguzi wa mifumo, usalama wa mifumo pamoja na usimamizi wa miradi ya TEHAMA .

Nae, Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk. Juma Malik Akil alisema umefika wakati kwa Wizara hiyo kutuma mapendekezo serikalini kuhusiana na Mashirika ya Serikali yasioleta na tija na kubainisha umuhimu wa kuendelea kuwepo au vinginevyo.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.