Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amejumuika na Wananchi wa Tanzania Kuuaga Mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli Uwanja wa Jamuhuri Dodoma 22-3-2021.

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameon goza viongozi kutoka sehemu mbali mbali duniani pamoja na maelfu ya Watanzania kumuaga aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli aliyefariki dunia Machi 17.2021.

Hafla hiyo ya kuagwa Kitaifa ilifanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Afrika na nje ya Bara la Afrika pamoja na wananchi ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi walihudhuria katika hafla hiyo.

Akihutubia katika hafla hiyo ya Kitaifa, Rais Samia Suluhu Hassan amewatoa hofu wenye mashaka kuhusu uongozi wake akisema kwamba yuko tayari na anao uwezo mkubwa wa kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kuwa licha ya kuwa mwanamke lakini yuko imara na kwamba amepita kwenye mikono ya Hayati Magufuli na hivyo amejivunza mambo mengi kwa sababu alikuwa sio mtu wa kuyumbishwa na mwenye msimamo thabiti kwa kile alichoamini kina maslahi kwa Watanzania na kwamba yeye aliongoza Taifa buila mashaka yoyote.

“Kwa wale ambao wana mashaka mwanamke huyu ataweza kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka niwaambie huyu aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni mwanamke”,alisisitiza Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, alisema kuwa yeye pamoja na viongozi wenzake wako tayari kuendeleza miradi yote iliyoanzishwa na Serikali chini ya uongozi wa Hayati Magufuli huku akimtaja Hayati Magufuli kwamba alikuwa mwanamageuzi, mpambanaji, mtetezi wa rasilimali za Taifa aliyetaka Tanzania iwe nchi ya Viwanda kiongozi ambaye hakuyumbishwa wala kutetereshwa.

Nao Marais waliohudhuria katika tukio hilo walimuahidi Rais Samia Suluhu Hassan kwamba wako tayari kufanya kazi na yeye.

Viongozi hao walimueleza Rais Magufuli kuwa ni simba na shujaa wa Afrika kutokana na uchapa kazi wake mahiri na namna alivyoitetea na kuipigania Tanzania pamoja na Bara lote la Afrika.

Wakitoa salamu zao wamesema Tanzania, Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC na Bara zima la Afrika wamepoteza mtu muhimu katika kipindi hichi ambaye alikuwa bado anahitajika katika kuipaisha Tanzania na Bara zima la Afrika.

Walieleza namna alivyoipigania lugha ya Kiswahili na kuwa na kiu ya kuhakikishwa lugha hiyo inazungumzwa katika Bara la Afrika sambamba na kuipigania Zimbabwe katika kuhakikisha inaondokana na vikwazo vya kiuchumi kwa kuweka tarehe maalum ya kupinga hali hiyo.

Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Makamo Mwenyekiti wa CCM Bara Philip Mangula aliwaeleza wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba anamatarajio makubwa kwamba Rais  Samia Suluhu Hassan atayaendeleza yale yote yaliyoachwa na Hayati Magufuli kwani wote walitembea nchi nzima kuinadi Ilani ya CCM, hivyo anamatarajio makubwa kwamba yote yaliyoahidiwa yatatekelezwa.

Maelfu ya wananchi walihudhuria katika tukio hilo lililopelekea uwanja wa Jamhuri kujaa na kupelekea kuzuiliwa watu kuingia ndani huku wananchi wakitangaziwa kujipanga barabara kwa ajili ya kuuga mwili wa mpendwa wao katika barabara za mji huo wa Dodoma uliojinamia kutokana na kifo cha Rais Magufuli.

Mapema ulipoingia mwili wa Hayati magufuli uwanja ulizizima kwa vilio baada ya wananchi na viongozi kuliona jeneza la mpendwa wao Hayati Magufuli na baada ya hapo taratibu zote za kuagwa kwa mwili wa kingozi Kuu Kitaifa zilifuata ikiwa ni pamoja na Gwaride la Mazishi ya Hayati Magufuli.

Pia, Dua na Sala kutoka TEC iliyosomwa na Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga Rais wa TEC, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania alisoma dua kwa upande wa dini ya Kiislamu, Askofu Dk. Dickson Chilongani, Mwenyekiti wa CCT Dodoma pamoja na Hindu walitoa sala sao.

Wimbo wa Taifa na wimbo wa Afrika Mashariki pamoja na Nyimbo maalum ziliimbwa katika hafla hiyo huku Amidi wa Sherehe hizo Profesa Palamabamba Kabudi Waziri wa Mammbo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisoma wasfu wa Hayati Magufuli.

Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Mazishi alieleza jinsi ya taratibu zote za mazishi zinavyofanyika na zinazyoendelea kufanyika huku akieleza mashirikiano mazuri anayoyapata kutoka kwa Makamo wake Hemed Suleiman Abdullah Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.