Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amehudhuria Maziko ya Hayati Dkt Jihn Pombe Magufuli Kijijini Chato Mkoani Geita leo 26/3/2021.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakiweka Shada la Maua katika kaburi la Hayati Dkt.John Pombe Magufuli aliyekiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yaliofanyika Kijijini  kwao Chato Mkoani Geita leo.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Tanzania (JWTZ), Samia Suluhu Hassan ameongoza mazishi ya Hayati Dk. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mazishi yaliyofanyika mjini Chato, Mkoa wa Geita.

Mwili wa Hayati John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyefariki tarehe 17 Machi 2021 Jijini Dar-es-Salaam umelala katika nyumba yake ya milele eneo la Kilimani Chato Mkoani Geita hivi leo.

Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walihudhuria wakiwemo Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo pia, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa pamoja na Mama Mariam Mwinyi walihudhuria.

Mazishi ya Hayati Dk. John Pombe Magufuli yalifanyika kwa taratibu zote za kidini pamoja na zile za kijeshi ambazo anapaswa kupatiwa Amiri Jeshi Mkuu ikiwemo mizinga 21 ilipigwa ikiashiria heshima kubwa kwa kiongozi huyo.

Hayati Rais Magufuli amezikwa katika makaburi ya familia hapo Chato, Mkoani Geita ambapo vilio vilitawala kutoka kwa familia, viongozi pamoja na wananchi waliokuwepo katika tukio hilo na wale waliokuwa wakiangalia moja kwa moja kupitia televisheni pamoja na wale waliokuwa wakisikiliza kutoka redioni.

Kabla ya kupigwa mizinga hiyo 21 wawakilishi wa familia pamoja na baadhi ya viongozi wakiongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan walipata fursa ya kuweka udongo pamoja na maua katika kaburi la Hayati Dk. John Pombe Magufuli.

Mapema asubuhi huko katika kiwanja kilichopewa jina lake, kiwanja cha Magufuli kiliopo mjini Chato, Misa takatifu ya kuuombea Hayati Rais Magufuli ilifanyika katika viwanja hivyo ambayo iliongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga.

Ambapo kwa upande wa Ibada ya mazishi iliongozwa na Askofu Serverine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara.

Sambamba na hayo, viongozi mbali mbali walipata fursa ya kutoa salamu zao za pole kwa wanafamilia pamoja na Watanzania wote kwa jumla.

Akitoa salamu zake za pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan alitoa pole kwa familia ya Hayati Dk. John Pombe Magufuli kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Rais Samia aliwahakikishia wakaazi wa Chato pamoja na Watanzania wote kwa jumla kwamba atahakikisha ahadi zote zilizotolewa katika Ilani ya Uchaguzi na zile alizozitoa Hayati Magufuli zitatekelezwa hatua kwa hatua.

Rais Samia alitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama, familia pamoja na Ofisi ya Hayati Magufuli kwa mashirikiano yao waliyoyaonesha katika kipindi hichi cha msiba.

Alieleza utekelezaji wa ahadi ya Hayati Rais Magufuli ya kuifanya Wilaya ya Chato kuwa Mkoa na kusisitiza kwamba mchakato tayari umeshaanza na kinachoangaliwa ni vigezo na iwapo vigezo havijakidhi maelekezo yatatolewa ili kuhakikisha hilo linafanikiwa kwa azma ya kumuenzi Hayati Rais Magufuli. 

Viongozi mbali mbali walipata fursa ya kumueleza Hayati Magufuli kwa mazuri yote aliyowafanyia wananchi wa Tanzania ambapo Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Ali Hassan Mwinyi walimuelezea Rais Magufuli jinsi alivyokuwa shujaa na alivyowapenda Watanzania sambamba na alivyotekeleza miradi ya maendeleo.

Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete alieleza kwamba Rais Hayati Magufuli alimuamini na alikuwa ni jembe lake wakati wa uongozi wake na ndio maana alimteua kuwa Waziri katika Wizara tatu tofauti katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake huku akitumia fursa hiyo kumuhakikishia mashirikiano makubwa Rais Samia kutoka kwa Marais Wastaafu.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi alimuelezea Rais Magufuli kwamba alikuwa mtetezi wa wanyonge na kueleza jinsi alivyowasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu Wamachinga, alivyojenga miundombinu ya barabara, alivyonunua ndege pamoja na kutekeleza vyema uongozi wake uliotukuka.

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein alimuelezea Rais Magufuli jinsi alivyokuwa shujaa na jinsi alivyofanya mambo yake kwa kutomuogopa mtu na badala yake alimuongoza zaidi Mwenyezi Mungu pekee.

Philip Mangula Makamo Mwenyekiti wa CCM Bara, alimuelezea Rais Magufuli jinsi alivyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na kueleza jinsi alivyokitendea haki chama chake cha CCM pamoja na wanachama wake huku akieleza matumaini yake makubwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Viongozi wa dini nao walipata nafasi ya kutoa pole kwa kifo cha Rais Magufuli ambapo Mufti Mkuu wa Tanzania alieleza jinsi Rais Magufuli alivyotoa mashirikiano kwa dini zote bila ya ubaguzi huku Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) likisema kuwa litashirikiana vyema na Rais Samia katika kutekeleza majukumu ya kuliongoza Taifa.

Mkuu wa Majeshi nchini Tanzania, Venance Mabeyo amemuhakikishia Rais wa  Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama vitamtii na kutekeleza majukumu yake kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nae Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amemkaribisha Bungeni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan huku akimhakikishia ushirikiano na Wabunge kwa ajili ya kuleta maendeleo ndani ya nchi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.