Habari za Punde

Somo la historia ya Tanzania kusomeshwa Maskulini Zanzibar

 Na Maulid Yussuf WEMA

UNGUJA
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema itatekeleza agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mhe Dk John Pombe Magufuli la kuwataka kusomesha somo la historia ya Tanzania katika maskuli katika ngazi zote.

Akizungumza wakati akifungua kongamano la siku moja kujadili historia hiyo katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Kiembesamaki,  katibu Mkuu wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar bwana Ali Khamis  Juma amesema  agizo hilo wametakiwa kulitekeleza mapema mwakani, hivyo amewataka wadau kufanya haraka kujadili suala hilo ili liweze kutekelezeka kwa muda uliopangwa.

Amesema Wadau wote wa Elimu watambue kuwa wana jukumu kubwa katika kuhakikisha watoto wanafaulu vyema masomo yao, kwani watoto wamekuwa wakifeli, hivyo endapo hawataojipanga vizuri katika kuchambua vyema somo hilo, idadi ya kufeli kwa watoto itaongezeka kutokana na kuongezeka kwa masomo.

Aidha amewataka walimu kutokuwa wavivu kuusoma mtaala huo wa somo hilo la Historia ya Tanzania ili kwenda sambamba na walimu wa Tanzania bara kwa kuleta ushindani katika ufaulu.

Hata hivyo ameitaka Taasisi ya Elimu kutoweka upendeleo kwa walimu katika kuwapatia elimu kwa kuwaangalia zaidi wenye vigezo kupitia somo hilo.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Zanzibar, mwalimu Suleiman Yahya Ame amesema Taasisi ya Elimu baada ya kupata agizo hilo, imeamua kuanza kufanya mapitio ya mtaala wa somo hilo ili kuwafikishia wadau mihutasari ya somo hilo  na kuweza kutoa maoni yao ili kuweza kusaidia kupata mtaala sahihi kwa maendeleo ya Taifa.

Amesema suala la usomeshaji wa somo hilo, Zanzibar itafaidika sana kwani tayari Taasisi hiyo imeshaanza  kufanya mapitio ya mtaala wake wa Elimu ya Maandalizi na msingi ikiwemo kuliingiza na  somo hilo.

Aidha amewataka wadau hao kutoa maoni yao kwa kuangalia masuala ya msingi ili kuepusha somo hilo kuwa na mambo mengi yatakayofanya kuwa mrundikano wa masomo mengi watoto.

Amesema somo la (history) la zamani litakuwepo kama kawaida katika lugha yake ya kiengereza, na somo la historia ya Tazanzia litakuwepo kama ni somo maalumu ambalo litafundishwa wa lugha ya kiswahili na mtihani wake utakuwa ni kwa lugha ya kiswahili.

Amesema kuingizwa kwa somo la Historia ya Tanzania ndani ya Mtaala wa elimu, hauendani na Sera ya Elimu ya Zanzibar Bali linaendana na Katiba ya nchi, hivyo amewataka wadau hao wa Elimu kutokuwa na wasiwasi juu ya kuingizwa somo hilo katika mtaala kwa kuangalia Sera ya Elimu ya Zanzibar.

Akiwasilisha rasimu za mihutasari, Meneja mitaala na vifaa kutoka Taasisi ya Elimu Zanzibar mwalimu Abdullah Mohammed Mussa amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeona ipo haja ya kusomeshwa somo la historia ya Tanzanzia katika Skuli ili kuwasaidia watoto kuijua historia ya nchi yao.

Amesema ipo haja kwa Taasisi kutafuta mabalozi ambao wanaijua historia ya nchi na uzalendo kwa kupata misingi ha maendeleo kwa watoto wao.

Aidha amefahamisha kuwa Taasisi ya Elimu imeona haja ya kufanya mapitio ya mtaala wa Elimu na kuliingiza somo hilo katika mtaala wake ili kusaidia kutambulika na jamii na hasa watoto ambao ndio tegemeo la Taifa.

Nao washiriki wa Kongamano hilo wamesema wamelipokea somo hilo sambamba na kushauri kuwekwa mazingatio ya hali ya juu katika ufudishaji wa somo hilo kwa kuwekwa mpangilio mzuri wa somo (sylabus) ili kuepuka kusomeshwa kwa kila mwalimu kusomesha anavyotaka na kufanya lengo lisifikiwe.

Wamesema somo hilo linatakiwa lisomeshwe kwa kishwahili lakini Skuli za binafsi zinasomesha Wanafunzi wao kwa lugha ya kiengereza,  hivyo wameomba kuwa somo hilo mtihani wake uwe kwa lugha ya kiengereza.

Hata hivyo wameshauri kuhakikisha kunapatika vitabu vya kufundishia kwa walimu na vya kusomea kwa wanafunzi ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa vitabu katika somo hilo.

Akitoa shukurani zake, AFISA Elimu mkoa wa Mjini Magharibi  Mohamed Abdallah Mohamed kwa niaba ya washiriki wenziwe ameishukuru Wizara ya Elimu kupitia Taasisi hiyo kwa kuamua kuanza kutekeleza agizo hilo ambapo amesema itaweza kusaidia kuwaweka wananchi na vijana kwa ujumla kuwa wazaendo zaidi kwa nchi yao.

Kongamano hilo la siku moja limewashirikisha maafisa Elimu Mkoa, Wilaya, Wasaidizi Wakurugenzi Elimu, Washauri wa masomo ya Historia pamoja na washiriki kutoka Skuli binafsi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.