Habari za Punde

Waziri Kabudi na Waziri Mambo ya Nje wa Burundi Albert Shingiro, TPA-Burundi Yaipongeza Tanzania Kuboresha Bandari.

Na Mwandishi wetu ,  Kigoma

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Balozi Albert Shingiro, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanya maboresho makubwa ya miundombinu ya Bandari na reli ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo baina ya nchi hizo. 

Shigiro na ujumbe kutoka Burundi jana walifanya ziara katika Bandari ya Kigoma na kujionea miundombinu ya bandari hiyo kikiwemo kituo cha Bandari Kavu ya Katosho na gati ya mizigo na abiria katika bandari ya Kigoma, mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Tume ya Pamoja ya kudumu baina ya nchi hizo. 

"Tumefurahi sana kuja kutembelea bandari hii tunaipongeza Serikali na uongozi wa bandari hii kwa kazi kubwa walioifanya kuboresha miundombinu. Hii itawapa urahisi wafanyabiashara wetu na kupunguza gharama za usafirishaji na bei ya bidhaa, " alisema Balozi Shigori. 

"Burundi tutaendelea kutumia bandari za Kigoma na sasa tunapata urahisi kwa kuwa tuna njia mbili moja ya nchi kavu kupeleka mizigo mikoani na njia ya maji kwenda Bujumbura," alisema. 

Kwa uoande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,  Mhandisi Leonard Chamurio, alisema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya bandari sambamba na reli na meli ili kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini. 

Alisema katika kuboresha mazingira ya usafirishaji Serikali ina mkakati wa kuongeza meli kwa kukarabati meli za MT Sangara,  MV Liemba na MV Mwongozo ambazo alisema kufikia mwakani zote zitakuwa zinafanya kazi. 

Aidha alisema Serikali pia ipo kwenye mchakato wa ujenzi wa meli kubwa ya tani 4000 katika ziwa Tanganyika. 

"Nawashauri wenzetu wa Burundi waendeles  kuitumia bandari hii na bandari zingine kupitisha mizigo yenu kwani asilimia 99 ya mizigo yenu inapita hapa kwa usalama," alisema. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema wazo la ujenzi wa bandari za Kigoma lilitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za bandari kutokana na miundombinu iliyokuwepo kuwa haitoshelezi mahitaji. 

Alisema kutokana na mahitaji hayo walikuja na wazo la kujenga bandari kavu ya Katosho kwaajili ya kujudumia mizigo inayotoka na kuingia nchini kwa njia ya barabara. 

Alisema mradi huo umenza kwa kulipa fidia ya eneo na kuzungusha ukuta na ujenzi awamu ya kwanza utaanza kwa kujenga mita za mraba 40,000, eneo la kuegesha malori 100 na ofisi za awali. 

"Tunatarajia mradi utakamilika Juni mwakani kwasababu unatarajia kuanza Aprili mwaka huu," alisema. 

Aliongeza kuwa Bandari Kavu hiyo pia itaunganishwa na reli katika awamu ya pili ya ujenzi ili kuweza kuingiza mizigo moja kwa moja katika bandari hiyo kwa njia treni. 

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi ya Bandari ya Kigoma Kaimu Meneja wa Bandari hiyo, Nyoni alisema maboresho ya bandari zake yamesaidia kuongeza shehena kutoka tani 139,317 mwaka 2015/16 hadi tani 680,000 mwaka 2018/19 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 10 kwa mwaka.

Alisema maboresho mengine yanaendelea kuboresha zaidi ikiwemo ujenzi wa kituo cha kibirizi unaohusisha ujenzi wa gati, ofisi,  jengo la abiria na maghala matatu. 

Aidha alisema kuna ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya bandari za kigoma ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 85.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.