Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Azungumza na Mwenyekiti wa Tume ya Haki Za Binaadam Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Jaji Mstaafu Methew Mwaimu alipofika Ofisini kwake Vuga Zanzibar kwa mazungumzo leo, akieleza majukumu ya Taasisi yake katika kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Mheshimiwa Hemed na baadhi ya Wajumbe wa Tume ya Haki za Binaadamu wakimsikiliza Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Methew Mwaimu hayupo pichani.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti kutoa ushirikiano kwa taasisi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha wanakaa pamoja ili kujadili mustakbali wa maendeleo kwa pande zote mbili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, ameyasema hayo alipokutana na uongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, walipofika Ofisini kwake Vuga kujitambulisha.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo wazi kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, juu ya kuzidisha mashirikiano kupitia vikao vya pamoja katika kujadilii masuala mbali mbali.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed, ameongeza kuwa serikali iko tayari kusaidia Watendaji wa Tume hiyo pale watapohitaji msaada ili kuwawezesha watanzania kupata haki zao stahiki katika Tume hiyo.

Akizungumza kuhusiana  na suala la ajira Mheshimiwa Hemed amesema kuwa, serikali itazingatia kufuatwa kwa taratibu, ili kuweza kutoa ajira pande zote mbili za muungano.

Ameushukuru Uongozi wa Tume hiyo kwa utekelezaji wa majukumu yake na kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr Hussein Ali Mwinyi, imejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanafaidika na matunda ya serikali yao.


Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Jaji Mstaafu Methew Mwaimu alisema ujio wao umelenga kuongeza ushirikiano wa karibu kwa vile  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na ile ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndizo               zinazoratibu masuala ya Muungano.                                                                                                        

Ameendelea kueleza kuwa Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania ina wajibu wa kusimamia haki za Kijamii nchini, ili kuongeza kasi ya maendeleo.

Aidha Mwenyekiti huyo, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanza vizuri Awamu ya Nane, jambo ambalo limepelekea kuongezeka Imani ya wananchi kwa serikali yao, namna inavyojitoa katika kusaidia wananchi wa Zanzibar.

Tume ya Haki za Binadamu yenye Makao Makuu yake jijini Dodoma, ikiwa pia na Ofisi yake Zanzibar, na matawi mengine katika maeneo mbali mbali ikiwemo Pemba, Lindi, Mwanza na Dar -es- salaam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.