Habari za Punde

Mrajisi wa Asasi Zisizo za Kiraia Atembelea wa Viongo, Mbogamboga na Matunda Pemba.

Afisa kilimo anayeshughulika na mboga kanda ya Pemba,  Sada Juma Segeja, (kushoto) akitoa maelezo kwa mrajisi wa asasi zisizo za kiserikali wakati wa ziara.


MRAJISI wa asasi zisizo za kiserikali Zanzibar, Ahmed Khalid Abdalla, amewataka wakulima kisiwani Pemba kuchangamkia fursa za uwepo wa mradi wa  Viungo, Mboga na Matunda Zanzibar ili uwasaidie kujikwamua kiuchumi kupitia uzalishaji wa mazao hayo.

Mrajisi ametoa wito huo wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo ya shamba darasa yaliyotengwa kwaajili ya kuwafundishia wakulima wanufaika wa mradi huko katika Shehia za Ole na Mjini Ole Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema Serikali inamatumaini makubwa na utekelezaji wa mradi huo kwa wakulima Zanzibar kwani unalenga kuwakomboa wakulima wa mazao hayo kwa kukuza uchumi pamoja na upatikanaji wa chakula majumbani.

“Serikali inaridhishwa sana na mradi huu kwani ni mradi ambao umekuja kuisaidia serikali kuwainua wakulima wetu kupitia shughuli hizi za kilimo ambacho mradi unafanyia kazi. Nikuombeni endeleeni kuchangamkia fursa hii kwa kutumia taaluma mnayoipata kila siku kutoka kwa wataalam huku mkitambua kwamba serikali inaungana nayi katika kila hatua,” alisema.

Aliwataka wakulima kutokatishwa tamaa na changamoto zinazowakabili katika hatua ya awali na badala yake kufanyakazi kwa karibu na wataalam wa kilimo ili kuzitaftia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza.

“Naomba tusivunjike moyo, tuendelee tuwe na ari ya kufanya kazi. Nafahamu mwanzo ni mgumu lakini tunatakiwa tushirikiane na tupokee yale tunayoelekezwa na wataalam wetu wa kilimo. Najua kwenye jamii wapo baadhi ya watu watakao wabeza kwa juhudi zenu, lakini fanyeni malengo yenu yaliyokusudiwa na mradi huu hatimaye mtakuja kuona faida yake,” alisema.

Katika hatua nyingine Ahmed alisema ufanisi wa utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) utaisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi kufanikisha kutekeleza ahadi yake ya upatikanaji wa ajira laki tatu Zanzibar.

Alisema, “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, imezungumzia suala la ajira laki tatu. Nimearifiwa kwamba mradi huu ukikamilika karibu ajira 21,000 zinaweza kupatikana, sasa ajira hizi zikipatikana maana yake lengo la Serikali kuongeza fursa za ajira limetekelezeka.”

Meneja wa mradi huo, Amina Ussi Khamis alisema ziara hiyo imelenga kukagua maendeleo ya uandaaji wa shamba darasa na kubaini changamoto zinazowakabili wakulima katika uandaaji wa maashamba hayo wakati ambapo wakulima wanaendelea na zoezi la uandaaji wa mashamba yao kwaajili ya upandaji wa mazao.

Alisema, “leo tumekuja hapa kwa lengo la kuangalia maendeleo yetu ya maandalizi ya shamba darasa ili tuweze kujua kila hatua ambayo tumeifikia katika utekelezaji wa mradi wetu wa Viungo.”

Mapema akitoa maelezo wakati wa ziara hiyo, afisa kilimo anayeshughulika na mboga kanda ya Pemba,  Sada Juma Segeja, alisema taaluma inayotolewa na wataalam wa kilimo kupitia Shamba darasa zilizoandaliwa katika Shehia ambazo mradi unatekelezwa itasaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao na kufanikisha kwa haraka ufikiaji wa malengo ya mradi.

Wakulima kupitia mradi huo wameshukuru uwepo wa mradi kutokana na taaluma wanayoipata kupitia shamba darasa imewawezesha kila mkulima kuanza maandalizi ya shamba lake kwaajili ya uzalishaji.

Ziara hiyo ya Mrajisi wa asasi zisizo za kiserikali Zanzibar ni  mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa Viungo, Mboga na Matunda unatekelezwa Zanzibar na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania, Zanzibar, (TAMWA ZNZ), People’s Development Forums, (PDF) na Community Forests Pemba (CFP) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).

Meneja wa mradi huo, Amina Ussi Khamis (kushoto), mrajisi wa asasi zisizo za kiserikali Zanzibar, Ahmed Khalid Abdalla(katikati) na meneja uendeshaji wa mradi wa VIUNGO kanda ya Pemba Sharif Maalim Hamad (kulia) wakiwa shambani wakati wa ziara.
 MRAJISI wa asasi zisizo za kiserikali Zanzibar, Ahmed Khalid Abdalla akitoa maelekezo kwa wakulima.
Meneja wa mradi wa VIUNGO, Amina Ussi Khamis akizungumza wakati wa ziara.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.