Habari za Punde

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Wajane Zanzibar (ZAWIO) Bi. Tabia Makame Mohammed,(kulia kwa Rais) wakati walipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi  ya Wajane Zanzibar.(ZAWIO) Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Mgeni Hassan Juma, wakati wa mkutano wake na Uongozi wa Taasisi hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar na (kulia kwa Rais) Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Bi. Tabia Makame Mohammed.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Taasisi ya Wajane Zanzibar (ZAWIO) ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo ambae pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Mgeni Hassan Juma na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Bi. Tabia Makame Mohammed, mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza haja ya kurekebishwa Sheria kandamizi ambazo zimekuwa zikiwakosesha haki zao za msingi wanawake wajane hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya  mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Wanawake Wajane Zanzibar (ZAWIO), walipofika Ikulu Jijini Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema kwa Jumuiya hiyo kuwa na mapendekezo yatakayosaidia kubadilisha Sheria ili kuondosha mapungufu yaliopo katika jamii ambayo yamekuwa yakiwasibu wanwake wajane. 

Alisema kwamba si jambo la busara mwanamke kuachwa katika ndoa na kuachiwa watoto akihangaika nao bila ya kupewa msaada wowote wa kukidhi maisha yake.

Alisisitiza kwamba wapo wanawake ambao huchuma mali na wenza wao na mara wanapoachana hawaambulii chochote jambo ambalo alisema si busara licha ya baadhi ya wanaume kutoa visingizio vya kidini jambo ambalo si sahihi.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba yuko tayari kutekeleza mabadiliko ya Sheria ili  sheria zisikandamize upande mmoja.

Rais Dk. Mwinyi ameipongeza Jumuiya hiyo ya Wanawake Wajane Zanzibar (ZAWIO) kwa kazi nzuri ya kujitolea katika kuwasaidia Wajane katika jamii Unguja na Pemba.

Alifahamisha kwamba kazi wanayoifanya viongozi wa Jumuiya hiyo malipo yake yanatoka kwa MwenyeziMungu kwani ni kazi kubwa na inahitaji moyo.

Kutokana na juhudi hizo, Rais Dk. Mwinyi ametoa jumla ya TZS Milioni kumi kwa ajili ya kuendesha ofisi ya Jumuiya hiyo pamoja na vyakula vya futari kwa ajili ya Wajane 300 wenye mazingira magumu zaidi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali itahakikisha inaiunga mkono Jumuiya za Jumuiya ya (ZAWIO) katika kufikia malengo yake na kusisitiza kwamba yapo mambo matatu makubwa ambayo yanahitajika katika kuimarisha Jumuiya hiyo ikiwemo soko, mtaji na elimu ya ujasiriamali.

Alisisitiza kwamba ni vyema Jumuiya hiyo ikahakikisha katika juhudi zake za kuwakwamua wajane na changamoto walizonazo kwa wale watakaozalisha bidhaa wakahakikishawanafanya utafiti wa soko la kuuza bidhaa zao wanazozitengeneza.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuiunganisha Mifuko yake yote ili iwe rahisi kuyashughulikia makundi yanayohitaji huduma kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.

Alisisitiza kwamba tayari Serikali inalisimamia jambo hilo huku taasisi binafsi zikiwemo Benki ambazo zimeanza kuunga mkono juhudi hizo ikiwemo benki ya CRDB ikiisaidia Jumuiya hiyo.

Rais Dk. Mwinyi aliipongeza Jumuya hiyo kwa kuanza kuzalisha baadhi ya bidhaa sambamba na kuwa na lengo la kuanzisha viwanda vidogo vidogo huku akisisitiza kwamba tatizo si fedha bali ni kuwepo kwa soko,utendaji na elimu.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya (ZAWIO) Mgeni Hassan Juma alieleza juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya hiyo huku akiahidi kuhakikisha kwamba marekebisho ya Sheria husika yanatekelezwa katika Baraza la Wawakilishi.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ambaye pia, ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuiunga mkono Jumuiya hiyo huku akimpongeza Mama Mariam Mwinyi kwa kuilea na kuisaidia.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Wajane Zanzibar (ZAWIO), Tabia Makame Mohamed alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuijali na kuiunga mkono Jumuiya hiyo pamoja na kuthamini juhudi zake.

Mkurugenzi huyo pia, alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio na changamoto za Jumuiya hiyo iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Asasi za Kiraia Zanzibar ya mwaka 1995, ambayo imejikita katika kuwasaidia wajane wa Zanzibar ambayo ilisajiliwa rasmi Disemba 12, 2019.

Alisema kuwa Zanzibar hivi sasa kuna wajane wapatao 16,000 Unguja na Pemba idadi ambayo ni kubwa na imekuwa ikiongezeka kila siku.

Katika maelezo yake Mkurugenzi huyo wa (ZAWIO) alisema kuwa Jumuiya hiyo ina waratibu Unguja na Pemba na imekuwa ikiwafunza wanawake wajane katika kuwapa elimu ya ujasiriamali.

Aidha, alieleza kwamba tayari wanawake hao wajane wamekuwa wakizalisha bidhaa mbali mbali kutokana na michango yao wenyewe wanayoifanya na kugawana kupitia vikundi vyao kila wanapokutana Jumamosi ya mwisho wa wiki.

Alizitaja baadhi ya bidhaa wanazotengeneza kuwa ni sabuni, vikoi, udi na bidhaa nyenginezo.

Pamoja na hayo, alieleza juhudi zinazofanywa na Jumuiya hiyo katika kuwaendeleza wanawake wajane ambapo hivi sasa wanampango wa kuwasomesha udereva wajane 10 baada ya kupata ufadhili wa masomo ya udeva kutoka kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar pamoja na kuanzisha mkahawa wa vyakula vya asili huko Matemwe.

Nao viongozi wengine wa Jumuiya hiyo walieleza haja ya kuondoshwa kwa sheria kandamizi ambazo haziwatendei haki huku wakimpongeza Mama Mariam Mwinyi kwa juhudi zake za kuwasaidia kuwaunganisha na Benki ya CRDB ambayo imekuwa ikiwasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuendesha shughuli zao.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.