Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ameeleza Umuhimu wa Kuwasaidia Walimu wa Madrasa na Kuwachangia Kwa Hiari.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza umuhimu wa kuwasaidia walimu wa madrasa na kuwachangia kwa hiari bila ya kusubiri kuombwa au kushurutishwa.

Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo huko katika uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar katika hafla ya mashindano ya kuhifadhi Kur-an Kitaifa  yaliyoandaliwa na Taasisi ya Maahil Irfaan kutoka Dar-es-Salaam na Taasisi ya kuhifadhisha Kurani Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini na Serikali kutoka Zanzibar na Tanzania Bara akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Mawaziri pamoja na wananchi mbali mbali.

Katika hotuba yake, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema Wazazi wakaona kazi kubwa na ngumu inayofanywa na walimu wa madrasa ya kuwasomesha na kuwalea watoto na wawe tayari kuchangia kwa hiari bila kusubiri kushurutishwa.

Alisema kuwa katika mfumo wa maisha ya zamani ambao bado unaendelea katika sehemu zote za Unguja na Pemba walimu wa madrsa walijitewezesha wenyewe lakini katika uhalisia wa maisha ya sasa jambo hilo ni gumu hasa ikizingatiwa idadi ya wanafunzi katika madrsa imeongezeka.

Aliongeza kuwa walimu wanahitaji muda zaidi wa kuwasomesha na kuwasimamia wanafunzi wakati wa kudurusu hivyo ni vyema wema na ihsani hiyo ya kujenga utamaduni wa kupenda kuchangia madrasa ukathaminiwa.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa bado hakujawa na mfumo rasmi wa kuwatambua na kuwasaidia walimu wa madrasa hapa Zanzibar.

Aliendelea kufahamisha kwamba baadhi ya walimu wa madrasa hasa katika sehemu za shamba wanaosomesha watoto wanaishi katika mazingira magumu kutokana na hali ya maisha kwani wanafanya kazi ya kujitolea wakitegemea malipo kwa MwenyeziMungu.

Katika hotuba yake hiyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba wazazi na walezi wana jukumu la kuzijenga na kuziimarisha madrasa badala ya kuona kwamba suala la ujenzi wa madrasa na kuwasaidia walimu ni jukumu la wafadhili kutoka nje.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa juhudi hizo za kuwafundisha watoto kuhifadhi Kurani ni vizuri zikaenda sambamba na juhudi za kuwafundisha tafsiri ya Kurani, ili kuwajengea misingi imara na kuimarisha imani ya uchamungu.

Alhaj Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuishi kwa kupendana na kuheshimiana ili Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla ibaki kuwa mfano wa nchi zenye hali kubwa ya usalama duniani.

Aliwahimiza walimu wa madrasa kuendelea kushirikiana vizuri na wazee pamoja na Serikali katika kuwaandaa vizuri watoto kwa kuwapa elimu na malezi bora kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa Kizanzibari.

Alisisitiza haja ya kuwalinda vizuri watoto na vitendo vinavyoweza kuathiri maisha yao ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika kupiga vita vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa watoto.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba moja kati ya mambo yaliyohimizwa kufanywa katika Uislamu kwenye kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kukithirisha kuisoma Kurani Tukufu.

Aliipongeza Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar, Taasisi ya Manaahil Irfaan kutoka Dar-es-Salaam na Taasisi ya Kuhifadhisa Kuarni Zanzibar kwa kushirikiana katika kuandaa mashindano hayo makubwa ya kihistoria hapa Zanzibar.

Pia, Alhaj Dk. Mwinyi aliipongeza Benki ya Watu ya Zanzibar (PBZ) na mfanyakazi wa Zenjibar TV Online, Salum Mardhia kwa kutoa zawadi za washindi wa mashidano hayo.

Alisema kuwa mashindano ya Kurani popote yanapofanyika huwa yanadhihirisha uwezo mkubwa wa akili ya mwanaadamu katika kuweka kumbukumbu na kuhifadhi mambo muhimu kwa maisha yake.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa washiriki wote kwa kuonesha vipaji tofauti baadhi yao wakiwa wadogo sana hivyo, mashindano hayoyanatoa mafunzo kwamba akili ya mwanaadamu ina uwezo mkubwa usiomithilika katika kujifunza mambo muhimu katika maisha.

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa zawadi ya TZS Milioni moja kwa kila mshiriki wa juzuu 30 kwa wale wote ambao hawakupata zawadi za ushindi.

Nae Mratibu wa Mashindano hayo ya 12 ambayo ni ya kwanza kufanyika hapa Zanzibar ambae pia, ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam Sheikh Alhad Mussa Salim alitoa pongezi kwa wale wote waliojitolea kutoa zawadi kwa washindi.

Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa upande wake alitoa shukrani kwa kufanyika mashindano hayo hapa Zanzibar kwani ni kitovu cha elimu ya Uislamuhuku akitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kusoma dua misikitini kwa ajili ya kukitokomeza kimbunga kinachotarajiwa kutokea.

Nae Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Mfaume alitumia fursa hiyo kwa kuwataka walimu wote wa madrasa za Unguja na Pemba kuzifunga madarsa zao kwa siku ya kesho na keshokutwa ili kuhakikisha watoto wote wanabakia majumbani.

Mapema katika risala yao  Taasisi ya  Maahil Irfaan kutoka Dar-es-Salaam ilieleza mafanikio waliyoyapata mapoja na changamoto walizonazo ambapo pia, ilieleza utaratibu mzima wa mashindano hayo ulivyofanyika tokea yalipoanza mnamo Januari 17 mwaka huu 2021.

Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza kwa Juzuu 30 ni Yunuss Masoud Mwaboko kutoka Kenya ambaye amezawadiwa TZS milioni 10, mshindi wa pili ni Ayoub Hassan Ali kutoka Somali amezawadiwa TZS Milioni7 na mshindi wa tatu ni Mbarouk Othman Ali kutoka Zanzibar ambaye amepata TZS milioni 4.

Kwa upande wa Juzuu 20 mshindi wa kwanza ni Biubwa Mbwana Hamad kutoka Darajabovu Zanzibar ambaye amepata zawadi ya TZS Milioni 3 na Juzuu saba mshindi ni Imran Ali kutoka Zanzibar aliepata zawadi ya TZS milioni moja na Juzuu tatu mshindi ni Nasra Idd kutoka Barabara ya 16 Tanga aliyepata TZS laki 7.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.