Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amewaapisha Makamanda wa Vikosi vya SMZ Aliowachagua Hivi Karibuni na Kuivunja Bodi ya ZSSF.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wakuu wa Idara Maalum za SMZ baada ya kuwaapisha katika ukumbi wa Ikulu Jijini  Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Makamanda wapya aliowateua kuwa Wakuu wa Vikosi Maalum vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,waende wakajenge na kurudisha nidhamu katika vikosi hivyo.

Hafla hiyo ilifanyika Ikulu Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais Othman Masoud, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Othman Makungu, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa dini, watendaji wa Serikali na wanafamilia.

Alisema kwamba Jeshi ni nidhamu na ikikosekana nidhamu hakuna Jeshi, hivyo,   nidhamu ilitetereka katika vikosi na ndipo alipoamua kuwachangua Makamanda hao ili walete uzoefu wao wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa aliona haja na sababu ya kuwatumia Maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania ili waweze kuiweka nidhamu katika vikosi vya SMZ.

Pia, Rais Dk. Mwinyi aliwataka kwenda kusimamia rasilimali zilizopo katika vikosi hivyo na taasisi walizopewa dhamana kwani kuna ubadhirifu mkubwa, wizi na mambo mengine ambayo hayapaswi kufanywa.

Alisema kuwa Serikali imegundua kwamba wahasibu katika vikosi hivyo wanalipa mishahara ya watu ambao hawapo, wahasibu wanakata  posho za askari ambapo pia,  wanalipa mpaka watu ambao tayari washastaafu.

Alisema kwamba yeye mwenyewe amethibitisha hayo kwani hana nia ya kumuonea mtu, hivyo aliwataka wakuu hao wapya wa vikosi vya SMZ kuhakikisha wahasibu hawafanyi vitendo hivyo na kutaka yale mambo yasiofaa yote yawe basi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba maduka ya vikosi yalikuwa yakitumika vibaya ambapo  wahasibu hao walikuwa wakichukua mishahara ya askari kwa kisingizio cha makato ili ionekani walikuwa wamekopa halafu fedha zilikuwa zinakwenda kuchukuliwa madukani.

Alisema kwamba maduka hayo yanadhamira njema ya kuwasaidia maafisa na askari na isiwe vichochoro vya kupitisha fedha haramu.

Katika suala zima la uzalishaji mali, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa wakati wa amani kazi ya vikosi vya ulinzi ni mafunzo na uzalishaji mali na kuvitaka vikosi hivyo vikajipange kupunguza ruzuku inayotoka Serikalini.

Hivyo, alivitaka vikosi kupunguza fedha zinazotoka Serikali zinazokwenda kwenye vikosi, ambapo awamu ya pili iwe kuondokana na ruzuku kwa kujitegemea na kutoa gawiwo kwa Serikali kwani vikosi hivyo vina fusra za kuzalisha mali.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba ndani ya vikosi kuna viwanda, kampuni ya ulinzi, mashamba, maeneo yanayofaa kwa utalii pamoja na chelezo na kueleza kwamba ipo haja ya chelezo kutumika kibiashara na kutaka kuhudumia meli mbali mbali zikiwemo zile za Zanzibar na nje ya Zanzibar.

Alivitaka vikosi kuingia kwenye ubia na watu wenye uwezo, alitaka mashamba yazalishe hasa ikizingatiwa kuwa uwezo huo upo na kutaka vikosi kuzalisha mali ili serikali ipunguze mzigo wa kubeba vikosi hivyo, huku akisisitiza kupatikana kwa haki kwa askari na maafisa sambamba na kupata stahili zao kwa wakati.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba sio kama anapenda kufukuza watu wala hana nia ya kutafuta mchawi wala hana nia ya kufufua makaburi lakini pale mtu anapokuwa mbadhirifu, wizi wa mali ya umma wa fedha za Serikali hatonyamaza kimya na hilo litaendelea mpaka mambo hayo yakome.

Alisema kwamba ndio kwanza anaanza na nguvu bado hazijesha na kutoa mfano pale alipoivunja Bodi ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), kutokana na ubadhirifu na kutoa angalizo kwa wengine.

Rais Dk. Mwinyi alishangazwa na Bodi ya ZSSF kwa kufanya ubadhirifu na kusema kwamba kuanzia Januari hadi Machi Bodi hiyo imefanya vikao zaidi ya sita ndani ya miezi mitatu ambapo fedha zilizotumika ni TZS Milioni 99.7

“Najiuliza kulikuwa na dharura gani ya kufanya vikao sita ndani ya miezi mitatu.....kwa kawaida Bodi zinatakiwa kufanya vikao vinne kwa mwaka na ikitokea kuna dharura ndio wanaweza kukutana zaidi ya hapo lakini kuwe na dharura”, alisema Rais Dk. Mwinyi.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliivunja Bodi hiyo na kusema kwamba hatosita wala kusimama kuvunja Bodi mpaka ubadhirifu wote uondoke.

Aidha, alisema kwamba wakati Serikali inajenga wapo watu wanaobomoa, na kusema kwamba wanaobomoa wakiwemo ndani ya Serikali na Taasisi nyengine mafanikio hayatopatikana na yeye ataendelea kupambana nao.

Rais Dk. Mwinyi alitoa onyo kwa wengine na kusema kwamba yapo Mashirika ya Serikali hapa Zanzibar ambayo yanayopata faida ni machache sana na karibu yote ni hasara hivyo haiwezekani kuendelea na Bodi zenye hasara.

Aliwapongeza Wakuu wote wa Vikosi aliowaapisha hivi leo na kutaka wakafanye kazi kwa bidii na kuwataka askari na Maafisa wote wa vikosi vya SMZ kutokuwa na wasiwasi kwani lengo lake ni kujenga ili vikosi viwe madhubuti, vilivyowezeshwa na kuwa na mafunzo ya kutosha.

Mapema Rais Dk. Mwinyi ambaye pia, ni Mkuu wa Vikosi hivyo kabla ya kuwaapisha Wakuu hao kwa mujibu wa Sheria aliwapaindisha vyeo vya Ukuu wa Vikosi hivyo ya SMZ.

Pia, alitumia fusra hiyo kumshukuru Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Kamanda Simon Siro kwa kukubali pendekezo lake la kuwateua Makamanda hao na kusisitiza kwamba yeye alikuwa na lengo la kutafuta viongozi na sio wataalamu kwani anachotaka ni viongozi na si fani zao.

Walioapishwa katika hafla hiyo ni Kanali Azana Hassan Msingiri kuwa Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), Kanali Makame Abdallah Daima kuwa Mkuu wa Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kanali Rashid Mzee Abdallah kuwa Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Ukozi.

Wengine ni Luteni Kanali Khamis Bakari Khamis kuwa Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo, Luteni Kanali Burhani Zubeir Nassoro kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Uratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya pamoja na ACP Ahmed Hamis Makarani kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA).

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.