Habari za Punde

Serikali Yatoa Tamko Kuhusiana na Kampuni ya Masterlife Microfinance Ltd Ikijihushisha na Shughuli za Kifedha Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar wakati akitowa taarifa ya Serikali kuhusiana na Kampuni ya Masterlife Microfinince Ltd, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.  

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali          Mwinyi amesema serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha inapata fedha zilioko mikononi mwa Kampuni ya Masterlife Microfinance Ltd ili hatimae zirudi            mikononi mwa wananchi waliowekeza .                                                                          

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokuwa akitoa taarifa ya Serikali, kuhusiana na shughuli zilizokuwa zikifanywa na Kampuni ya Masterlife Microfance Ltd hapa Zanzibar, kwa waandishi wa habari.

Amesema Kampuni ya Masterlife Microfanance Ltd iliosajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Tanzania Bara pamoja na Bodi ya Mapato Tanzania (TRA), haikutekeleza majukumu yake  ya kufuga wanyama na kusindika vyakula kwa mujibu wa usajili na badala yake iliendesha shughuli za kukusanya Fedha kwa wananchi..

Alisema uchunguzi uliofanywa na taasisi zinazohusiana na uendeshaji wa biashara za kifedha, umebaini Kamapuni hiyo haikuwa na biashara inayotoa faida na badala yake ilikuwa ikizungusha fedha hizo miongoni mwa wateja wake.

Alisema kutokana na utaratibu huo idadi ya wanachama iliongezeka kutokana na shauku ya kupata faida kubwa waliyopewa watu waliowekeza mwanzoni, hatua inayofanya kiwango cha fedha kinachohitaji kulipwa kuwa kikubwa kuliko makusanyo.

Alisema Kampuni hiyo imeleta mtafaruku mkubwa kwa wananchi, ikizingatiwa kiwango kikubwa cha fedha za Kitanzania zipatazo Bilioni 38. 5 kilichowekwa na wananchi wanaokadiriwa kufikia 39,000.

“Hali hii imeleta taharuki katika nchi yetu kwa vile wananchi walikuwa na matumaini makubwa na biashara hiyo, kwani baadhi walijiunga kwa kuchukua mikopo mikubwa kutoka Benki ziliopo nchini”, alisema.

Aidha, alisema biashara hiyo haikuwa halali kwa vile fedha zilizowekezwa hazionekani katika Mabenki yalioko nchini.

Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali inaendelea na na uchunguzi wa shauri hilo na pale utakapokamilika italifikisha suala hilo kwenye vyombo vya sheria kwa uamuzi.

Alisema tayari Serikali imezuia jumla ya shilingi Bilioni 4.79 kutoka maeneo mbali mbali yaliowekezwa na mmiliki wa Kampuni hiyo pamoja na mali mbalimbali, ikiwemo magari ya kifahari, bidhaa  na majengo anazomiliki.

Aliwataka wananchi kuwa waangalifu na kuepuka kujiingiza katika biashara za aina hiyo, sambamba na kuwataka kuwa wastahamilivu pamoja na kutoa mashirikiano kwa vyombo vya Dola kadri itakavyohitajika.

Alisema Serikali inaendelea na uchunguzi na ufuatiliaji wa Kampuni na taasisi zinazojishughulisha na biashara zisizofuata taratibu na kusababisha madhara ya kiuchumi kwa Serikali na wananchi wake.

Aidha,alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha haki za wananchi waliowekeza kwa mujibu wa sheria zinalindwa kadri itakavyowezekana kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Mnamo Machi 4, 2021 Serikali ilichukuwa hatua ya kuizuwia Kampuni ya Masterlife Microfanance Ltd kuendelea na shughuli zilizokuwa zikiendeshwa katika maeneo mbali mbali ya nchi kwa kufanya shughuli hizo kinyume na taratibu na sheria za nchi.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.