Habari za Punde

Jamiii yatakiwa kuzingatia malezi bora ya watoto

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiwasalimia Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mtaa wa Magogoni Wilaya ya Magharibi B mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ijumaa wa Taqwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiwasalimia Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mtaa wa Magogoni Wilaya ya Magharibi B mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ijumaa wa Taqwa.


Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kwenye Makaazi ya Yake Bwelezo Wilaya ya Magharibi.

Mh. Hemed alifika nyumbani kwa Mzee Mwinyi kumsalimia baada ya kumaliza Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Taqwa uliopo Mtaa wa Magogoni Amani.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Kassim Salum, OMPR 

Jamii nchini imeshauriwa kuzingatia malezi bora kwa watoto ili kujenga Taifa lenye kuzingatia maadili yanayoonyesha njia ya kupata viongozi bora wa baadae.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, alitoa ushauri huo wakati akisalimia waumini wa Masjid TAQWA uliopo magogoni Wilaya ya Magharibi ‘’B’’  mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Alisema katika jamii ya sasa kumeibuka changamoto kubwa kwa walezi kushindwa kuwasimamia vijana wao kimaadili jambo linapelekea mzigo kwa Serikali kwa kukithiri vijana wanaojiingiza katika vitendo viovu akitolea mfano vitendo vya udhalilishaji na utumiaji wa madawa ya kulevya .

Aidha Makamu wa Pili wa Rais amesema wazazi bado hawajachelewa kuchukua hatua za kuwarekebisha watoto wao kimaadili na watumie fursa hii kwa kumuunga mkono Mhe. Rais Dk. Mwinyi.

“Mhe Rais wetu ni muumini mkubwa katika kuzingatia ukuaji wa maadili kwa vijana wetu, hivyo hakuna budi tuungane nae pamoja katika kufanikisha azma yake hiyo” Alisema Mhe. Hemed.

Akizungumzia juu ya suala la uwajibikaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali ya Awamu ya nane inayoongozwa na Dk Hussein Mwinyi imekusudia kuweka uwazi katika utendaji kazi wa Serikali kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi kwa watumishi wa serikali.

Aliesema kitendo cha ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kusomwa hadharani na wananchi wote kupata taarifa juu ya mambo mbali mbali yanayoendelea nchini ni kiashiria kizuri kwamba Serikali inakusudia kuwatumikia wananchi wake.

Aliendelea kuwakumbusha wananchi kuutumia mfumo wa sema na Rais Mwinyi katika kutuma maoni na changamoto zinazowakabili na Serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo kuzitatua ili wananchi wapate huduma bora kama Serikali ilivyoahidi.

Mhe. Hemed alihitimisha salamu zake kwa kuwataka waumini na wananchi kwa ujumla kuendelea kuienzi na kudumisha amani iliopo kwani Serikali imelipa  kipaumbele jambo hilo kwa umuhimu wake wa kuliletea maendeleo taifa kwa maslahi ya wananchi wake.

“Ndugu zangu waumini niseme tu zipo nchi zimekosa kusali ata hii sala ya Ijumaa kama tulivyosali sisi kutokana na kukosekana kwa amani katika nchi zao” alieleza Makamu wa Pili wa Rais.

Nae Khatibu wa Sala ya Ijumaa Ustadh Hamad Zubeir Hamad katika Khutba yake aliwakumusha waumini kuendeleza umoja na mshikamano kwa kuepuka vitendo vya chuki miongoni mwao ili kufikia lengo la uchamungu kama Allah (S.W) alivyoeleza katika Suratul Al Imran.

Wakati huo huo Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifika Bweleo katika makazi ya Rais Msaatafu  Mzee Ali Hassan Mwinyi kumjuulia hali na kubadiishana nae mawazo.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.