Habari za Punde

Makamu wa kwanza wa Rais Mhe Othman Massoud alikubali kubeba jukumu baada ya ushawishi mkubwa wa viongozi wake wa chama cha ACT


Mjumbe wa kamati kuu wa chama cha ACT wazalendo Othman Masoud Othman amesema alikubali kuchukua nafasi ya makamu  wa kwanza wa Rais kupitia  chama  hicho  baada  ya ushawishi mkubwa viongozi wake.

Aliyaeleza hayo huko Bububu wilaya ya magharibi A (Mkoa wa Magharibi A kichama) wakati akiwa katika muendelezo wa utambulisho wake kwa viongozi wa Mikoa na wafuasi wa chama hicho Visiwani Zanzibar.

Alisema Kabla na baada ya uteuzi viongozi wa chama hicho waliwasiliana naye kuashiria imani waliyonayo katika utendaji wake.

“Lakini Makamu mwenyekiti wa Chama chetu Juma Duni Haji  yeye aliona kunipigia simu nitamdanganya basi akanifata nyumbani, hapo sikuwa na jinsi, nikakubali kuchukuwa nafasi hii ambayo leo ninayo” alieleza Mjumbe huyo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa rais wa Zanzibar.

Alibainisha kuwa chengine kilichomfanya akubali ni dhamira ambayo chama hicho inabeba na kueleza kuwa ni kuleta mabadiliko ya kweli Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake.

“Tunachokipigania ni kuleta Mabadiliko na  kusimamia kuwa na utawala bora ambao ndio misingi bora ya nchi yetu” alisema Othman.

Akifafanua juu ya suala ya utawala bora aliseema ni lazima uwepo wa mahakama huru, tume huru ya uchaguzi pamoja uhuru wa kujieleza,

Alisema dhamira ya ACT ni kuhakikisha unakuwepo uwajibikaji katika kuongoza watu ambao utaleta utawala wa kisheria na kuheshimu matakwa ya wananchi wanaopiga kura.

“Mtu  yoyote anayetetea haki yake au jambo lolote lile basi ni ibada” alisema.

Alieleza Othman akitilia mkazo juu ya masuala ya ushirikiano juu ya masuala ya kisiasa na kijamii.

Kwa upande hamasa na ari ya kukijenga chama  Othman aliwataka wafuasi wa chama hicho kutokurudi nyuma na badala yake waongeze bidii katika mapambano ya kuleta mabadilko Zanzibar.

Aidha mjumbe huyo alisema  kwa dhati ya moyo wake yupo tayari kupigania haki ya wananchi pamoja na chama chake kwa hali yoyote.

Othman ambaye alizaliwa tarehe 7 Februari 1963 na leo kufika umri wa miaka 57 alieleza kuwa kwa umri wake alionao sio umri wa kutafuta kitu kwa maslahi yake pekee na badala yake atapigania haki za wazanzibari mpaka mwisho wa maisha yake.

Akifungua kikao hicho mwenyekiti wa Mkoa wa Magharibi A kichama Bi Raisa Abdallah Mussa alisema alimkaribisha kiongozi huyo na kumuambia kuwa wananchi wote wako nyuma yake kwa maslahi ya Zanzibar na watu wake

Alisema mkoa wa magharibi A kichama ni mkoa ambao uko imara licha ya changamoto mbali mbali unaokabiliwa katika mkoa huo kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.