Habari za Punde

Taasisi, wahisani na wafadhili wenye uwezo kujitokeza na kuwasaidia wananchi waliopatwa na athari ya janga la kuunguliwa na moto eneo la Kiponda

Kamishna wa kikosi cha zimamoto na uokozi Zanzibar Kanali Rashid Mzee Abdalla aliyevaa kofia ya chuma akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla hatua zilizochukuliwa na Kikosi chake katika uokozi wa maisha ya Wananchi na mali zao kwenye nyumba tatu zilizoathiriwa na kuingiwa na moto katika eneo la Kiponda wilaya ya Mjini Unguja.
Baadhi ya Wananchi wa nyumba tatu zilizoathiriwa na kuingiwa na moto katika eneo la Kiponda wilaya ya Mjini ambao hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuwahifadhi katika majengo ya Nyumba za Wazee Sebleni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Mwakilishi wa Jimbo la Malindi Mh. Mohamed Ahmada Salum mara baada ya kufanya ziara ya kukagua nyumba zilizoathiriwa na kuingiwa na moto katika eneo  hapo Kiponda wilaya ya Mjini.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito kwa Taasisi, wahisani na wafadhili wenye uwezo kujitokeza na kuwasaidia wananchi waliopatwa na athari ya janga la kuunguliwa na moto lililosababisha athari kubwa ya upotevu wa mali na Makaazi.

Mhe. Hemed alieleza hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua nyumba tatu zilizoathiriwa na kuingiwa na moto lilitokea katika eneo la Kiponda wilaya ya Mjini Unguja.

Alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha familia zizopatwa na athari zinabaki kuwa salama muda wote kwa kushirikiana pamoja na serikali ya wilaya  na viongozi wa jimbo la Malindi.

Makamu wa Pili wa Rais alitumia fursa hiyo kukipongeza kikosi maalum cha zima moto na ukozi kwa jitihada zao walizozichukua katika kuukabili na hatimae kufanikiwa kuuzima moto mkubwa uliokuwa tishio kwa maisha ya wakaazi wa nyumba hizo.

“Kipekee nitumie fursa hii kukupongeza sana Kamishna na watandaji wako kwa jitihada mulizozichukua katika kuuzima moto huu” Alisema Mhe. Hemed

Kufuatia tukio hilo Mhe. Hemed alitoa wito kwa wananchi waliopatwa na kadhia hiyo pamoja na wananchi wa eneo la jirani kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na taasisi husika ikiwemo wizara ya Aridhi, Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa na Mamlaka ya uendelezaji Mji Mkongwe ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.

Nae  Muwakilisho wa Jimbo la Malindi Mhe. Mohamed Ahmada Salum alipongeza serikali kupitia kikosi cha zimamoto na ukozi kwa ushirikiano wao waliotoa katika kuhakikisha familia zilizopatwa na Mafaa hayo zinabaki kuwa Salama.

Alieleza kuwa, pamoja na jitihada hizo zilizochukuliwa aliomba serikali kuchukua jitihada za maksudi za kuyafanyia matengenezo nyumba zilizomo katika eneo hilo la mji mkongwe kutokana na uchakavu wa muda mrefu sasa.

Kwa upande wake Kamishna wa kikosi cha zimamoto na uokozi Zanzibar Kanali Rashid Mzee Abdalla alimueleza Makamu wa Pili wa Rais Kuwa kikosi anachokisimamia kimejitahidi kufanya kazi kubwa katika kuhakikisha maisha ya watu yanakuwa salama.

Nao wananchi waliopatwa na athari ya kuunguliwa na moto walisema wanashukuru serikali kwa jitihada walizozichukua katika kuwafariji na wameiomba iendelee kuwapatia huduma muhimu katika kipindi hiki kigumu ikiwemo nguo, chakula na Makaazi.

Akizungumzia Changamoto zilizowakabili Canal Rashisd alieleza kuwa miundombinu hafifu ya kupitishia vifaa vyao imepelekea kuchukua muda katika kukabiliana na moto huo kwani imewalazimu kuweka vifaa vyao katika umbali mkubwa na eneo la tukio.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais alizitembelea na kuzifariji familia zilizopatwa na athari ambazo zimepatiwa hifadhi katika eneo la kwa wazee Sebleni.

Mhe. Hemed wakati akiwafariji wahanga hao ametoa agizo kwa mamlaka zote zianazosimamia utoaji wa huduma ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya Taifa kuchukua jitihada za haraka kwa kuhakikisha wananchi hao wanapatiwa stakabadhi zao ili ziwasaidie kupata haki zao za msingi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.