Na. Paschal Dotto-MAELEZO.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,
ametaja maeneo muhimu yaliyoguswa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika siku 100
tangu alipoapishwa Machi 19, mwaka huu, yakiwa ni pamoja na uboreshaji wa
mazingira ya biashara na kudumisha Amani
yakiwa ni mambo yaliyopewa kipaumbele katika uongozi wake.
Akizungumza katika Kongamano la
siku 100 za Rais Samia, iliyoambatana Mkutano wa wadau wa Baraza la Uwezeshaji
Biashara Tanzania (TNBC), Waziri Mkuu alisema kuwa mafanikio ambayo yamefikiwa
ni kwa sababu ya kuwepo kwa utulivu na ushikamano kwa watanzania ambao Rais
Samia anandelea kuisimamia.
“Leo kwetu ni siku muhumu sana, siku ambayo tumekuja kuhitimisha mkutano wetu wa 12 wa TNBC, lakini pia Rais Wetu Mpendwa leo anafikisha siku 100 tangu alipochukua usukani wa kuiongoza nchi yetu, katika siku hizo Rais Samia amedumisha amani, mshikamano na utulivu miongoni mwa Watanzania na hiyo ni kutokana na ubora wa uongozi wake”, Alisema Kassim Majaliwa.
Majaliwa alisema kuwa mazingira ya biashara yameboreshwa katika siku hizo 100 na hivyo kuvutia wawekezaji, mpaka sasa Wizara ya Uwekezaji kupitia Taasisi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), imesajili miradi ya uwekezaji 93 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.6 na inatarajiwa kuzalisha ajira 24,600.
Pamoja na hilo, alisema amerahisisha upatikanaji wa vibali vya kazi kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi jambo ambalo lilikuwa kero kwa wawekezaji waliokuja nchini na sasa wawekezaji wanapotaka kuomba vibali vya wafanyakazi katika miradi wanayotekeleza wanapata kwa wakati.
Aidha, Majaliwa alisema kuwa ndani ya siku 100 Rais Samia ameboresha mazingira ya biashara baada ya kuagiza kufunguliwa kwa akaunti zote za wananchi na wafanyabiashara zilizokuwa zimefungwa, pia kufuta tozo kero 232 ambazo zilikuwa kikwazo kwa wafanyabiashara
Majaliwa alisema kuwa Rais Samia ndani ya siku 100 alikutana na wafanyabiashara wakubwa na wadogo akiwemo mwekezaji wa kiwanda cha saruji, Aliko Dangote kujadili namna ya kuboresha uchumi wa nchi kupitia uwekezaji.
Katika kuwainua vijana, Majaliwa alisema kuwa Rais Samia ndani ya siku hzio ameridhia ufadhili wa mafunzo ya Ufundi kwa vijana 14,444 kwa miezi sita katika vyuo mbalimbali vya ufundi ili wapate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.
Katika hilo, alifafanua kuwa Rais Samia ndani ya siku 100 ameruhusu mijadala ya maboresho ya mitaala ya elimu ili kujenga ujuzi utakaoendana na mazingira ya nchi, pia ameibua hamasa na kujiamini kwa wanawake katika mambo mbalimbali.
Majaliwa alisema kuwa Rais Samia ameendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya Serikali na ndani ya siku 100 ameweza kusimamia ujenzi wa meli katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Mwanza katika ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na bahari kuu, ujenzi wa Reli ya Kisasa, Bwawa la umeme pamoja na mdaraja ambapo utekelezaji wake uko kwenye hatua nzuri.
“Katika siku 100 ambazo Rais Samia amekuwepo madarakani kama kiongozi wetu ameweza kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi na ukarabati wa Meli, ujenzi wa madaraja, barabara za juu, Bwawa la umeme, Reli ya kisasa na Bomba la mafuta ghafi, hii inadhihirisha kuwa Serikali inaendelea kuaminika kwa wananchi”, Alisema Kassim Majaliwa.
Aidha, Majaliwa alisema kuwa ndani ya siku 100 Rais Samia amegusa ni uboreshaji wa maslahi ya watumishi wa umma, ikiwemo kupandisha madaraja na kupunguza kodi katika mishahara.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Rais Samia ndani ya siku hizo amegusa sekta ya huduma ambapo ameamua kujenga shule za Sekondari za wasichana katika kila Halmashauri na kutoa kiasi cha sh. milioni 500 kwa kila Jimbo kukarabati miondombinu ya barabara.
Pia, alisema katika siku hizo kiongozi huyo ameonyesha kudumisha Diplomasia ambapo amekutana na viongozi mbalimbali kutoka mataifa mengine na kufanya ziara katika nchi za Kenya, Uganda na Msumbiji.
No comments:
Post a Comment