STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
09.06.2021
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi ametoa shukurani kwa viongozi wa dini kwa kushirikiana na
Serikali ya Awamu ya Nane katika kuhamasisha amani na utulivu hapa nchini.
Dk. Mwinyi ameyasema
hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na viongozi mbali
mbali wa dini wakiwemo viongozi wa Dini ya Kiislamu chini ya Mufti Mkuu wa
Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih na viongozi wa dini ya Kikristo wakiongozwa na
Askofu Dickson Kaganga Katibu wa Umoja wa Dini mbali mbali hapa Zanzibar.
Katika maelezo
yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa utayari wa viongozi hao wa kushirikiana na
Serikali ili nchi iendelee kuwa ya amani na utulivu unatoa mwanga mkubwa katika
kuijenga nchi.
Aliongeza kwamba
viongozi wa dini na Serikali wanapaswa kuwa kitu kimoja katika kuendeleza na
kuhamarisha masuala ya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.
Aidha, Rais Dk.
Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi
hao wa dini kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuijenga amani
sambamba na kuondosha ubaguzi hatua ambayo itaiimarisha nchi na kuiletea maendeleo endelevu.
Alieleza kwamba
Serikali ya Awamu ya Nane imechukua juhudi za makusidi katika kuhakikisha aina
zote za ubaguzi zinaondoka hatua ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa hivi
sasa hapa nchini.
Rais Dk. Mwinyi
alieleza haja kwa viongozi hao kwa pamoja kubeba ajenda ya uchumi wa Zanzibar hivi
sasa ambao ni uchumi wa Buluu ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa
sambamba na kuielewesha jamii juu ya dhana hiyo.
Aliongeza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Nane imedhamiria kuja na ajenda ya
uchumi wa Buluu kwa kuona kwamba Zanzibar imezungukwa na bahari na kuwa na rasilimali
nyingi huku ikizingatiwa kwamba ardhi iliyopo haitoshi.
Katika maelezo
yake Rais Dk. Mwinyi alifahamisha haja ya kutoa elimu juu ya uchumi wa Buluu
ili jamii iweze kuuelewa ipasavyo sambamba na malengo yake na kuwataka viongozi
hao kutoa elimu kwa jamii juu ya sekta hiyo.
Rais Dk. Mwinyi
katika maelezo yake aligusia changamoto iliyopo katika ukusanyaji wa kodi hapa
Zanzibar hali ambayo inatokana na matatizo ya kimifumo hatua ambayo alisema
inafanyiwa kazi ili kuhakikisha kila anaepaswa kulipa kodi analipa.
Pia, Rais Dk.
Mwinyi aligusia suala zima la unyanyasaji wa kijinsia na kueleza jinsi hatua za
makusudi zinavyochukuliwa katika kuhakikisha janga hilo linaodoshwa na kutoa
shukurani kwa viongozi wa dini kwa mashirikiano wanayoyatoa kutokana na kadhia
hiyo.
Rais Dk. Mwinyi
alieleza jinsi Serikali pamoja na vyombo vyake ilivyoweka mikakati katika
kuhakikisha janga hilo linapigwa vita.
Aidha, Rais Dk.
Mwinyi alieleza azma ya Serikali katika kuliimarisha soko la ajira kwa
kuitekeleza ipasavyo miradi yake ya maendeleo iliyoipanga ili kuhakikisha
changamoto ya ajira inapatiwa ufumbuzi.
Mapema viongozi wa
dini kwa upande wao walitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa mwanzo
mzuri alioanza nao katika kutekeleza azma yake ya kuwaletea maendeleo wananchi
wote wa Zanzibar.
Viongozi hao
walieleza jinsi walivyofarajika na hatua za makusudi anazozichukua Rais Dk.
Mwinyi katika kuhamasisha amani, umoja na mshikamano huku wakisisitiza haja kwa
viongozi wengine wa Serikali kufuata nyayo zake.
Aidha, walieleza
jinsi Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi ulivyoweka
mikakati ya kuimarisha uchumi wake katika kupitia uchumi wa Buluu huku
wakiahidi kuendelea kumuunga mkono ili kuhakikisha maono yake yanatimia.
Sambamba na hayo,
viongozi hao walieleza jinsi hatua za makusudi zilizochukuliwa na Rais Dk.
Mwinyi mara tu baada ya kuingia madarakani za kuhakikisha anawaweka wananchi
kuwa kitu kimoja na kuondosha ubaguzi wa aina zote.
Viongozi hao,
walieleza matarajio makubwa waliyonayo wananchi wa Zanzibar kutokana na uongozi
thabiti wa Dk. Mwinyi ambapo kwa muda mfupi aliyoongoza wameanza kupata mwanga
wa matumaini sambamba na mabadiliko yaliyopo katika nyanja tofauti.
Walieleza na
kusifu hotuba zake anazozitoa kwa wananchi katika hafla mbali ziwe za kidini
ama kiserikali ambazo zimekuwa dira ya kutekeleza yale yote aliyokuwa
akiyaahidi katika Kampeni zake za uchagauzi.
Pamoja na hayo,
viongozi hao walieleza haja ya kuhakikisha wawekezaji wanawekewa mazingira
mazuri ili waendelee kuja kuekeza hapa Zanzibar huku wakiahidi kwa upande wao
kuwahamasisha wawekezaji wadogo wadogo nao waendelee kuekeza hapa nchini.
Viongozi hao
walipata fursa ya kufanya mahojiano na waandishi wa habari na kueleza utayari
wao wa kumuunga mkono Rais katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment