Habari za Punde

Serikali Yaunda Kamati ya Mpito ya Uratibu wa NGOs Kuhakikisha Uchaguzi wa NaCoNGO Unafanyika

Na Mwandishi Wetu Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameunda Kamati ya mpito ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi  wa viongozi na wajumbe wa Baraza la Taifa la Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali(NaCoNGO) unafanyika.

Akizungumza na waandishi wa habari  Jijini hapa leo, Dkt. Gwajima amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria, Viongozi waliopo madarakani katika Baraza hilo muda wao ulikwisha tangu mwaka 2019.

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Baraza hilo limeshindwa kufanya uchaguzi kwa kipindi chote pamoja na kuelekezwa na Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufanya hivyo kwa muda mrefu.

"Nimeelezwa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali iliwapa Baraza la Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali muda mwingi na nyongeza pia ili kufanya uchaguzi lakini bado hawakutekeleza maagizo hayo" alisisitiza Waziri Dkt. Gwajima

Waziri Dkt. Gwajima amefafanua  kuwa kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 38 (1) na (2) cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002, kuhusu usimamizi wa Sheria hii na utekelezwaji wa kanuni zake, ikiwemo Kanuni za Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za mwaka 2016, ameagiza uchaguzi huo ufanyike haraka ili kuwezesha vyombo vya usimamizi wa Mashirika hayo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria. 

 “Kwa mamlaka niliyopewa kuhusu  usimamizi wa Sheria hii ya utekelezwaji wa Kanuni zake, ikiwemo Kanuni za Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali naunda Kamati ya mpito ili kuhakikisha Uchaguzi unafanyika haraka kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi zilizopo." alisema Dkt. Gwajima.

Ameitaka Kamati hiyo kuhakikisha uchaguzi unafanyika haraka iwezekanavyo  ili kuwezesha vyombo vya usimamizi wa Mashirika hayo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

Aidha, amesisitiza kuwa Wizara haitavumilia tena watendaji na washirika ambao  wanatekeleza wajibu wao kwa kasi isiyoridhisha kwani wanaathiri utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Kamati hiyo ya watu 10 ni inaundwa na Flaviana Charles  Mwenyekiti wa Shirika Mtandao la Coalition for Women Human Rights Defenders in Tanzania (CWHRDsTZ).
Francis Kiwanga – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Civil Society (FCS).
Dkt. Tulli Tuhuma – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la JSI Research and Training Institute (JSI) na
Edward Porokwa – Mratibu wa Shirika Mtandao la Pastoralist Indigineous Non-Governmental Organizations Forum (PINGOs Forum).

Wengine ni Tike Mwambipile – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Women Lawyers Association (TAWLA).
Yassin Ally – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini Womens Rights Organization (KIVULINI).
Anna Kulaya – Mratibu wa Kitafa wa Shirika la Women in Law and Development Africa (WiLDAF).
Audax Rukonge – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agicultural Non State Actors Forum (ANSAF).
Gunendu Roy – Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la BRAC Maendeleo Tanzania (BRAC).
Dkt. Astronaut Bagile – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Women in Social Enterpreneurship (WISE). 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.