Habari za Punde

Wanawake wa UWT Jimbo la Magomeni Watakiwa Kulipa Ada Ili Ili Kuimarisha na Kusimamia Vyema Jumuiya.

Na Mwashungi  Tahir      Maelezo         26/6/2021.

DIWANI wa viti maalum Jumuiya ya UWT Mkoa wa Mjini Wilaya ya Amani Bi.Khadija Ame Haji amewataka akinamama wa Jimbo la Magomeni kulipa ada ili kuimarisha na kusimamia vyema jumuiya hiyo ambayo ndio inayoongoza mustakbali mzima wa jumuiya hiyo.

Ameyasema hayo huko katika ukumbi wa Jimbo la Magomeni wakati alipokuwa akifungua baraza la UWT kwa niaba ya mwakilishi wa viti maalum wa jumuiya hiyo Saada Mwenda na kuwataka akinamama hao kujikita katika ulipaji wa ada ikiwa ni moja kati ya kuimarisha chama  na  jumuiya zake.

Amesema hivi sasa akinamama tuwe na mashirikiano katika jumuiya ili tuweze kusonga mbele kwani tunaweza kupata  maendeleo ambapo  kila jambo  huanzia chini hadi kufikia ngazi za juu tunaona  Serikali  ya Jamhuri ya Muungano imemuweka mama Samiya Suluhu  kuwa Rais ambaye ameanzia chini katika jumuiya ya UWT.

Pia amewataka akinamama kurejesha malezi ya zamani  kwa watoto wetu ili kuwalinda na vitendo vya udhalilishaji kwa kushirikiana  na familiya zetu ili kuwanusuru na majanga haya yalokuwemo na kuwa nao karibu na kufatiliya nyendo zao wakati wa kwenda skuli na madrasa au hata katika michezo yao wanayokuwa wanacheza.

"tuyarudishe malezi ya zamani ya kuleya watoto wetu kwa mashirikiano iwapo pale unamuona anaenda kinyume kwani mtoto wa mwenzio na weye wako",amesema Diwani huyo.

Aidha diwani huyo ambae pia ni Naibu  Meya katika Manispaa ya Mjini amehimiza akinamama hao kujisajili katika vikundi vya ushirika ili waweze kupatiwa mitaji waweze kujiendeleza na pia kufanya vikao ikiwa ni uimara wa jumuiya hiyo.

Akisoma Taarifa ya kazi  kwa kipindi cha kuanzia January hadi June 2021  Katibu wa Jumuiya ya UWT Jimbo la Magomeni Mwanaidi Rashid  amesema uhai wa Jumuiya umezidi kuimarika kwa kuweza kuongeza wanachama wapya 78  na kufikia wanachama 731.

Vile vile amesema kwa upande wa hali ya kisiasa ndani ya jimbo hilo lipo vizuri wanafanya kazi kwa mashirikiano wao pamoja na viongozi wa jimbo hilo.

Akiwasilisha mada ya Uongozi katika baraza hilo mwanachama wa jumuiya ya Vijana  Nihifadhi Faki Ali amewataka akinamama kujitayarisha kuchukua fomu za uchaguzi  ifikapo mwaka 2022 katika nafasi za uongozi kuanzia shina, wadi  hadi ngazi za juu na kuwaomba wasiziache fursa hizo.

Mada nyengine alizoziwasilisha ni pamoja na ulipaji wa ada, uingizaji wa wanachama katika jumuiya na chama cha Mapinduzi kwa kupitia katika madarasa ya itikadi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.