Habari za Punde

MABALOZI WA KODI KUELEZA MAFANIKIO YA SERIKALI YALIYOPATIKANA KWA ULIPAJI KODI

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) akiwataka Mabalozi wa Uhamasishaji wa Ulipaji Kodi kwa Hiari kushirikiana na Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuelezea mafanikio ya Serikali yaliyopatikana kwa njia ya kulipa kodi ikiwa ni pamoja na miradi ya maendeleo, alipofanya mkutano na Mabalozi hao, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) akiongoza mkutano kati yake na Mabalozi wa Uhamasishaji wa Ulipaji Kodi kwa Hiari, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Uhamasishaji wa Ulipaji Kodi kwa Hiari ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Kusini Pemba, akichangia mada wakati wa Mkutano kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (hayupo pichani) na Mabalozi wa Uhamasishaji wa Ulipaji Kodi kwa Hiari, jijini Dar es Salaam

Wajumbe wa Mkutano kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) na Mabalozi wa Uhamasishaji wa Ulipaji Kodi kwa Hiari, wakichangia mada, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.

 (Picha na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam)

Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ametoa rai kwa Mabalozi wa Uhamasishaji wa Ulipaji Kodi kwa Hiari kushirikiana na Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuelezea mafanikio ya Serikali yaliyopatikana kwa njia ya kulipa kodi ikiwa ni pamoja na miradi ya maendeleo.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano na Mabalozi hao ambao waliteuliwa na Waziri wa Fedha na Mipango kwa nyakati tofauti.

Mhandisi Masauni alisema kuwa Mabalozi hao ambao ni pamoja na  wabunge walioteuliwa wanalo jukumu la kueleza namna Serikali ya Awamu ya Sita ilivyojidhatiti katika kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kupanua wigo wa kodi ili kuongeza tija kwa mwananchi katika sekta mbalimbali za kukuza uchumi.

“Mabalozi hawa wanawasikilizaji au watazamaji wa aina mbalimbali  hivyo iwapo watatumia majukwaa yao vizuri kwa kushirikiana na TRA itasaidia katika kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya nchi”, alieleza Mhandisi Masauni.

Alisema mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TRA ni kuhakikisha inatanua wigo wa ulipaji kodi, ambapo kwa sasa mikakati hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje kwa kuondoa vikwazo na kusaidia kuwapata walipakodi wakubwa.

Aidha alisema kuwa Serikali inategemea kodi kwa kiasi kikubwa kwa walipakodi wakubwa hivyo inapoongeza wigo wake kwa kuvutia wawekezaji inajiimarisha zaidi katika kutoa huduma kwa wananchi na kuwaletea maendeleo.

“Serikali imejiandaa kuhakikisha inaweka mifumo mizuri ili kodi inayokusanywa iwafikie walengwa ikiwa ni pamoja na kutekeleza mipango ya maendeleo”, alifafanua Mhandisi Masauni.

Kwa upande wa Kodi ya Miamala ya Simu, alisema kuwa tayari Rais alishatoa maelekezo kwa Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu kuunda timu ya wataalamu ili waweze kuona ni namna bora ya kuboresha kodi hiyo ikiwa ni pamoja na kuangalia marekebisho ya Sheria

Lengo la Serikali kuhusu kodi hiyo ilikuwa zuri ikiwa ni pamoja na kusaidia katika Bima ya Afya kwa wote, hivyo wale ambao hawana uwezo waweze kupata matibabu kwa uhakika na pia kushusha gharama za maisha kwa wananchi kwa kuweka miundombinu mizuri ya usafiri na usafirishaji itakayorahisisha maisha.

Vilevile alisema kuwa huduma ya miamala kutoka Kampuni za Mawasiliano imekuwa ikitozwa fedha kwa anaetoa na anaepokea hivyo sio jambo geni, aidha ametoa angalizo kwa baadhi ya Kampuni hizo kwa namna zinavyofanya promosheni yake kuhusu kodi ya Serikali kwa njia ya miamala kwa kutoa taswira mbaya pekee na sio faida zitakazo mgusa mwananchi moja kwa moja.

Mhandisi Masauni amewapongeza Mabalozi wa kuhamasisha kulipa kodi kwa hiari kwa kuonesha nia ya dhati katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kujua umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo yao.

Kwa upande wao Mabalozi wa kuhamasisha kulipa kodi kwa hiari, waliipongeza Serikali kwa hatua yake ya kuwateua na kutambua umuhimu wao katika uhamasishaji, aidha wameahidi kufanya kazi kwa bidii katika jukumu hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.