Habari za Punde

Mhe Hemed afungua kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Mjini Unguja

Mjumbe wa kamati kuu ya halmshauri kuu ya CCM taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wanachama wa Umoja wa Vijana wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Mjini kilichofanyika katika Ukumbi wa Zanzibar Ocean View Kilimani.

 Wajumbe wa kikao cha Baraza kuu la UVCCM Mkoa wa Mjini wakifuatilia kwa umakini hotuba ya Mgeni rasmi Mjumbe wa Kamati kuu Mhe. Hemed alioitoa wakati akifungua kikoa cha Umoja huo katika ukumbi wa Zanzibar Ocean View.

Na Kassim Abdi, OMPR

Mjumbe wa kamati kuu ya Halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi Taifa Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema chama cha Mapinduzi kina matumaini makubwa na Jumuiya za chama katika kufanikisha Fikra,mikakati na mitazamo ya kuwaandaa vijana wake kushika nafasi za uongozi.

Mjumbe huyo wa kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa alieleza hayo wakati akifungua mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa vijana wa chama cha Mapinduzi(UVCCM) Mkoa wa Mjini uliofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Ocean View Hotel uliopo kilimani.

Alisema wajibu wa wanachama wa chama cha Mapinduzi pamoja na Jumuiya zake zina jukumu la kuhakikisha CCM inashinda katika chaguzi zote kama ilivyo elezwa ndani ya katiba ya chama ibara ya 5(1) ikiwemo kushinda uchaguzi wa Serekali kuu na Serekali za mitaa kwa upande wa Tanzania Bara.

“Mnapaswa kuelewa kuwa Jumuiya za chama cha Mapinduzi zimeundwa ili kuisaidia CCM, UVCCM Ikiwa ni moja ya Jumiya hizo ina Jukumu la kutimiza malengo ya CCM “Alisema Mhe.Hemed.

Aliwakumbusha wasimamizi wa Jumuiya hiyo ya Umoja wa vijana kutosahau wajibu wao wa kuwaandaa vijana ili wawe viongozi Bora wa baadae kupitia chama na Serekali sambamba na kulinda,kutetea,pamoja na kushawishi vijana wengine kujiunga na chama hicho.

Alieleza kuwa, suala la Serekali inayo tekeleza Ilani ya CCM kuwapa nafasi za uongozi vijana ni jambo lisilo epukika kwa kuzingatia mahitaji ya jamii na uwendeshaji wa Nchi kuhitaji vijana wenye uweledi waliopikwa kupitia chama cha Mapinduzi.

Mhe.Hemed aliwaeleza vijana wa UVCCM kwamba, chama cha Mapinduzi kupitia Serkali zake zote mbili kimetoa nafasi nyingi za uongozi kwa vijana ambapo Mara Rais wote wawili kupitia teuzi zao wameonesha jinsi walivyojenga matumaini na kuwapa nafasi za uongozi vijana wanaotokana na chama cha Mapinduzi.

“Napenda niwathibitishie vijana wote walioteuliwa wameonesha ujuzi,maarifa na uwezo wa uongozi katika nafasi walizopewa,Hivyo naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza sana UVCCM kwa weledi na kuiva kiuongozi”Alieleza Mjumbe huyo wa kamati kuu.

Makamu wa Pili wa Rais Mhe.Hemed alisema bado ipo haja ya kuwapa fursa vijana kupitia chaguzi mbalimbali hususani majimboni ili chama kiendelee kuwaanda vijana waweze kushika nafasi za uongozi.

“Sisi katika chama chetu hatuoni vijana ni tishio la uongozi bali ni chachu ya kuharakisha utendaji kazi kupitia Nyanja zote za kisiasa na kiuchumi”Alisema Makamu wa Pili wa Rais.

Akisoma risala kwa niaba ya vijana hao wa UVCCM Mkoa wa Mjini Katibu wa Vijana wilaya ya Mjini Ndugu Ramadhani Abass Mcheju alimueleza mgeni rasmi kuwa Umoja wa vijana wa chama cha Mapinduzi ni chombo cha kuwaunganisha vijana pamoja kwa lengo la kuwapatia taaluma itakayowasaidia katika harakati za maisha yao ya kila siku.

Alisema Mkutano huo wa Baraza kuu la Umoja wa Vijana Mkoa wa Mjini pia utajadili na kutathimini siku mia moja (100) za Mama Samia tangu angie madarakani ambapo wamefarajika sana na imani alioionesha kwa kuwateua vijana kuwakabidhi dhamana ya Uongozi.

Katika risala yao vijana hao walimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa mkakati aliokuja nao wa kudhibiti mapato ya serikali na kuhakikisha anaziba mianya yote ambayo watumishi wasiokuwa waaminifu hutumia kwa kujinufaisha binafsi.

Kuhusiana na Changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Umoja wa Vijana Mkoa wa Mjini walisema  umoja huo unakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa maeneo kwa ajili ya kujenga nyumba za watendeji wa Jumuiya.

“Ndugu mgeni rasmi aliekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa ndugu Heri Denis James alitoa agizo kujengwa kwa nyumba za watendaji lakini hapa kwetu bado tunasuasua katika utekelezaji wa agizo hilo kwa kukosa maeneo ya kujenga nyumba hizo”. Alisema Katibu Mcheju

Nae, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM anaefanyia kazi zake Zanzibar ndugu Mussa Haji Mussa alimuhakikishia Mjumbe wa kamati kuu ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kufuatia uchaguzi mdogo wa jimbo la konde Unatarajiwa kufanyika Julai 18 mwaka huu umoja wa vijana utahakikisha ushindi wa jimbo hilo unapatikana mchana kweupe.

Vile vile, Ndugu Mussa aliwaomba vijana wa umoja huo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbali mbali kufuatia uchaguzi wa chama kupitia ngazi tofauti unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka ujao pamoja kuepuka tabia ya kutengeneza makundi yatakayosababisha kudhoofisha maendeleo ya Jumuiya hiyo na chama kwa Ujumla. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.