Habari za Punde

Zaidi ya Shilingi Bilioni 42 Kutumika Kuboresha Umeme Mkoani Tabora – BYABATO

 

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato akizungumza na Waandishi wa Habari alipotembelea  kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Kiloleni kilichopo Tabora mjini, mkoani Tabora 
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato akipata maelezo kutoka kwa msimamizi wa Kituo cha Kiloleni Frank Chengula namna chombo cha kuongozea mitambo kinavyofanya kazi kituoni hapo

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Mwandamizi wa Mifumo ya Umeme wa Kanda ya Magharibi TANESCO, Yahya Ngasongwa kuhusu upokeaji na usambazaji wa umeme kituoni hapo tarehe 10 Julai, 2021.

Zaidi ya shilling Billion 42 zimetengwa na Serikali kwa ajili ya kuboresha kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Kiloleni, wilayani Tabora mjini, mkoani Tabora ili kuimarisha huduma ya umeme mkoani humo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato tarehe 10 Julai, 2021 alipotembelea  kituo cha kupozea na kusambaza  umeme cha Kiloleni kilichopo Tabora mjini, mkoani Tabora.

Naibu Waziri Byabato amesema, Tabora ni mkoa wa kimkati wenye fursa nyingi za maendeleo ikiwemo migodi, kilimo na viwanda hivyo, unahitaji kuwa na umeme wa uhakika kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa kasi.

Ameongeza kuwa, umeme wa uhakika mkoani Tabora utawezesha uendeshaji wa train ya kisasa (Standard Gauge) ambayo uzinduzi wa shughuli za ujenzi wake unatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Naibu Waziri Byabato ameeleza kuwa, kituo cha kupozea na kusambaza  umeme cha Kiloleni, kinachopokea umeme kutoka mkoa wa Shinyanga na kusambaza katika wilaya za Tabora, Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui kikiwa na megawatt 24 kilianza kazi mwaka 1989 hivyo ni muhimu kukiboresha ili kiwe na umeme wa uhakika na kuwa fedha zilizotengwa zitapelekea kituo hicho kuwa na megawatt 72.

Aidha, Naibu Waziri Byabato amebainisha kuwa, Kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Kiloleni ni miongoni mwa vituo 9 vinavyotarajiwa kuboreshwa mkoani Tabora ili kuwa na umeme wa uhakika.

Vilevile, Naibu Waziri Byabato ameagiza kutengenezwa kwa transfoma iliyoharibika ndani ya Mwezi Julai, 2021 ili kuongeza nguvu ya umeme kituoni  Kiloleni licha ya kuwa kuna transfoma moja inayofanya kazi.

Aidha Naibu Waziri Byabato ameelezea kuridhishwa kwake na utendaji wa Ofisi ya TANESCO mkoa wa Tabora na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa kasi, ubunifu na usahihi ili kufikia malengo ya Kitaifa katika sekta ya Nishati.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.