Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi - Zanzibar, Mhe. Rahma Kassim Ali akikata utepe, wakati akizindua rasmi Minara nane za Mawasiliano jana, Alhamisi, katika kijiji cha Bumbwini Mafufu. Kulia kwake (aliyeshikilia utepe) ni Mkuu wa Zantel-Zanzibar, Mohammed Khamis Mussa.
Waziri wa
Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi - Zanzibar, Mhe. Rahma Kassim Ali akimsikiliza
Afisa Mkuu wa Teknolojia wa Kampuni ya Zantel, Lucas Nchimbi (aliyesimama
katikati) wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Minara nane ya Mawasiliano
jana, Alhamisi, katika kijiji cha Bumbwini Makoba. Kulia kwake ni Mkuu wa
Zantel-Zanzibar, Bw Mohammed Khamis Mussa.
Katika jitihada za
kuboresha huduma za mawasiliano visiwani Zanzibar, Kampuni ya Mawasiliano ya
Zantel, imezindua minara nane ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa
na mtandao hafifu ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora.
Minara hiyo iliyopo katika vijiji vya Seacliff, Kisiwa Uzi, Bumbwini Mafufu, Kisiwani, Chambani, Makangale, Maziwa N’gombe
na Jongowe imezinduliwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi -
Zanzibar, Rahma Kassim Ali.
Akizunguza wakati wa hafla ya uzinduzi, Mkuu wa Zantel-Zanzibar, Mohammed
Khamis Mussa alisema lengo ni kuhakikisha Zanzibar yote inapata huduma bora na
za uhakika za mawasiliano pamoja na mtandao wa intaneti.
“Zantel tumeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuboresha huduma za
mawasiliano hapa Visiwani Zanzibar.Leo tuna furaha kukamilisha minara hi inane
mipya ambayo itasaidia katika kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja wetu,”
alisema.
Aliongeza “Mbali na kusogeza huduma za kupiga simu kwa watu, dhamira
ya Zantel kwa sasa ni kuendeleza matumizi ya intaneti na mfumo wa kidijitali
katika masoko yetu. Tunaendelea
kuboresha mtandao wetu wa intaneti kutoka kasi ya 2G na 3G na kuweka mtandao wa
4G katika baadhi ya maeneo,” aliongeza.
Pia, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara
ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji pamoja Wakala wa Miundombinu ya Tehama
(ZICTIA) kwa kushirikiana kwa karibu na kampuni ya Zantel ambapo mpaka sasa zaidi ya asilimia 86 ya
Zanzibar imeunganishwa na mtandao.
Kupitia ushirikiano na ZICTIA, Zantel imefanikisha kuunganisha
zaidi ya minara 33 kwenye mkonga wa Mawasiliano (Fibre) kwa zaidi ya kilomita
28 ambayo imesaidia kuongeza ufanisi wa huduma.
Akizindua minara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi -
Zanzibar, Rahma Kassim Ali aliipongeza Zantel kwa uwekezaji mkubwa ambao
imeufanya katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano kote Unguja na Pemba.
“Kampuni ya Zantel imekuwa karibu sana na serikali katika kutatua
changamoto za mawasiliano zinazowakabili wanachi wetu wa Zanzibar, ninawapongeza
sana kwa hili,” alisema.
Aliongeza “Mawasiliano ni muhimu sana katika upatikanaji wa taarifa
sahihi zinazofika kwa wakati sahihi ili kufanya maamuzi ya kimaendeleo. Ndiyo
maana serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za Kujenga
miundombinu madhubuti ya TEHAMA kama vile Mkonga wa Mawasiliano wa Taifa na
vituo vya kutunzia taarifa (data centre) ambayo imesaidia kukuza mawasiliano
nchini na kuhakikisha usalama wa mawasiliano.”
Alisema kuwa, kuimarika kwa huduma za mawasilaino kutachangia
kukuza uchumi wa Bluu kwa kuimarisha upatikanaji wa taarifa za masoko katika
sekta hiyo.
Aidha, Zantel imechukua hatua kadhaa katika kuelimisha wananchi juu
ya umuhimu wa intaneti kupitia kampeni yake kabambe ya PASUA ANGA KI ZANTEL
4G ili wateja waweze kuelewa umuhimu wa mtandao na kuweza kunufaika na
fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment