Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais azuru Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja atoa maagizo mazito

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akitembelea vitengo mbali mbali vinavyopatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja wakati alipofanya ziara Leo kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi katika sekta ya Afya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Dk. Msafiri Marijani  kutoa kipaumbele maalum kwa Maabara ya kupimia vinasaba mbali mbali kutokana na umuhimu wake katika kutoa majibu ya vipimo kwa wananchi.
Mtaalamu wa kupima vinasaba vya Ugonjwa wa Covid-19 akimpatia maelezo ya Kitaalamu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.Mhe Hemed Suleiman Abdulla, wakati alipotembelea maabara hiyo akiwa katika muendelezo wa ziara zake katika sekta ya Afya

Na Kassim Abdi, OMPR

Uongozi wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia wazee na watoto umetakiwa kusimamia vyema majukumu yake katika sehemu za kazi ili kurejesha nidhamu kwa Watumishi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara katika Hospital ya Rufaa ya Mnazi Moja ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kuimarisha utendaji kazi katika taasisi mbali mbali za serikali.

Alieleza kuwa, uongozi wa Wizara ya Afya unatakiwa kusimamia kwa karibu kurugenzi zake kwa lengo la kuhakikisha ufanisi unapatikana kwa wananchi wanaofika kupata huduma katika vituo vya Afya.

Mhe. Hemed alisema kuna kila sababu kwa Wizara hiyo kuwa makini katika utendaji wa kazi zake za kila siku kwani ripoti zinaonesha kwamba Wizara ya Afya imo katika orodha ya taasisi zisizozingatia nidhamu katika matumizi ya Fedha za serikali.

Makamu wa Pili wa Rais katika kurejesha nidhamu ya matumizi ya fedha za serikali alimuagiza Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii wazee, Jinsia na watoto  kuhakikisha dawa na Vifaa tiba vinavyonunuliwa viwe vinaendana na Thamani halisi Fedha inayotumika.

Alifafanua kuwa, Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Mwinyi imedhamiria kuimarifa huduma zinazotolewa na Sekta ya Afya sambamba na kudhibiti matumizi ya Fedha za serikali na itakapobidi haitasita kubadilisha baadhi ya sheria ili kufanikisha lengo hilo la serikali.

Akikagua Maabara ya kufanyia vipimo vya vinasaba mbali mbali Mhe. Hemed aliuagiza uongozi wa wizara  hiyo kutoa Kipaumbele maalum kwa kitengo hicho kutokana na umuhimu wake kwa kutatua changamoto za vifaa pamoja na kuangalia maslahi ya wafanyakazi ya watendaji katika sekta ya Afya kutokana na kufanya kazi katika mazingira hatarishi.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka viongozi wanaosimamia kipimo cha vinasaba vya Covid-19 kuacha kuwaharakisha wataalamu wanaofanya vipimo hivyo ili waweze kutoa majibu sahihi kwa sampuli zinazowasilishwa katika maabara hiyo.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed alisikitishwa kwa kusuasua kwa huduma ya upatikanaji wa mashuka kwa wakati kulikosababishwa na kuharibika kwa kifaa cha mashine ya kufulia, kifaa ambacho harama yake haizidi shilling Laki Nne (400,000/=).

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Hopital ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Dk. Msafiri Marijani alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa mbali na jitihada zinazochukuliwa na watalamu katika Hospital hiyo lakini wanakabiliwa na changamoto tofauti ikiwemo upungufu wa wataalamu wa kada mbali mbali, uhaba wa idadi ya Vyumba vya kuendesha matibabu ya upasuaji pamoja na upungufu wa Vitendanishi kwa ajili ya kufanya vipimo katika maabara.

Kwa Upande wake Afisa Muuguzi Mkuu Hamida Hamid alieleza kuwa, Hospital ya Rufaa ya Mnazi Mmoja imekuwa ikikabiliwa na Changamoto ya kuzidiwa na watu wengi kunakosababishwa na wananchi wengi kukiuka taratibu kwa kutoanzia kupata huduma katika vituo vyao vya karibu katika sehemu wanazoishi.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais amendelea kutoa wito kwa wataalamu wa sekta ya Afya kuendelea kujitokeza kupata chanjo dhidi ya Maradhi ya Covid-19 ili kujikinga na maumbukizi ya virusi vinavyosababishwa maradhi hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.