Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Aendelea na Ziara Yake katika Taasisi Mbalimbali za Serikali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akitembelea na kukagua dawa na vifaa tiba katika Bohari Kuu ya dawa iliopo Maruhubi wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Bohari hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.Mhe Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi Jijini Zanzibar wakati wa ziara yake katika Taasisi hiyo inayotowa huduma za usambazaji wa Dawa kwa Mahospitali ya Zanzibar. 

Na.Abdi Kassim OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameutaka uongozi wa Bohari Kuu kusambaza vitendanishi (Reagents) katika vituo vya afya vyenye uhitaji ili kuwaondelea usumbufu wananchi wanaohitaji huduma iyo.

Mhe. Hemed ametoa agizo hilo katika ziara ya kushtukiza aliyoifanya Bohari kuu ya dawa iliyopo Maruhubi Jijini Zanzibar

Alisema amesikitishwa kuona baadhi ya Vituo vya Afya kukosa huduma hiyo wakati Ghala la Bohari kuu limesheheni mzigo mwingi wa dawa na vifaa vya kutosha vinavyohitajika katika vituo vya Afya.

Mhe. Hemed alieleza kuwa si vyema wananchi kulipia huduma nje ya vituo vya afya ambapo huwagharimu kiasi cha fedha kupata huduma hiyo ilhali huduma hiyo kuna uwezekano wa kupatikana kwa Hospital za serikali.

Alifafanua kwamba  kutokana na uzembe unaofanywa na baadhi ya watendaji wa vituo hivyo kushindwa kuagiza vifaa hivyo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo pasi na usumbufu.

Makamu wa Pili wa Rais alimuagiza Mkugenzi Mkuu Wizara ya Afya kutowavumilia na kuwachukulia hatua watendaji wanaochelewa kuagiza dawa bohari kuu kwani kufanya hivyo kunawachelewesha wananchi kupata huduma stahiki.

Akigusia suala la uendeshaji Mhe Hemed aliwapongeza watendaji wa Bohari hiyo kwa uwajibikaji wao na kuwataka kuharakisha mfumo wa kuorodhesha dawa zinazoagizwa ili dawa zipatikane kwa wakati.

Kuhusu changamoto ya usafiri Makamu wa Pili wa Rais alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya kuzifanyia matengenezo gari za kusambazia dawa ndani ya mwezi mmoja ili kuzidisha kasi ya usambazaji wa dawa vituoni.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari hiyo Dk. Zahran Ali Hamad alisema wizara itaendelea kuandaa wataalamu na kuwasambaza katika vituo vya wilaya ili waweze kukagua vifaa katika vituo vya Afya mbali mbali ili kuitatua changamoto ya ubovu wa vifaa inayojitokeza.

Wakieleza changamoto wanazokumbana nazo wafanyakazi wa bohari hiyo wamemueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa ucheleweshaji wa maombi ya dawa kutoka vituoni hupelekea kuchelewa kwa usambazaji wa dawa zinazohitajika, jambo ambalo linapelekea wananchi kupoteza imani na serikali yao.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitembelea kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki Beitrasi kwa ajili ya kujionea maendeleo ya kituo hicho namna kinavyozalisha vifaranga ikiwa ni ufatiliaji wa ziara yake aliyoifanya Novemba 20 mwaka jana.

Katika ziara hiyo Mhe. Hemed amejionea amefurahishwa na maendeleo mzauri ya usiamamizi wa kituo hicho.

Mhe. Hemed alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imepanga kukuza uchumi wake kupitia uchumi wa Buluu, eneo ambalo wananchi wa Zanzibar wana imani kubwa katika kujipatia kipato sambamba na kutoa ajira kwa wananchi.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa idara ya uvuvi na mazao ya Baharini Ndugu Salum Soud Muhamed alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa uongozi wao unategemea kuanzisha mradi wa kuzalisha kole kole kwa mashirikiano na Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam ambapo ndani ya miezi sita watazalisha samaki wa kutosha.

Pamoja na mambo mengine Mkurugenzi Salum aliomba Serikali kuzidisha juhudi zaidi za kukuza uzalishaji wa samaki wa maji baridi ambapo kuna wawekezaji mbali mbali wameshaanza kuonesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa samaki hao, akitolea mfano muwekezaji mmoja ambae ameshakamilisha taratibu zote za Mamlaka ya  Uwekezaji Zanzibar.

Katika ziara hiyo Mhe. Hemed alijionea aina mbali mbali za samaki wanaozalishwa katika kituo hicho ikiwemo, sato, kambare,Mwatiko, kole kole, kaa na majongoo.

Ziara hizo za Makamu wa Pili wa Rais zinalenga kufuatilia na kuimarisha utendaji kazi katika taasisi mbali mbali za serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.