Habari za Punde

Mkutano wa Kikao Kazi cha IORA Chafungwa

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu  -Zanzibar Ndg.Zahor Kassim Mohd  akizungumza na wadau wa (IORA) kuhusu uvuvi wa Bahari kuu katika Ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari kuu huko Fumba mara walipofika  Ofisini hapo katika mwendelezo wa Ziara yao ilionzia eneo  la kutotolea Vifaranga Beit-Ras Kibweni Mjini Unguja.

Na. Issa Mzee - Maelezo 15/09/2021                                                                                                          

Wadau wa jumuiya ya nchi zilizopo kwenye mwambao wa bahari ya hindi wametakiwa kuzitangaza fursa zilizopo nchini ili kuimarisha uwekezaji katika sekta ya uvuvi.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu Ikulu, Mussa Haji Ali wakati akifunga kikao cha siku tatu cha wadau wa jumuiya ya nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi kilichofanyika katika Ofisi za ZURA Maisara Mjini Unguja.

Alisema fursa zilizopo katika bahari ya Hindi ni nyingi ikiwemo uwekezaji katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu ambao unaleta faida kubwa katika kukuza uchumi wa buluu nchini.

Alieleza kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa jumuiya ya nchi zilizopo kwenye mwambao wa bahari ya hindi hasa katika kuutangaza utalii ambao unasaidia katika kukuza uchumi wa taifa.

Alisema Serikali zote mbili zinaendelea kufanya jitihada za kuimarisha matumizi bora ya bahari ikiwemo kupiga vita uvuvi haramu katika bahari ili kulinda uchumi wa bahari.

Aidha katibu huyo alisema ziara zilizofanywa na wadau hao ya kutembela kituo cha kutotolea vifaranga Kibweni na Mamlaka ya bahari kuu Fumba ziwe ni chachu ya kuibua mawazo mazuri yatakosaidia katika kufanikisha uchumi wa buluu nchini.

Mapema Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uvuvi wa bahari kuu, Dk. Emmanuel Sweke ameswema ipo haja ya kuwahamasisha wazawa kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu ili rasilimali za taifa zitumike kuwanufaisha wananchi.

Alifafanuwa kuwa wawekezaji wengi wanaokuja kuwekeza katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu ni wageni, hivyo ipo haja ya kuwawezesha wazawa kimtaji ili waweze kuwekeza.

Aidha alipendekeza ujenzi wa bandari ya uvuvi nchini,ujenzi wa viwanda vya samaki,upatikanaji wa boti, na ufugaji wa samaki ufanyike nchini ili rasilimali ya bahari ilete manufaa makubwa zaidi kwa taifa na kuzalisha ajira kwa watanzania.

Wadau wa jumuiya ya nchi zilizopo kwenye ukanda wa bahari ya hindi walipata fursa ya kutembelea kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki Kibweni na Mamlaka ya Uvuvi wa bahari kuu Fumba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.