Habari za Punde

UWT Wilaya ya Amani Kichama Kuadhimisha Wiki ya UWT 4-10-2021.

Na Mwashungi  Tahir  Maelezo   29-9-2021.

Mwenyekiti wa Kamati  tekelezaji ya UWT Wilaya ya Amani  Fatma Amrani Abdullah  amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi  na jumuiya  kushirikiana  kuwa karibu na wanachama wao ili waweze kusikiliza changamoto zinazowakabili ili wakae pamoja na kuzitatua.

Ameyasema hayo leo huko  Wilaya ya Amani wakati kamati tekelezaji ya UWT Wilaya Amani ilipokuwa na ziara ya kuwakagua waasisi wa UWT ambao hivi sasa wagonjwa ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya wiki ya UWT ambayo inatarajiwa kuadhimishwa ifikapo tarehe 4-10-2021.

Amesema ni faraja kubwa kuwatembelea akinamama hao ambao wametumikia Chama na Jumuiya zake kwa muda mrefu na kufikia pahala pazuri katika utendaji  na kuwaomba viongozi wa ngazi zote ikiwemo Mkoa na Wilaya  na viti maalum wa UWT kuwapitia mara kwa mara  na  kuwafariji ili waone  mchango wao unatambulika kwa kipindi chote walichotumikia .

“Nawaomba viongozi wenzangu tuwe na muda wa kuwatembelea wanachama wenzetu huku tukikumbuka mchango wao waliofanya katika chama na jumuiya itawapelekea kuhamasika na kujua na wao wanakumbukwa  kwa yale waliyofanya katika kuleta maendeleo  katika majimbo yao”, alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha amesema akinamama hao walikuwa mstari wa mbele katika kukiendeleza chama pamoja na jumuiya kwa kuleta maendeleo katika mambo mbali mbali  kuhakikisha jumuiya inasonga mbele kwa kupatikana viongozi waliyo imara.

Hivyo ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka vituo vya polisi katika kila baadhi ya shehia kwa lengo  la kukomesha vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto  ambavyo hivi sasa vinazidi kushamiri ndani ya mitaa  na kujenga khofu kwa jamii hasa  ukatili wa kupigwa mapanga na visu  na kutaka sheria kali itumike.

Nae Katibu wa UWT Wilaya ya Amani Sufiya Ubwa Mamboya  amesema  tumuunge mkono Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  kwa kuwataka viongozi wa majimbo washuke chini kwa wanachama ili kuweza kusikiliza changamoto zao  na kukaa pamoja katika kuzitatua.

“Wamefanya kazi kubwa walipokuwa na nguvu zao hadi sasa hawajiwezi tena wanahitaji kusaidiwa kwa kuwapitiwa huduma ambazo wanazihitaji.

Kwa upande wao wagonjwa hao wameishukuru kamati hiyo kwa kuwatembelea na kuwafariji na wameomba iwe endelevu  na kuwataka na viongozi wa juu kuwatembeleya.

Pia wamewaomba viongozi walioko hivi sasa katika jumuiya ya UWT kufanya kazi kwa mashirikiano kama walivyofanya wao wakati wa uzima wao, kwani wakifanya hivyo kutaweza kukuza chama na jumuiya kwa vizuri zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.