Habari za Punde

Wananchi Kisiwani Pemba Watakiwa Kujikita Katika Kilimo cha Zao la Alizeti.

Mratibu wa Uchumi Jamii kutoka Milele Zanzibar Foundation, Alice Mushi akizungumza na wanakikundi cha Tupate sote kilichopo Mavungwa wakati wa ziara ya kukitembelea kikundi hicho.

Na.Mwandishi Wetu TAMWA-ZNZ.

JAMII kisiwani Pemba imeshauriwa kujikita katika uzalishaji wa zao la Alizeti ili kukiwezesha kiwanda cha kutengeneza mafuta ya alizeti kilichopo Mavungwa, Shehia ya Mbuzini Wilaya ya Chake chake Pemba kuzalisha kwa wingi mafuta hayo na kufikia lengo la uwepo wa kiwanda hicho.

Wito huo umetolewa na mratibu wa Uchumi Jamii kutoka Milele Zanzibar Foundation, Alice Mushi wakati wa ziara ya kutembelea kiwanda hicho kinachomilikiwa na kikundi cha Tupate Sote kupitia mradi wa kuwawezesha Wanawake kiuchumi Zanzibar unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ).

Alisema ili lengo la kuwainua wanawake kiuchumi liweze kufikiwa, kiwanda hicho bado kinahitaji upatikanaji wa malighafi za kutosha jambo ambalo linahitaji msukumo wa hamasa kwa wananchi kuzalisha kwa wingi zao hilo ili kukidhi mahitaji ya kiwanda hicho.

“Kuna haja ya kufanya kampeni ya kuhamasisha watu ili walime alizeti kwa wingi kwa lengo la kupata malighafi za kutosha kutengenezea mafuta hayo,” alisema.

Aliongeza iwapo wakulima watazalisha kwa wingi zao hilo itawezesha kiwanda kuzalisha mafuta kwa wingi na kusaidia kupunguza uhaba wa mafuta visiwani kulingana na ukubwa wa kiwanda chenyewe.

Alisema, “tukiwa na watu wengi wanaolima zao hili, hii mashine itakaa inafanya kazi saa 24 na hivyo itasaidia sana upatikanaji wa mafuta hapa.”

Kwa upande wake afisa uwezeshaji wanawake kiuchumi (WEZA) kutoka TAMWA ZNZ.Bi. Asha Mussa Omar aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika upatikanaji wa malighafi ili kukifanya kiwanda kuendeleza uzalishaji ipasavyo.

“Niwakati mwafaka kwa wadau kujitokeza na kuja kuwekezeka katika kiwanda hiki ili kusaidia kuongeza nguvu ya uzalishaji wa kiwanda kutokana na changamoto kubwa inayokikabili kiwanda ni uhaba wa malighafi jambo ambalo litasaidia ufikiaji wa malengo ya kikundi,” alisema.

Katibu wa kikundi hicho, Meiye Hamad Juma alisema changamoto kubwa ambayo inawakabili kwasasa ni kukosa mtaji kwani mahitaji ya soko yameongezeja licha ya juhudi walizochukua kuomba mikopo kwaajili ya kujiimarisha lakini bado hawajafanikiwa kupata mikopo. 

Alisema, “Tunashukuru wateja wapo wengi sana kwa sasa lakini changamoto kubwa inayotukabili hatuna mtaji kwani tumeomba mkopo Wizara ya Uwezeshaji, Baraza la Mji na SMIDA lakini mpaka sasa hatujapata kwahiyo hii imeturejesha sana nyuma kutokana na hatuna uwezo wa kununua alizeti za kutosheleza mahitaji ya soko letu.”

Ziara ya kutembelea kikundi hicho ni mwendelezo wa ziara za Milele Zanzibar Foundation kutembelea wanufaika wa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi (WEZA) unaotekelezwa na TAMWA ZNZ katika maeneo mbalimbali Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.