Habari za Punde

DK. Khalid Amefungua Mkutano wa Kuthibitisha Rasimu ya Sera ya Kinga ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu.

Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Braza la Wawakilishi Dkt. Khalid Salum Mohammed akifungua Mkutano wa kuthibitisha Rasimu ya Sera ya kinga ya Usafirishaji Haramu wa Binaadamu na Kinga ya Uhamiaji Haramu katika bara la Afrika,hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Madinatul Bahari Mbweni Zanzibar.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa kuthibitisha Rasimu ya Sera ya Kinga ya Usafirishaji Haramu wa Binaadamu na Kinga  ya Uhamiaji Haramu katika Bara la  Afrika wakifuatilia mkutano huo uliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Madinatul Bahari Mbweni Zanzibar.

Na Issa Mzee - Maelezo Zanzibar   06/10/2021

Kamisheni ya Haki za Binadamu  ya Umoja wa Afrika (AU), imeamuwa kuweka sera ya kinga dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, na uhamaji haramu kwa lengo la kupiga vita  uvunjifu wa Haki za Binadamu unaofanywa Barani Afrika.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Kuthibitisha sera hizo katika ukumbi wa Hotel ya Madinatul Bahri Mbweni Zanzibar ,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi,  Dk, Khalid Salum Mohamed amesema umefika wakati wa kuhakikisha uhalifu huo unapotea Afrika.

Alisema kwa muda mrefu Barani Afrika kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu kwa kusafirisha watu kwenda nje ya Afrika jambo ambalo huwaletea madhara makubwa wanapofika ugenini.

Alieleza kuwa, ni jambo lisilopingika kuwa, Nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania zinaathirika vibaya kutokana na usafirishaji haramu wa binadamu, licha ya kuwepo sheria ya kimataifa inayokataza uhalifu huo.

“Uhalifu huu huwaathiri na  kuwakumba zaidi wanawake na watoto na kupelekwa nchi mbalimbali ikiwemo Mashariki ya Kati na hata Barani Ulaya ambapo hukutana na vitendo mbalimbali vya uvunjifu wa haki za binadamu ikiwemo mauaji” alisema Waziri huyo.

Hivyo ,alisema uthibitishwaji wa sera ya Kinga ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu na Kinga Ya Uhamaji Haramu katika Bara la Afrika ni hatua muhimu na  itasaidia katika kuondoa uhalifu huo.

Nae Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la Wahamaji(IOM) Tanzania, Qassim Sufi,alisema shirika hilo linatambua madhara ya uhalifu huo ambao kwa kiasi kikubwa husababishwa na hali ya kukosekana kwa amani na utulivu katika baadhi ya mataifa ya Afrika.

Alisema licha ya kuwepo kwa sera hizo, ipo haja kwa kila Nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha Raia wanalindwa hasa wanawake na watoto.

Aidha alieleza kuwa, Shirika linaloshughulikia Wahamaji Duniani (IOM),linapenda kuona haki za binadamu zinalindwa hasa kwa wahamaji, kwani ni haki ya kila mwanadamu kuheshimiwa na kupewa haki zake popote Duniani.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Michezo  Utamaduni, Kazi,  Ajira  na  Uhamaji kutoka Umoja wa Nchi za Afrika(AU), Bw.Sabelo Mbokazi, alisema Bara la Afrika haliwezi kuwa na amani wala maendeleo ikiwa uhalifu wa kusafirisha binadamu unaendelea kuwepo.

Alieleza kuwa, upatikanaji wa haki za binadamu na uwepo wa sera na sheria madhubuti, utasaidia katika kuhakikisha Raia wa Afrika wanabaki salama katika Mataifa yao.

Alisema utekelezaji wa sera mbili zinazotarajiwa kuthibitishwa katika mkutano huo ni miongoni mwa hatua madhubuti zinaweza kusaidia katika kutokomeza uhaklifu huo Barani Afrika.

Hata hivyo, alisema umefika wakati wa kuhakikisha wahalifu wote wanaohusika nauhalifu huo wanafikishwa katika vyombo vya sharia na kufunguliwa mashataka ili kukomesha vitendo hivyo.

Mkutano huo uliolenga kuthibitisha Sera ya Kinga ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu na Kinga ya Uhamaji Haramu umehudhuriwa na nchi mbalimbali  za Umoja wa Afrika  ikiwemo Zambia, Algeria,Mauritania  na Tanzania.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.