Habari za Punde

Serikali Kupunguza Gharama za Kusafisha Figo

 Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO.

Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) inatarajia kupunguza gharama za huduma ya kuchuja damu kutoka shilingi 189,000 – 300,000 iliyopo sasa hadi shilingi 100,000 kwa matibabu ya awamu moja.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya MSD kuingia mikataba na watengenezaji wa mashine na vifaa vya kuchuja damu kununua moja kwa moja kutoka kwao.
 
Gharama hizo zimetajwa na Mkurugenzi Mkuu Bohari ya Dawa, Meja Jenerali Gabriel Mhidze (Dkt) wakati akizungumza na Maafisa Habari wa Idara ya Habari - MAELEZO hivi karibuni kuhusu maboresho yaliyofanywa na taasisi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja, hasa katika kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa bidhaa za afya endelevu na kwa bei nafuu. 
 
Meja Jenerali Mhidze amesema hatua ya kununua mashine hizo moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji imewezesha bidhaa hizo na vitendanishi vyake kushuka bei kwa zaidi ya asilimia 50, ambayo inategema kuokoa fedha za Serikali shilingi Bilioni 62 kwa miaka Mitano.
 
"MSD kwa sasa inanunua mashine hizi kwa shilingi bilioni 10.9 ukilinganisha na shilingi bilioni 20.6 ambazo zingetumika kununua kutoka kwa Washitiri, tumeamua kufanya hivyo ili kupunguza gharama ya kusafisha figo kwani gharama zake hapa nchini ziko juu", alisema Meja Jenerali Mhidze.
 
Ameongeza kuwa tayari mashine za kusafisha damu zimenunuliwa na tayari zimeshafungwa hospitali ya UDOM, Chato, Sekou Toure na Mafia, na tayari hospitali nyingine zimeshaomba kununua na kufungiwa mashine hizo, hatua ambayo itaongeza maeneo ya huduma hiyo, na kwamba hospitali nyingine za Rufaa na Mikoa zinaendelea kufanya mawasiliano na MSD kwa ajili ya huduma hiyo. 

Kwa upande mwingine, MSD tayari imefanya mazungumzo na Mfuko wa Bima ya afya wa Taifa (NHIF) ambapo wao watavikopesha vituo vya kutolea huduma za afya nchini vifaa mbalimbali vya maabara, wakati NHIF ikishiriki katika ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma hizo.
 
Akifafanua kushuka kwa bei ya mashine za maabara, baada ya kuingia mikataba ya ununuzi na wazalishaji, Afande Mhidze amesema kuwa kwa sasa shilingi Bilioni 10.9 zinatumika kununua vifaa vya maabara na vile vya kuchuja damu, badala ya shilingi Bilioni 20.6 ambazo zingetumika kununua bidhaa hizo kutoka kwa washitiri kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.