Habari za Punde

Wataalam Kufanya Tathimini Kubaunisha Mipaka Pori la Akiba Mkungunero.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mery Masanja akizungumza na wananchi wa Bereko wilayani Kondoa mkoa Dodoma wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi 
Mbunge wa Jimbo la Kandoa ambaye ni Waziri wa Habari, Mwasiliano na Teknolojia Dkt Ashatu Kijaji  akizungumza wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi kwenye kijiji cha Bereko wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma
Sehemu ya wananchi wa Bereko wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mawaziri wa kisekta wakati wa ziara ya kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wakazi wa kijiji cha Bereko wilayani Kondoa mkoa Dodoma wakati wa ziara ya mawaziri wa kisekta kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi 

Na Munir Shemweta, WANMM KONDOA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema timu ya wataalamu itapelekwa katika Pori la Akiba la Mkungunero lililopo wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma kufanya tathmini na kuweka mipaka upya kwa lengo la kuepusha kuvamiwa.

 

Waziri Lukuvi alibainisha hayo tarehe 6 oktoba 2021 wilayani Kondoa mkoani Dodoma wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Bereko akiwa katika ziara ya Mawaziri wa kisekta ya kutoa mrejesho wa utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 920.

 

"Katika Pori la Akiba la Mkungunero tutafanya tathmini upya na kuweka mipaka upya ili wananchi wajue eneo lililohifadhiwa linaanzia wapi na  linaishia wapi" alisema Lukuvi.

 

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, baada ya kufanyika tathmini upya na mipaka kupimwa hatarajii kuona wananchi wakivamia maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba na kueleza kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kumaliza migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Akielezea mgogoro wa matumizi ya ardhi eneo la Bereko wilayani Kondoa, Lukuvi alisema, eneo hilo halina mgogoro mkubwa ukilinganisha na maeneo mengine kwa kuwa mgogoro uliopo unaohusisha ekari 17.2 pekee.

 

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka wakazi wa Bereko kujiepusha na tabia ya kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji na kubainisha kuwa, serikali haitasita kuwaondoa watakaojenga kandokando ya mito.

 

Mapema Mbunge wa jimbo la Kondoa ambaye ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia  Dkt. Ashatu Kijaji aliueleza ujumbe wa Mawaziri nane wa kisekta kuwa  wananchi wa eneo la Bereko wana tatizo na msitu wa TFS kwenye mlima Salanka aliouleza kuwa mipaka yake imekuwa haitabiriki kutokana na kuhamahama.

 

"Msitu katika Mlima Salanka umekuwa kero na wananchi wanaumizwa, msitu una mipaka isiyotabirika kwa kuwa inahamahama na wakati mwingine inasogezwa kwenye mbaazi" alisema Dkt Ashatu.

 

Timu ya Mwaziri nane ikiongozwa na Waziri Lukuvi imemaliza ziara yake kwenye mkoa wa Dodoma katika wilaya ya Kondoa kwa kutembelea vijiji na mitaa kwenye pori la akiba la  Swagaswaga na vijiji vilivyopo kinga la mita 500 katika pori la akiba la Mkungunero na baadaye kuelekea mkoa wa Manyara kuendelea na ziara ya kutoa mrejesho wa utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya hifadhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.