Habari za Punde

Dk Hussein Mwinyi: Kushuka kwa kiwango cha usalama husababisha kuporomoka kwa utalii


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa matukio mbali mbali yakiwemo kushuka kwa kiwango cha hali ya usalama husababisha kuporomoka kwa utalii.

 Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo  katika uzinduzi wa Kikosi cha Polisi wa Utalii na Diplomasia, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar.

 Katika hotuba yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa baadhi ya nchi zimepoteza watalii baada ya kushuka kwa kiwango cha hali ya usalama pamoja na mambo mengineyo yakiwemo kutokea kwa machafuko ya kisiasa, vita vya wenyewe kwa wenyewe, miripuko ya maradhi na majanga.

 Alisema kuwa uchumi wa Zanzibar ulitetereka kwa kiwango kikubwa kutokana na kuibuka kwa janga la maradhi ya UVIKO 19 ambapo hili ni janga la Kimataifa lakini pia, ziko nchi kadhaa duniani ambazo zimepoteza watalii kutokana na matukio ya ndani ya nchi zao.

 Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba uanzishwaji wa Kikosi cha Polisi wa Utalii kwa madhumuni ya kulinda na kuimarisha usalama wa watalii ni hatua muhimu na inayoendana na dhamira ya kuhakikisha watalii na wageni wanaoitembelea Zanzibar wako salama na wakirejea kwao wanakuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza kwa mambo mazuri.

 Hivyo, alitumia fusra hiyo kwa kuwataka viongozi watakaopewa dhamana ya kuongoza Kikosi hicho wajifunze kutokana na mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya Kikosi kilichofanana na hicho kilichokuwepo hapo awali.

 “Imani yangu ni kwamba, Askari watakaoteuliwa katika kikosi hiki wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya kazi ya uaskari ipasavyo, wakijuwa kwamba wao wakichafua basi itakuwa ni vigumu kwa watalii kuiamini taasisi nyengine ikiwa wale waliopewa majukumu ndio wanaharibu”,alisema Rais Dk. Mwinyi.

 Aidha, aliwanasihi wananchi wa Mikoa, Wilaya na Shehia zote za Unguja na Pemba kushirikiana na askari hao ili kuhakikisha wageni wanaoitembelea Zanzibar pamoja na wananchi wote wanaishi katika mazingira yaliyo salama na yenye amani na utulivu.

 Dk. Mwinyi aliwataka wadau wa Utalii kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na Serikali katika kuiendeleza sekta ya utalii ili kuinua uchumi, kukuza ajira, kutoa huduma bora na kuimarisha mitaji na faida kwa wawekezaji waliojitolea kuja kuwekeza nchini.

 Alisisitiza kutafutwa njia na mbinu za pamoja za kuyaunganisha makundi ya wajasiriamali na sekta ya utalii ili kuwasaidia kupata masoko ya bidhaa wanazozalisha na huduma zanazotoa ili wajasiriamali hao wadgo wadogo na wao wafaidike na utalii.

 Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliyataja mambo ambayo bado hayajafanywa vizuri ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma kwa wageni hasa katika viwanja vya ndege na bandarini pamoja na utoaji wa huduma za upimaji wa maradhi ya UVIKO 19.

 Alisema kwamba bado hajaridhishwa na msongamano na foleni ndefu katika madeski ya kutolea viza, malipo ya benki, ukaguzi wa mizigo, utoaji huduma kwa wateja na ucheleweshwaji unaosababishwa na uzembe wa watendaji katika viwanja vya ndege.

 Nae Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Lela Muhamed Mussa alisema kuwa kikosi hicho kipya cha Polisi wa Utalii, maandalizi yake yalianza mwezi wa Aprili mwaka huu 2021 kwa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kake kushirikiana na Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ pamoja na Jeshi la Polsi kwa kuunda Kamati maalum ya kuratibu uanzishwaji wa kikosi hicho.

 Aliitaja Jumuiya ya Watembeza Wageni Tanzania (TATO) pamoja na Kikosi cha Polisi Utalii cha Diplomasia Arusha ambapo taasisi  hizo zimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kutoa uzoefu wa jinsi gani wamefanikiwa katika kukabiliana na uhalifu kwa upande wa Tanzania bara hasa Mkoa wa Arusha ambako wageni wengi hutembelea.

 Waziri Lela alisema kuwa gharama yote inayohitajika katika kuwekeza kwenye Kikosi hicho ni Bilioni 8 ambapo gharama za operesheni za kila siku ni takriban milioni 500 kwa mwaka hivyo, alizitaka sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizo za Serikali ya Awamu ya Nane za Kupambana na Uhalifu kwa wageni.

 Mapema, akisoma risala kwa niaba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Kamishna Msadiizi wa Jeshi la Polisi (ACP) Eugene Emanuel alisema kuwa Kikosi hicho cha Polisi Utalii kilichozinduliwa hivi leo kitakuwa na askari wasiopungua 150 kutoka kikosi cha Polisi, Uhamiaji, JKU, KMKM, KVZ,KZU na Chuo cha Mafunzo Zanzibar.

 Alisema kuwa askari hao watagawanywa katika Mikoa yote mitano ya Zanzibar ambapo kila Mkoa utakuwa na Kituo kikubwa cha Utalii chenye askazi 30 na kufuatiwa na vituo vidogo vitakavyojengwa katika maeneo yanayotembelewa zaidi na watalii.

Alieleza kwamba kwa upande wa Unguja vituo hivyo vitajengwa huko Nungwi, Kendwa, Kiwengwa, Matemwe na Pwanimchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkoa wa Kusini ni Chwaka, Uroa, Jambiani, Paje, Michamvi na Kizimkazi na kwa upande wa Mjini Magharibi vitajengwa huko Forodhani, Mtoni, Fumba, Uwanja wa Ndege na Chukwani na kwa upande wa Pemba vitajenwga Chakechake na Makangale.

 Katika hafla hiyo, Rais Dk. Mwinyi pia, alikabidhi vyeti maalum vya shukurani kwa Wakufunzi wa kikosi hicho pamoja na kuwakabidhi Wakuu wa Vikosi Maalum vya SMZ Vitambulisho vya Polisi wa Utalii na Diplomasia ambapo mapema akiwasili katika eneo hilo alianza kwa kupokea Gwaride Maalum la Kikosi cha Polisi wa Utalii.

  Imetayarishwa na kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.