Habari za Punde

Madhehebu Yatakiwa Kuwa na Mahusiano Mazuri na Jamii.

Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Dkt Magnus Mhiche akimpongeza baada ya kumtunuku cheti mmoja wa wahitimu 32 wa Stashahada ya Theolojia katika Chuo cha Western Bible College kilichoko Mkoani Tabora jana. Picha na Lucas Raphael,

Na.Lucas Rphael,Tabora 

MADHEHEBU ya dini nchini yameshauriwa kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka ili neno la Mungu liweze kuwafikia kwa wepesi zaidi na kuongeza idadi ya waumini.

 

Rai hiyo imetolewa jana na Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) hapa nchini Dkt Magnus Mhiche katika Mahafali ya 3 ya Chuo Cha Western Bible College kilichoko Mkoani Tabora.

 

Alisema kujenga mahusiano mazuri na jamii kutafungua milango ya ushirikiano baina ya kanisa na wakazi wa eneo husika hivyo kuwafanya watu wengi zaidi kumwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao.

 

Alisisitiza kuwa dini yoyote inayojali jamii na kujenga mahusiano mazuri haiwezi kukosa waumini, hivyo akawataka Maaskofu na Wachungaji kuhimiza waumini  wao kuwa na mahusiano mazuri na jamii.

 

Alitoa mfano wa kanisa la TAG jinsi ambavyo limekuwa mstari wa mbele kutoa misaada mbalimbali kwa kijamii ikiwemo kuchimba visima vya maji safi ya kunywa katika maeneo mbalimbali, kujenga shule na kuchangia huduma za afya.

 

Askofu Mhiche aliwataka Watumishi 32 waliohitimu masomo yao ya Theolojia kwenda kuwa mfano wa kuigwa katika utumishi wao huku akiwataka kwenda kuanzisha makanisa na kuleta uamsho mpya katiba ibada zao.

 

‘Kanisa linahitaji uamsho mpya wenye nguvu katika makanisa yetu, ili agizo kuu la Yesu Kristo lidhihirike, roho mtakatifu ashuke kwa nguvu makanisani, ishara na miujiza mikubwa itendeke na waumini waendelee kuongezeka ’, alisema.

 

Alisisitiza kuwa Mungu humwongezea nguvu yeye asiye na uwezo (Isaya 40: 29-31) na huwapa nguvu wazimiao hivyo akawataka kutokataa tamaa katika utumishi wao hata kama huduma zao zitakuwa zinachechemea.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Rev.Kenedy Lukilo alisema wahitimu hao wamepikwa vizuri kiroho na kimwili, wameiva na sasa wako tayari kuingia kwenye  utumishi wa Mungu.

 

Alitaja baadhi ya shughuli ambazo wamefanya wakati wa mafunzo yao kuwa ni kushiriki kazi za mikono, kuhubiri neno la Mungu, kushiriki ujenzi wa makanisa vijijini, kuchangia damu ili kuokoa maisha ya jamii, kushiriki ujenzi wa vyoo vya shule na nyinginezo nyingi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.