Habari za Punde

NAIBU WAZIRI MABULA AKAGUA MAJENGO YA NHC KARIAKOO YANAYOWEZA KUTUMIWA NA WAMACHINGA

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa pili kulia) akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji na Uendelezaji Biashara wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) William Genya (kulia) akiwa kwenye mitaa ya Kariakoo jijini Dar es Salaam kukagua majengo ya NHC yanayoweza kutumiwa na Wamachinga.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipanda katika moja ya majengo wakati wa ziara ya akikagua majengo ya Shirika la Nyumba la Tiafa (NHC) yanayoweza kutumiwa na Wamachinga kwenye maeneo ya Kariakoo Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga Tanzania Stephen Lusinde wakati akikagua majengo ya Shirika la Nyumba la Tiafa (NHC) yanayoweza kutumiwa na Wamachinga kwenye maeneo ya Kariakoo Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa pili kulia) akiangalia baadhi ya majengo kwenye mtaa wa Tandamti Kariakoo wakati akikagua majengo ya Shirika la Nyumba la Tiafa (NHC) yanayoweza kutumiwa na Wamachinga jijini Dar es Salaam


Na Munir Shemweta, WANMM

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametembelea eneo la Karikaoo kwa lengo la kuangalia namna bora ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga kutumia majengo ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kufanyia biashara.

Hatua ya Naibu Waziri inafuatia wafanyabiashara hao kuandika barua Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupatiwa sehemu za kufanyia biashara kwenye majengo ya Shirika la Nyumba la Taifa yaliyopo kariakoo kufuatia Seriali kuamua kuwaondoa wale waliokuwa wakifanya biashara maeneo ya barabarani.

Ombi la wafanyabiashara hao lilisababisha Ofisi ya Rais TAMISEMI kuiomba Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuangalia namna ya kuwasaidia Wamachinga kwa kuwapatia sehemu kwenye baadhi ya majengo ya NHC yaliyopo maeneo ya Kariakoo jijini Dar es Salaam ili waweze kufanya biashara. Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) liko chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Hatua hiyo ya TAMISEMI ilimfanya Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuamua kufanya ziara ya kukagua majengo ya NHC yaliyoainishwa kwenye mitaa ya Tandamti na Msimbazi kwa ajili ya kujiridhisha na kuona kama majengo hayo yanaweza kufaa kwa biashara za wamachinga.

Hata hivyo, majengo ya NHC yaliyoainisha katika mtaa wa Msimbazi na Nyamwezi yameonesha kutokidhi vigezo lakini Naibu Waziri wa Ardhi na timu ya viongozi wa NHC walibaini majengo mengine matatu yatakayofaa kwa shughuli za wamachinga.

Akiwa ameambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji na Uendelezaji Biashara wa Shirika la Nyumba la Taifa William Genya, Kamishna wa Ardhi Msaidzi mkoa wa Dar es  Salaam Idrisa Kayera na Meneja wa NHC mkoa wa Ilala Erasto Chilambo tarehe 3 Oktoba 2021, Dkt Mabula alitembelea majengo kadhaa na kuridhika majengo matatu yaliyopo mtaa wa Mkunguni na Nyamwezi kwa kueleza kuwa majengo hayo yanaweza kuboreshwa na kutumika.

Akielezea uamuzi wa kufanya ziara katika maeneo ya kariakoo, Naibu Waziri Dkt Mabula alisema uamuzi huo unalenga kuangalia namna bora ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo hasa baada ya TAMISEMI kupeleka ombo na kubainisha kuwa msisitizo ni kuwapatia Wamachinga maeneo ya kudumu yakiwa na miundombinu.

‘’TAMISEMI walianisha mitaa ya Tandamiti na Msimbazi kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo lakini maeneo hayo yameonesha kutokidhi mahitaji lakini sisi tumeona majengo matatu yaliyopo mtaa wa Nyamwezi na Mkunguni karibu kabisa na Soko Kuu la Kariakoo yanaweza kufanyiwa mabadiliko kwa ajili ya shughuli za kuhudumia mahitaji ya wafanyabiashara wadogo wamachinga’’. Alisema Naibu Waziri Dkt Mabula

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo wa Ardhi alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa kulichukulia suala hilo kwa umuhimu mkubwa na haraka  kutokana na changamoto zake na kusisitiza kuwa wakati hatua za utekelezaji maendelezo ya majengo yaliyoainishwa ukifanyika ni vyema kila kitu kikawekwa ili wafanyabiashara wakaelewa muelekeo wao.

‘’Hili ni suala la msingi na lazima lifanyike kwa haraka na sisi Wizarani tulipate taarifa mapema na tujue majengo haya yatachukua watu wangapi na uendelezaji wake utachukua muda gani ili wafanyabiashara wajue kuna eneo maalum la kufanya biashara kama kama ambavyo wamekusudia wao kupatiwa’’ alisema Dkt Mabula.

Taarifa aliyoiomba Dkt Mabula inatakiwa kueleza namna NHC itakavyoendeleza majengo yaliyoainishwa, idadi ya wafanyabiashara watakaotumia majengo hayo pamoja na gharama zitakazotumika katika kubadilisha matumizi.

Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga Tanzania Stephen Lusinde kwa upande wake alisifu uamuzi wa Naibu Waziri Dkt Mabula kutembelea majengo ya NHC yaliyoainishwa na kubainisha kuwa hatua hiyo inaonesha kuwa sasa mambo yanaweza kukaa vizuri kwa wamachinga kupata muelekeo wa wapi pa kwenda.

‘’Tumezunguka na Naibu Waziri wa Ardhi kuangalia majengo ya NHC tuliyoainisha kwa ajili ya wamachinga hii inaonesha kuwa sasa mambo yanaweza kukaa vizuri kwa wamachinga kupata ule muelekeo wa wapi kwa kwenda kwa ajili ya kufanya shughuli zao’’ alisema Lusinde.

Amesema, hatua inayofanywa na Serikali kutaka kuwapatia wamachinga majengo yanayomilikiwa na NHC kwa ajili ya kufanyia biashara ni kuonesha kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya mama Samia Sulkuhu Hassan inakwenda kutekleleza zile ajira ambazo walizitangaza katika kampeni za ccm 2020.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.