Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ameweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya L'oasis Beach Resort Kizimkazi leo.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja (hawapo pichani) wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya L’oasisi Beach Resort, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha Mwaka Mmoja wa Uongozi wake

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi wa Mikoa na  Wilaya zote nchini kuhakikisha vijana wa Kizanzibari wanapewa kipaumbele katika upatikanaji wa nafasi za ajira katika miradi yote ya Uwekezaji inayotekelezwa katika maeneo yao.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo leo katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi wa Hoteli ya Kitalii ya L’oasis Beach Resort, ilioko Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni maadhimisho ya kutimia mwaka mmoja tangu kiongozi huyo aingie madarakani.

Amesema Viongozi wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wawekezaji wana wajibu wa kuhakikisha vijana wa Kizanzibar, hususan wale walioko katika maeneo ya miradi wanapewa kipaumbele katika suala la uaptikanaji wa nafasi za ajira ili waweza kunufaika na uwepo wa uwekezaji huo.

Alisema Viongozi hao pia wana jukumu la kusimamia na kuhakikisha hoteli hizo zinanunua bidhaa zote zinazopatikana au kuzalishwa katika maeneo hayo, ikiwemo bidhaa zitokanazo na uvuvi, kilimo, pamoja na ufugaji, ikiwa ni hatua ya wananchi hao kupata soko la bidhaa zao.

Rais Dk. Mwinyi akwia amefuatana na Mama Mariam Mwinyi katika hafla hiyo, aliwataka viongozi hao kuhakikisha Wawekezaji wanasaidia upatikanaji wa huduma za jamii katika maeneo wanayowekeza, ikiwemo suala la maji, elimu , huduma za Afya pamoja na miundo mbinu ya barabara.“Wajibu wa Wawekezaji katika kuisaidia jamii ufanyike vyema ……”, alisisistiza.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Wawekezaji wako tayari kuwekeza baada ya kujenga imani kubwa na Serikali kutokana na kuwepo kwa amani, umoja na mshikamano nchini, hivyo akabainisha umuhimu wa Uwekezaji huo kuleta tija  kwao na kwa Taifa.

Aliwashukuru Wawekezaji hao kwa imani hiyo na kuwekeza miradi mikubwa hapa nchini, hivyo akatumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kuitunza amani iliopo  ili Utalii uweze kuleta tija na manufaa kwa Taifa na wananchi kwa ujumla.

Alisema Sekta ya Utalii itaendelea kuwa sekta kuu ya uchumi wa Zanzibar, mbali na uchumi huo kushuka kutokana na janga la ugonjwa wa UVIKO 19 ulioikumba dunia.

Hata hivyo, alieleza kuwa hali imeendelea kutengemaa baada ya ugonjwa huo kuonyesha dalili za kupungua, hivyo akawataka wanachi kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili ugonjwa huo umalizike kabisa.

Mapema, Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Hadidi Rashid Hadidi alisema uongozi wa Mkoa huo kwa kutambua kuwa   Mkoa uko katika ukanda wa Utalii, umelazimika kuweka kipambele katika  suala la usafi katika maeneo yote ya Mkoa huo.

Alisema hatua ya kufanyika maridhianao ya kisiasa hapa nchini kumeshajiisha uwepo wa amani na hivyo kuhamasisha  shughuli za uwekezaji.

Mkuu wa Mkoa huyo alieleza kuwa Mwekezaji wa Hoteli ya L’ oasis Beach Resort ameweza kutekeleza mradi huo kutokana na imani kubwa aliyonayo kutokana na uhamasishaji unaofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Nae, Mkurugenzi wa Mradi huo wa Hoteli ya L’oasis Beach Resort Ahmeid Saber alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuunga  mkono utekelezaji wa mradi huo, pamoja na kuahidi kutekeleza kikamilifu sheria na miongozo yote ya Uwekezaji. 

Ujenzi wa Hoteli ya L’oasis Beach Resort  umegharimu  Dolla za Kimarekani Milioni 15, inahusisha   vyumba 142, ikiwemo vyumba maalu vyenje hadhi ya juu 14 pamoja na Mabwawa ya kuogelea 23, ikiwa na  jumla ya  wafanyakazi 150 kati yao 103 kutoka Shehiya za Kizimkazi na pale  ujenzi wake utakapokamilika itakamilisha ajira za vijana 300.

Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.