Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametunukiwa cheo cha heshima na jukumu la kuwa kinara au bingwa wa Taifa wa Kampeini ya “The National Champion for the UN Women HeForShe campaign”

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Cheti cha Heshima cha Kinara au Bingwa wa Taifa wa Kampeni ya "The National Champion for UN Women Hefor She" na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughika na Maasuala ya Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women ) Bi. Hodan Addou na Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bw. Zlatan Millisic na (kushoto kwa Rais ) Mama Mariam Mwinyi na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar Mhe Nassor Ahmed Mazrui, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Hotel ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametunukiwa cheo cha heshima na jukumu la kuwa kinara au bingwa wa Taifa wa Kampeini ya “The National Champion for the UN Women HeForShe campaign” na kuahidi kwamba atakitumikia vyema cheo hicho.

Ahadi hiyo ameitoa leo wakati akisoma hotuba yake ya uzinduzi wa Kampeni ya HeForShe iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la UN Women, ambalo ndilo lililomkabidhi Rais cheo hicho katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Hoteli ya Verde, Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi aliahidi kwamba atakuwa bega kwa bega katika kupigania na kuimarisha usawa, haki, maslahi na ustawi wa wanawake pamoja na usawa wa aina zote kwa jinsia zote.

Alisema kuwa amekuwa akijitahidi kwa nguvu na uwezo wake wote kutoa haki kwa misingi ya usawa kwa jinsia zote kwani yeye ni muumini wa kweli wa haki na maendeleo ya wanawake.

“Suala la kuwatumia wananchi wa Zanzibar wa jinsia zote kwa misingi ya haki na usawa ni utii wa Katiba ya Zanzibar ambayo nimeilia kiapo kwamba, nitaitii kwa hivyo suala hilo kwangu ni la lazima”,alisema Rais Dk. Mwinyi.

Aidha, alisema kwamba suala la kuwepo kwa usawa wa kijinsia na kuimarisha maendeleo ya wanawake ni la lazima hasa ikizingatiwa kwamba Sensa ya Watu na Makaazi iliyofanywa mwaka 2012 ilionesha kwamba idadi ya wanawake Zanzibar ni 672,892 na wanaume 630,677 hivyo, ni dhahiri kwamba maendeleo hayawezi kupatikana iwapo sehemu kubwa ya nguvu kazi ya Zanzibar itawachwa nyuma na bila ya kuwezeshwa kwa misingi ya usawa.

Rais Dk. Miwnyi alisema kuwa hivi sasa amekuwa akiyatekeleza kivitendo yale aliyoyalia kiapo na yale aliyoyaahidi kwa nyakati mbali mbali katika teuzi anazozifanya ambapo amekuwa akiteua viongozi bila ya ubaguzi wa aina yoyote kwani amekuwa akijali sifa na uwezo wa watu.

Aliongeza kuwa amekuwa akiteua wanawake katika nafasi mbali mbali na kuwashirikisha kikamilifu katika utoaji wa maamuzi katika masuala muhimu ya Serikali na nchi kwa jumla  huku akisisitiza kwamba maendeleo yaliyopatikana hapa Zanzibar na katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha usawa wa kijinsia ni ya kupigiwa mfano.

Rais Dk. Miwnyi alisema kuwa idadi ya viongozi wanawake hapa Zanzibar inaendelea kupanda ikilinganishwa na miaka ya nyuma vile vile, ameteua Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi mwanamke na kumteua Mwanamama kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), ikiwa ni mara ya kwanza kwa nafasi hizo kushika wanawake.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza wanawake aliowateua katika Serikali yake kwani hawajamuangusha na wanafanya kazi vizuri na vyema kuliko wanaume na kueleza kwamba takwimu zilizopo za uongozi kati ya wanawake na wanaume Serikali zinaweza kubadilika muda si mrefu.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwataka Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid kushirikiana na UN Women kwa kwenda kufikisha ujumbe  maalum katika vyombo vya kutunga sheria wanavyoviongoza kuhusiana na malengo na maudhui ya Kampeni hiyo.

Rais Dk. Mwinyi aliiagiza Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jisnia na Watoto Zanzibar pamoja na taasisi zote za Serikali kufanya kazi kwa karibu na Shirika la UN katika kutekeleza malengo na maazimio ya Kampeni hiyo ili kuzidi kuimarisha uwasa wa kijinsia na maendeleo ya wanawake hapa Zanzibar.

Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Shirika la UN Women katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, unyanyasaji, mimba za umri mdogo, utelekezaji wa watoto na mambo yote ambayo ni kikwazo kwa maendeleo ya wanawake na watoto.

Nae Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui alieleza hatua zinazochukuliwa na Wizara yake katika kuhakikisha inapambana vyema na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Nao Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid walimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba wanamsaidia kufikisha Kampeni hiyo na kuwa tayari kwa marekebisho yoyote ya sheria ambayo bado ni kikwazo kwa maendeleo ya Kampeni hiyo.

Viongozi wa UN hapa nchini kwa upande wao na baadhi ya Mabalozi wa nchi za Ulaya waliohudhuria mkutano huo katika hotuba zao waliahidi kuendelea kuiunga mkono Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kampeni hio na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa jinsi anavyojali suala zima la jinsia katika uongozi wake huku wakiiwapongeza wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekekeleza kwa vitendo suala hilo na kuwa kinara kwa kuwa na Rais mwanamama.

Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.