Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ameshiriki Mbio za Zanzibar Blue Economy Hafla Marathon 2021 cKilomita 4.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Zawadi Maalum ya picha yake ya kuchora na Mwenyekiti wa Kamati ya “Zanzibar Blue economy half Marathon 2021” Bw.Abdalla Idrissa Majura, kwa ushiriki wake katika mbio hizo kwa kushiriki kilomita 4 kuazia Mapinduzi Square hadi Uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezindua mbizo za “Zanzibar Blue economy half Marathon 2021” ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya sherehe za mwaka mmoja tokea ashike madaraka ya kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambapo leo yamefikia kilele.

Uzinduzi huo wa mbio hizo ulifanyika leo (Novemba 06. 2021) mapema saa 12 za asububi kwa kuanza kutimua vumbi katika eneo la “Mapinduzi Square” Mwembe Kisonge Jijini Zanzibar na kuishia katika uwanja wa Amaan kwa kupitia katika mzunguko wa maeneo mbalimbali yaliyopangwa ambapo wanariadha hao walianza mbio hizo wakiwemo wakimbiaji  wa kilomita 10 na wale wa kilomita 21.

Mara baada ya uzinduzi huo Rais Dk. Mwinyi akiwa na Mama Maria Mwinyi aliwaongoza  viongozi akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla , wananchi pamoja na vikundi mbali mbali vya mazoezi katika matembezi ya kilomita nne  yaliyoanza hapo “Mapinduzi Square” Mwembe Kisonge hadi uwanja wa Amaan, Jijini Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa vyeti kwa baadhi ya wadhamini wa mashindano hayo kwa niaba ya wenzao pamoja na kutoa kuwavisha nishani washindi wa mashindano hayo ambapo pia, alipata fursa ya kuangalia mashindano ya riadha ya wazee kuanzia miaka 60 pamoja na mashindano ya riadha kwa watu wenye ulemavu wa miguu.

Akitoa maelezo mafupi juu ya mashindano hayo, Mwenyekiti wa “Zanzibar Blue economy half Marathon 2021” Abdalla Idrissa Majura alieleza kwamba mashindano hayo ni kwa ajili ya kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kutimiza mwaka mmoja tokea aingie madarakani kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Majura alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kuonekana kwamba Rais Dk. Mwinyi ameanza kutekeleza ahadi zake kwa vitendo akiwa na lengo la kuiletea maendeleo Zanzibar ambapo na wao wakiwa wanamichezo wanamuunga mkono Rais Dk. Mwinyi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya (CCM).

Aidha, Mwenyekiti huyo alisema kuwa mashindano hayo pia, yanawasaidia wananchi wa Wazanzibari katika kufanya mazoezi kwa lengo la kupambana na maradhi yasioambukiza.

Mwenyekiti huyo aliitaja mikakati waliyoiweka katika maandalizi ya mashindano hayo pamoja na namna ya upatikanaji wa fedha za mashindano hayo ulivyofanyika na kusisitiza haja ya mashindano hayo hapo mwakani kuungwa mkono zaidi na Serikali ili yawe ya Kimataifa kama yalivyo mashindano mengine yakiwemo yale ya Kilimanjaro Marathon.

Alieleza jinsi wadhamini mbali mbali waliojitokeza kuunga mkono mashindano hayo ya riadha ambapo miongoni mwa wafadhili hao ni  Benki ya “National Microfinance Bank” (NMB) waliodhamini mashindano ya kilomita 21 ambapo mshindi wa mwanzo alikabidhiwa TZS milioni moja, mshindi wa pili laki 8 na wa tatu laki 5.

Pamoja na hayo, kwa upande wa mashindano ya killomita 10, kwa maelezo ya Mwenyekiti huyio Benki ya “Kenya Commercial Bank” (KBC) iliyadhamini ambapo mshindi wa kwanza alipata TZS laki 8, mshindi wa pili laki 5 na wa tatu alipata laki 3.

Pia, (KCB) wamedhamini mbio fupi za uwanjani ambapo wanariadha wastaafu kila mmoja atapata TZS laki 1000,000 kwa wanaume na wanawake huku wanariadha wote 200 watakaoshiriki watapa TZS 50,000 bila ya kujali mshindi wa mwanzo au wa mwisho.

Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo alisisitiza lengo la Kamati ya mashindano hayo la kusaidia ujenzi wa soko la Fumba.

Wadhamini wengine wa waliosaidia mashindano hayo ni Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mohamed Raza kupitia ZAT, TRA, BUMACO POSTA,World of Sports Kikwajuni, PSSSF Zanzibar, Azam Media,TTCL, Shirika la Bandari Zanzibar pamoja na Sea Cliff Zanzibar.

Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.