Habari za Punde

RC Tabora Balozi Dkt.Buriani Ahimiza Wakulima wa Mazao Yanayohimili Ukame.

Mkuu wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani akitoa salamu za Serikali leo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Tabora.

Na Lucas Raphael,Tabora.

Viongozi wa kata,mitaa na vijiji katika manispaa ya Tabora wametakiwa kuwahimiza  wananchi  kulima mazao yanayohili ukame ili waweze kujikinga na njaa msimu ujao wa kilimo.

Alisema kwa mujibu wa utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa hapa nchini unaonyesha kuwa mvua za mwaka huu zitakuwa za wastani na chini ya wastani.

Wito huo ulitolewa jana  na  Mkuu wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati akitoa salamu za Serikali kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Tabora.

Alisema kufuatia kuwa mvua zitakazoanza kunyesha zitakuwa chini ya wastani ,wananchi wanatakiwa kulima mazao ambayo yakomaa kwa muda mfupi na yale ambayo yanahimili ukame kama vile viazi, mihogo, mtama  na choroko.

Aidha Balozi Dkt. Batilda alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kukabiliana na upungufu wa tatizo la mafuta ya kula nchini  na ndio maana imeamua kutoa mbegu za mkopo kwa wakulima walio tayari kulima alizeti.

Alisema wakulima ambao watapenda kulima alizeti watapatiwa mbegu kwa mkopo na watalipa mara baada ya kuvuna na kuuza alizeti yao.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito kwa wakulima wajiandikishe kwa Maafisa Ugani ili Serikali iweze kuwapa mbegu  zenye tija kwa mkulima.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Madiwani katika Manispaa ya Tabora kuanza mchakato wa kuanzisha Chuo Kikuu .

Alisema ikiwezekana wanaweza kuanzia katika Chuo cha Ualimu Tabora kwa kuanza na kozi za ualimu na baadaye wanaweza kuongeza kozi nyingine zikiwe za kilimo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.