Habari za Punde

Serikali kuwahamasisha wananchi kutembelea vivutuo vya utalii nchini - Utalii wa ndani


 WAJUMBE wa UWT kutoka Pemba wakiongozwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Leila Mohamed Mussa, wakiangalia kaburi la mrefu aliyejulikana kama Bi.Banji Faraji aliyekuwa mtawala wa Milki hiyo ya Fukuchani katika Karne ya 15 na 16.


NA  IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema inaendelea na juhudi za kuwahamasisha wananchi waendelee kutembelea vivutio vya utalii nchini.

Kauli hiyo ameitoa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe.Leila Mohamed Mussa, mara baada ya kushiriki ziara ya kutembelea vivutio vya utalii katika maeneo ya Fukuchani na Mvuleni uko Mkoa wa Kaskazini Unguja ya Wajumbe  wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kutoka Pemba.

Alisema utalii ni sekta muhimu inayoingizia Serikali fedha nyingi za kigeni zinazochangia kukuza uchumi wa nchi.

Leila alieleza kuwa serikali imeendelea kuweka mikakati imara ya kuhakikisha wananchi wazawa nao wanakuwa ni sehemu muhimu ya wadau wa utalii kwa kuhakikisha wanatembelea vivutio vya utalii na kuchangia fedha zinazoongeza kukua kwa pato la taifa.

Akizungumzia ziara hiyo Waziri huyo Leila, alisema UWT wameamua kutembelea vivutio hivyo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa ni kinara wa kutangaza sekta ya utalii kitaifa,kikanda na kimataifa.

Katika maelezo yake Waziri huyo aliwasihi wananchi mbalimbali wanaoishi katika maeneo yenye vivutio vya utalii kuhakikisha wanalinda rasilimali hiyo ili kuzuia uharibifu wa maeneo hayo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

 “Natoa wito kwa wananchi waendelee kuwa na utamaduni wa kutembelea vivutio vyetu vya utalii ili kujifunza na kujua mambo mengi kuhusu utalii na nchi kwa ujumla.

Leo nimeungana na wajumbe wenzangu kutoka Pemba tumetembele maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii tumepata historia ya maeneo hayo ambayo imetuongezea uelewa mkubwa katika shughuli zetu za kisiasa.”, alisema Waziri Leila.

Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kusini Pemba Bimkubwa Khamis Mohamed, alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa kwa kuona na vivutio vyenye historia nzuri ambayo awali hawakuijua.

Alisema kupitia ziara hiyo imemjenga kuwa balozi mzuri wa kutangaza utalii wa ndani hasa kwa wanawake na vijana ambao wengi wao wamekuwa na uelewa mdogo juu ya masuala ya utalii.

Bimkubwa, alipongeza Waziri huyo ambaye pia ni Mwakilishi wa Viti Maalum wa Mkoa wa Kusini Pemba kwa kuratibu ziara hiyo iliyowaongezea uelewa juu ya masuala ya utalii.

 

Kwa upande wake Sheha wa shehia ya Fukuchani haji Mohamed Juma, alisema serikali imevumbua maeneo ya Kale katika shehia hiyo ambayo yalikuwa wakiishi watu katika karne ya 15 na 16 jambo ambalo ni faraja kwa wakaazi wa eneo hilo.

Haji, alizija fursa mbalimbali wanazonufaika wananchi zikiwemo vijana kujiajiri na kupata kipato kinachotokana na kutembeza watalii wanaofika katika maeneo hayo.

 Maeneo yaliyotembelewa ni eneo la Fukuchani yenye majengo ya kihistoria lililokaliwa na Wareno,kaburi la mtu mrefu aliyejulikana kama Bi.Banji Faraji pamoja na pango la Ajabu katika eneo la Mvuleni.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.