Habari za Punde

Uwepo wa Mshikamano Tanzania Bara na Zanzibar Kushinda Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya - Mhe.Othman.


MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuna haja ya kufanyakazi kwa pamoja kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, ili kuyashinda magonjwa yasiyoambukiza na vita dhidi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo akiongea na Ujumbe wa Kamati ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Magonjwa yasiyoambukiza ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliomtembelea Ofisini kwake Migombani, Jijini hapa.

Amesema hii ni kutokana na ukweli kwamba pande mbili hizo zinahitaji mshikamano wa kubadilishana uzoefu ili kufikia mafanikio na kuongeza hatua zaidi kwaajili ya kushinda vita hiyo, pia kwa kuzingatia nyenzo ziliopo.

“Iwapo dunia inakuja pamoja katika kukabiliana na changamoto mbali mbali, kwa Zanzibar na Tanzania Bara wanahitaji mshikamano zaidi, ili kutekeleza na kufanikisha mapambano hayo”, amesema Mheshimiwa Othman.

Aidha Mheshimiwa Othman amebainisha changamoto zinazojitokeza kutokana na mbinu za kisasa wanazoendelea kutumia wahalifu wa dawa za kulevya, kulingana pia na mazingira ya kiutendaji yaliyopo, huku kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukishikilia sheria yake.  

Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bi Fatma Hassan Tawfik ameeleza imani na matumaini waliyonayo, na kupongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika vita hiyo, zikiwemo kuanzisha Kituo cha Kurekebisha Tabia kwa Waathika wa Dawa za Kulevya, kiliopo Kidimni  Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo ujumbe huo ulipata fursa ya kukitembelea.

Kamati hiyo iliyopo kisiwani hapa kwa ziara maalum ya kujifunza, imetoa wito kwa Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar, kuwapatia nyenzo na miongozo muhimu, vijana ambao watapata udakhili katika kituo hicho, zikiwemo stadi za kazi na maarifa, kwaajili ya maisha yao ya baadaye.

Ujumbe huo uliowajumuisha Wabunge na Watendaji mbali mbali, wakiwemo Kamishna Mkuu wa Dawa za Kulevya Tanzania Bara, Bw. Gerald Kusaya, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Dawa za Kulevya, Bw. David Maganga, na Wajumbe wa Kamati hiyo Bw. Khalifa Mohamed Issa, Dokta Alice Kayange, Bi Asia Msangi, na Dokta Steven Kiruswa, hapo kabla ulipokelewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Saada Mkuya Salum.

Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

16/11/2021

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.