Habari za Punde

Wataalamu wa Mifugo Wanaokiuka Taratibu Kuwajibishwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 39 wa kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) unaofanyika Mjini Dodoma ambapo ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kwa wataalamu wa afya ya wanyama wakiwemo madaktari wa mifugo ambao wataenda kinyume na taaluma na maadili ya taaluma yao.
Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (RVCT) Dkt. Bedan Masuruli akizungumza kwenye mkutano wa 39 wa kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) unaofanyika Mjini Dodoma juu ya maadili ya taaluma ya afya ya wanyama na madaktari wa mifugo katika kuzingatia taratibu za maadili. 
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) Prof. Esron Karimuribo akizungumzia juu ya mojawapo ya malengo ya TVA ni kuwa jukwaa la kuwezesha kubadilishana maarifa, ujuzi, mawazo, uzoefu na ubunifu kupitia mikutano ya kisayansi ambayo hukutanisha wataalamu wa tasnia ya tiba ya wanyama ndani na nje ya nchi. Prof. Karimuribo amebainisha hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 39 wa kisayansi wa TVA unaofanyika Mjini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Anneth Kitambi akifafanua juu ya sheria ya ustawi wa wanyama, wakati wa mkutano wa 39 wa kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) unaofanyika Mjini Dodoma
Muonekano wa baadhi ya washiriki wa mkutano wa 39 wa kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) unaofanyika Mjini Dodoma. Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Kuendeleza Afya Moja Katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Magonjwa ya Mlipuko Katika Kuunga Mkono Uchumi wa Kati na Malengo ya Maendeleo Endelevu.” (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Na. Edward Kondela

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kwa wataalamu wa afya ya wanyama wakiwemo madaktari wa mifugo ambao wataenda kinyume na taaluma na maadili ya taaluma yao.

 

Waziri Ndaki amebainisha hayo leo (24.11.2021) wakati akihutubia katika ufunguzi wa mkutano wa 39 wa kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) unaofanyika kwa siku tatu jijini Dodoma, ambapo amesema wafugaji wana changamoto nyingi hivyo wanawategemea wataalamu hao katika kuhudumia mifugo yao badala kuwaongezea matatizo kwa kufanya kazi kinyume na utaratibu na maadili.

 

Akizungumzia juu ya matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakijitokeza hapa nchini kwa baadhi ya wataalamu wa afya ya wanyama na madaktari wa mifugo ya kutoa chanjo kinyume na utaratibu kwa mifugo na kuisababishia madhara na mingine kufa pamoja na kushiriki matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwakandamiza wafugaji, Waziri Ndaki amesema ni wajibu wa wataalamu kuhakikisha wafugaji wako salama na mifugo yao.

 

“Wataalamu zingatieni taaluma na maadili ya taaluma za udaktari tusaidane na Baraza la Veterinari Tanzania, kuendelea kuwasimamia wanachama na kuwawajibisha kunapotokea ukiukwaji mkubwa wa kitaaluma na maadili, tusiwatetee.”

 

Ameongeza kuwa ili taaluma ya afya ya wanyama iende vizuri na kuheshimika ni lazima kuwajibishana pale ambapo yanafanyika mambo ambayo ni nje ya utaratibu na kukiuka maadili na kuacha utaratibu huo kuendelea.

 

Aidha, ametaka watanzania kwa ujumla wao wakiwemo wataalamu wa afya ya wanyama na wanachama wa TVA kuhakikisha wanaelewa vizuri na kusimamia Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na. 19 ya mwaka 2008.  

 

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Amosy Zephania, amesema wizara inafikiria namna ya kuangalia maadili ya taaluma ya afya ya wanyama ili kupatikana kile kinachotakiwa kutoka kwa wataalamu kwa kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa kimaadili na kitaaluma kutoka kwa baadhi ya wataalamu hao maeneo mbalimbali nchini.

 

Aidha, Bw. Zephania ameongeza kuwa Mwaka huu wa 2021 Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mapitio ya Sera ya Mifugo ya Mwaka 2006 iliyodumu zaidi ya miaka 15, ambapo wizara inahitaji ushiriki wa kikamilifu kutoka kwa wafugaji na wataalamu katika mapitio ya sera hiyo ili kuainisha mapungufu yaliyopo na kuyafanyia marekebisho.

 

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) Prof. Esron Karimuribo amesema mojawapo ya malengo ya TVA ni kuwa jukwaa la kuwezesha kubadilishana maarifa, ujuzi, mawazo, uzoefu na ubunifu kupitia mikutano ya kisayansi ambayo hukutanisha wataalamu wa tasnia ya tiba ya wanyama ndani na nje ya nchi.

 

Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (RVCT) Dkt. Bedan Masuruli akizungumza kwenye mkutano huo juu ya maadili ya taaluma ya afya ya wanyama na madaktari wa mifugo ili kuzingatia taratibu za maadili kunahitajika mabadiliko ili kuhakikisha kuwepo na maadili ya kutosha kwa wataalamu hao, huku Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Anneth Kitambi akifafanua juu ya sheria ya ustawi wa wanyama ambapo wanyama wamekuwa wakikosa haki zao za msingi zikiwemo za muda wa kufanyishwa kazi, usafirishaji, uchinjaji na malisho.

 

Kauli mbiu ya mkutano wa 39 wa kisayansi ulioandaliwa na Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA) ni “Kuendeleza Afya Moja Katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Magonjwa ya Mlipuko Katika Kuunga Mkono Uchumi wa Kati na Malengo ya Maendeleo Endelevu.”

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.