Habari za Punde

Bodaboda watakiwa kutii sheria

 

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Bi Rahma Kassim Ali amesema  sekta ya usafiri wa Bodaboda na Bajaji ni sekta mpya  kwa Zanzibar hivyo kuna haja ya kutoa elimu ya matumizi bora ya barabara hususani kwa waendesha bodaboda, bajaji na watumiaji wa huduma hiyo.

Aliyasema hayo  wakati akifungua mafunzo kwa waendesha bodaboda katika viwanja vya Mao Zedong Mjini Zanzibar ambayo yameandaliwa na Shirika la Bima Tanzania.

Alisema usafiri huo umerasimishwa rasmin Zanzibar kwa mujibu wa sheria hivyo matumaini yake kuwa washiriki wa mafunzo hayo watapata fursa ya kueleweshwa undani wa sheria na kauni zake pamoja na kujikinga na majanga yatokanayo na ajali za barabarani.

Waziri huyo aliipongeza Jumuiya ya Bodaboda kwa kujipanga na kusimamia uundwaji wa Jumuiya yao ambayo ni kiunganishi kikuu baina ya Serikali kupitiai Idara husika na waendesha bodaboda katika kuweka mazingira bora ya utendaji kazi, usalama wa raia na taifa kwa ujumla.

Alieleza kuwa aina hiyo ya usafiri ina changamoto nyingi hususan kwa madereva, abiria na watumiaji wa barabara na changamoto nyingi zinahusiana na ukiukwaji wa sheria na miongozo mbalimbali ya matumizi bora ya barabara kwa vyombo vya moto.

Kwa upande wake Kamishna wa Bima kutoka mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dk Mussa Juma, alisema wametoa elimu hiyo ili madereva hao kujua madhara wakati ajali inapotokea kwa kuokoa maisha yao na abiria wao.

Naye afisa mnadhimu wa kikosi cha Usalama wa Barabarani, Mkadam Khamis Mkadam  aliwataka madereva hao kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza madhara yatokanayo na ajali za barabarani.

Alisema kazi ya kusafirisha abiria kupitia usafiri wa bodaboda ni kazi kama kazi nyengine  hivyo aliwataka kuithamini kazi yao hiyo na kuwa wasafi  na watanashati ili kazi yao hiyo ikubalike katika jamii.

Mkadam ambae pia Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, alisema kuwa elimu hiyo wanayoitoa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais, Mhe Samia ya kuwataka wasiwe wakamataji tu lakini pia kutoa elimu kwa makundi yote ya watumiaji wa barabara.

Madereva waliopatiwa mafunzo hayo walisema kuwa watahakikisha elimu waliyopatiwa wanaifanyia kazi na kuwataka madereva wezao  kuhakikisha wanafuata sheria za barabarani ili kupunguza ajali za barabaran na kuokoa maisha ya wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.