Habari za Punde

Halmashauri zimetakiwa kutenga fedha kukarabati viwanja vya michezo nchini

 

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akiongea na wanamichezo na mashabiki wa michezo wakati wa kufunga mashindano ya ligi ya Chemchem Cup Desemba 24, 2021 katika kijiji cha Vilima Vitatu kata ya Nkaiti iliyopo katika wilaya ya Babati Vijijni mkoani Manyara

Na Eleuteri Mangi, WUSM, Babati

Wakurugenzi na Maafisa Michezo katika halmashauri zote nchini wametakiwa kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati viwanja vya michezo ili kuhakikisha michezo inachezwa kuanzia ngazi ya chini hadi kitaifa.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ametoa rai hiyo Desemba 24, 2021 katika kijiji cha Vilima Vitatu kata ya Nkaiti iliyopo katika wilaya ya Babati Vijijni mkoani Manyara wakati wa kufunga mashindano ya ligi ya Chemchem Cup ambayo imeshirikisha vijiji 10 wanachama wa jumuiya ya uhifadhi wanyama Kurunge.

Lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha jamii kuhifadhi wanyama pori na kutunza mazingira katika maeneo yanayozunguka hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara.

“Sisi kama Wizara tumeanza kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, tumeanza kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo, tumeanza na nyasi za bandia katika mwaka huu wa fedha na mmesikia Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametupa maelekezo pia tukae na wenzetu wa Wizara ya Fedha tuone ni kwa kiasi gani vifaa vya michezo vitapungua bei ili huku chini tuweze kumudu michezo” amesema Mhe. Gekul.

Naibu Waziri Gekul amewataka Wakurugenzi wa halmashauri waone sababu ya kukarabati viwanja hivyo kwa kuwa vipo chini ya Madiwani, Mwenyekiti wa halmashauri na chini ya kata na hivyo vikarabatiwe kwa kushirikiana kwa pamoja na wadau wakiwemo wawekezaji ambao wapo maeneo mbalimbali nchi nzima.

Ili kuhakikisha michezo inachezwa nchi nzima, Naibu Waziri amesema kuwa viwanja vingi vipo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), jukumu hilo siyo lao peke yao bali ni la Serikali nzima ambapo wanashirikiana kuhakikisha azma hiyo inafikiwa na inakuwa na tija kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Mashindano haya yawe ni chachu ya kupata timu ya mkoa ili kushiriki mashindano ya Taifa Cup ambayo imeanza mwaka huu, naamini kupitia mashindano ya wilaya zote za mkoa wetu tutapata wachezaji bora wanaounda timu ya mkoa wa Manyara, hatua hii itayowafanya wachezaji wetu waongeze wigo mpana katika michezo na kuwafanya waweze kusajiliwa kuweza katika vilabu vingine nje ya mkoa wetu” amesema Naibu Waziri Gekul.

Naibu Waziri Gekul amesisitiza kuwa Sera ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995 inaeleza michezo kuwa siyo suala la mtu mmoja, michezo ni ya Serikali Kuu kupitia Wizara yenye dhamana na michezo, ni ya Serikali za Mitaa, ni ya mtu mmoja mmoja na michezo ni ya wanajamii nzima.

Ligi hiyo ni ya saba na imegharimu zaidi ya Sh. milioni 25 yakihusisha gharama za uendeshaji, zawadi yakiwemo makombe kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu, timu yenye nidhamu, mfungaji bora, golikipa bora pamoja na kocha bora katika ligi hiyo ambayo ilishirikisha vijiji 10 ambapo timu ya Marcklione imeibuka kidedea na kuwa mshindi wa kwanza katika fainali hizo kwa kuifunga timu ya Minjingu Fc kwa jumla ya magoli 4-0.

Kwa upande wake Mwekezaji wa Chemchem ambayo inatoa huduma ya wanyamapori ya Burunge inayojumuisha vijiji 10 katika eneo hilo Bw. Nicolaus Negre amesema lengo la mashindano hayo ni kuwaleta watu pamoja ili kuwahamasisha juu ya kuwatunza wanyama pori pamoja na mazingira yanayowazunguka.

Aidha, Bw. Nicolaus ameongeza kuwa mashindano hayo yamekuwa na hamasa kwa vijana wa eneo hilo kwa kuwa yanawasaidia kuendeleza na kuonesha vipaji vyao hatua inayowasaidia kuweza kusajiliwa na vilabu vingine.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika kijiji cha Vilima Vitatu kata ya Nkaiti iliyopo katika wilaya ya Babati Vijijni mkoani Manyara wakati wa kufunga mashindano ya ligi ya Chemchem Cup

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul (wa kwanza) akikagua timu kabla ya kuanza kwa mechi ya fainali za mashindano ya ligi ya Chemchem Cup iliyozikutanisha timu za Marcklione na Minjingu Fc ambapo timu Marcklione imeifunga timu ya Minjingu Fc kwa magoli 4-0 Desemba 24, 2021 katika kijiji cha Vilima Vitatu kata ya Nkaiti iliyopo katika wilaya ya Babati Vijijni mkoani Manyara.

Baadhi ya mashabiki wakifuatilia mechi ya fainali ya mashindano ya ligi ya Chemchem Cup ambayo imezikutanisha timu za Marcklione na Minjingu Fc ambapo timu Marcklione imeifunga timu ya Minjingu Fc kwa magoli 4-0 Desemba 24, 2021 iliyochezwa katika kijiji cha Vilima Vitatu kata ya Nkaiti iliyopo katika wilaya ya Babati Vijijni mkoani Manyara

Mchezo wa fainali za mashindano ya ligi ya Chemchem Cup ambayo imezikutanisha timu za Marcklione (waliovaa jezi ya bluu) na Minjingu Fc ambapo timu Marcklione imeifunga timu ya Minjingu Fc kwa magoli 4-0 Desemba 24, 2021 katika kijiji cha Vilima Vitatu kata ya Nkaiti iliyopo katika wilaya ya Babati Vijijni mkoani Manyara.

Mwekezaji wa Chemchem lodge ambaye pia ni mdhamini wa mashindano ya ligi ya Chemchem Cup 2021 Bw. Nicolaus Negre akiongea na wananchi Desemba 24, 2021 katika kijiji cha Vilima Vitatu kata ya Nkaiti iliyopo katika wilaya ya Babati Vijijni mkoani Manyara wakati wa kufunga mashindano hayo ambayo lengo lake ni kuwahamasisha juu ya kuwatunza wanyama pori pamoja na mazingira yanayowazunguka.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akimkabidhi Nahodha wa timu ya Marcklione katika kijiji cha katika kijiji cha Vilima Vitatu kata ya Nkaiti iliyopo katika wilaya ya Babati Vijijni mkoani Manyara Desemba 24, 2021 ambayo imeifunga timu ya Minjingu Fc kwa jumla ya magoli 4-0 katika mashindano ya ligi ya Chemchem Cup iliyoshirikisha vijiji 10 wanachama wa jumuiya ya uhifadhi wanyama yenye lengo la kuhamasisha jamii kuhifadhi wanyama pori na kutunza mazingira katika maeneo yanayozunguka hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.