Habari za Punde

JAMANI MSINIUMIZIE

 

Na.Adeladius Makwega - WUSM-UW-BENJAMINI MKAPA.

Nikiwa darasa la tano mkondo D, shule ya Msingi Mnazi Mmoja. Mapumziko ya saa nne nilikuwa na shilingi tano mfukoni nilinunua mihogo ya kukaanga kwa bwana mmoja ambaye alikuwa bahari mstaafu akiuza mihogo na juice na miwa.

Shilingi mbili nilinunua mihogo miwili na shilingi nilinunua Ice Cream na kusalia na shilingi mbili mfukoni. Eneo la shule ya Msingi Mnazi Mmoja lilikuwa kubwa hadi makutano ya Barabara inayoshuka kuelekea Kisutu na makutano na Mtaa wa Lumumba, kuelekea Sokoni Kariakoo. Katika kona hiyo ndipo muuza mihogo baharia mstaafu alikuwepo.

Baada ya kumaliza kula mihogo na Ice Cream Kengele ililia na mie kurudi darasani.Saa nane kengele ilipigwa na kurudi nyumbani ambayo yenyewe ilikuwa hatukai mstarini bali ni kuondoka tu makwetu. Katika wanafunzi waliokuwa wakikaa mbali na shule mimi nilikuwa mmoja wapo. Sihlingi mbili iliyobaki katika matumizi ilikuwa ni nauli ya kutoka Mnazi Mmoja hadi Temeke, alafu shilingi nyengine kutoka Temeke hadi Mbagala kwa mwanafunzi.

Nikiwa na rafiki yangu aliyekuwa akifahamika kama Alexzander ambaye alikuwa akikaa Kurasini jirani na Chuo Cha Ualimu Chang’ombe siku hiyo tukielekea Stendi ya Mnazi Mmoja nilibaini kuwa nimeangusha pesa yangu ya nauli.

Nilishindwa cha kufanya bali nikamueleza rafiki yangu Alexzander, Ndugu huyu aliniambia kuwa hilo halina neno tutatembea kwa mguu kutoka Mnazi Mmoja hadi Kurasini alafu yeye akifika kwake atanipa shilingi moja yake ili nikapande basi Mtoni Azizi Ali ili niweze kufika nyumbani kwa siku hiyo.

Kweli tulitoka zetu kwa mguu tukaambaambaa na Mtaa wa Lumumba hadi Gerezani, tukapita Mtaa wa Mafia tukaibuka na Msimbazi. Hapo tukavuka makutano ya KAMATA tukaanza na Barabara ya Kilwa tukatembea kidogo tukafuka hadi katika Viwanja vya Mpira wa Pete che Reli Gerezani.

Ndugu yangu Alexzander akaniambia kwa muda bado twende tukaangalie kinachoendelea ndani ya uwanja huo maana kulikuwa na kelele nyingi za kushangilia.

Tukiwa nje ya uwanja huu huku magari yakipita kuelekea Kurasini na Mbagala, tulichungulia getini na tulikaribishwa na milio ya filimbi za mchezo huo, huku sauti za kike zikisikika zikiyataja majina ya wadada wanaocheza mpira pete…Halima, Jane, Anna, Rose, pili Amina na Latifa mithili ya mwalimu anayewaita wanafunzi majina.

Tulipenya getini, wakati linamfungulia Mgeni Rasmi ambaye nadhani alikuwa Salim Ahmed Salim kwa kuwa tulikuwa tumevalia sare zetu za kaptura ya bluu na shati jeupe, tukiwa na mifuko yetu ya madaftari ya nguo, tuliweka madaftari tukayakalia na kutazama mchezo huo. Nikiwa pale nilivutiwa mno na wachezaji wa mchezo huo namna walivyovalia jezi zao ambazo zilikuwa na vifupisho vya herufi GK, GD, GA, WD, C, WA na GS herufi hizo zikipachikwa katika jezi zao za juu.

Ndugu yangu Alexzander ambaye alikuwa anaishi jirani na Polisi Kurasini alikuwa akiufahamu mchezo huu huku akiniambia C ni mchezaji wa kati(CENTER) ambaye anacheza popote isipokuwa katika mzunguko duara la goli tu.GS akiniambia ni (GOAL SHOOTER) huyu ni mfungaji.GK (GOAL KEEPER) mlinzi wa lango, GA aliniambia (GOAL ATTACK) anapeleka mashambulizi golini, WA ni mshambuliaji wa pembeni (WING ATTACK), WD aliniambia ni mlinzi wa pembeni (WING DEFENCE) na GD ni mlinzi ambaye analinda hata lango la goli.

Jezi hizo zilikuwa na blauzi zenye mikono mifupi na sketi fupi sana ambazo zilinivutia mno namna walivyokuwa wakiruka juu wakiwa angani zikipepea kama bendera mlingotini kana kwamba mchezaji wa ngoma za asili aliyevalia kibwaya.

Huku chini wakiwa wamevalia viatu kama laba hivi ambazo ziliwasaidia kuweza kukimbia katika kiwanja hicho kilichokuwa kimejengwa kwa sakafu. Japokuwa siku hiyo sikuona mchezaji hata mmoja akidondoka.

Huku mie mtazamaji nikijiuliza je wakianguka itakuwaje? Alexzander alianiambia dawa zipo maana kwa chonjo niliona jamaa na sanduku lake la msalaba mwekundu.

“GK-GS, WD-WA, GD-GA, C-C, GA-GD, WD-WA na GK–GS Hivyo ndivyo wanavyocheza kwa kukabana kila mmoja na mwenzake.” Alisema rafiki yangu Alexzander.

Baada ya dakika kadhaa walibadilishana na mie nilimwambia rafiki yangu kuwa mimi naenda Mbagala ni mbali sana twende zetu.

Kweli tulitoka na kuendelea na safari yetu ya kuunga mkono azimio hadi Kurasini. Hapa ndugu yangu Alexzander alifika kwao na kubadilisha nguo na kunisindikiza hadi kambi ya Jeshi la Wananchi ya Twalipo huku akinikabidhi shilingi moja ya kwenda kupanda basi Mtoni Azizi . Nilipofika Aziz Ali nikapanda zangu UDA za Temeke- Kongowe hadi Mbagala 77 niliposhuka.

Nilipofika nyumbani tu huku nikiulizwa mbona leo naingia usiku wakati shule nimetoka mapema? Nilieleza kilichotokea huku nikikaa kimya kuwa pia nilipita kutazama mpira wa Pete pale Gerezani.

Nimelikumbuka tukio hili kwa kuwa sijautazama mchezo wa mpira wa pete kwa miaka mingi sana tangu tukio hili nililosimulia, nimeambiwa kuwa mwaka huu katika Samia Taifa CUP mpira wa Peta ni miongoni mwa michezo itakayochezwa

Nakwambia, mwanakwetu mimi nitakuwa mtazamaji mmojawapo ambaye sintokosa mechi hizo hasa mandari ya uwanja na wachezaji wake wakiwa na jezi zao namna watavyokuwa wakiruka juu kugombani mipira katika mechi hizo kati ya mikoa yote ya bara na viziwani.

Maana unaweza ukatazama mechi hizo alafu ukampenda mchezaji wa mkoa fulani alafu ukasikia neno limekutoka

“Jamani msiniumizie.”

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.