Habari za Punde

KRISIMASI YA ZAMANI TULILEWA TOGWA

 

Na.Adeladius Makwega -- MBEYA.

Maandalizi ya sikukuu ya Krisimasi majumbani mwa wakristo na wale wasio wakristo yamekuwa yakipitia hatua mbalimbali katika jamii za Kitanzania. Jambo hilo limekuwa likibadilika kulingana na muda. Nadhani hata namna Krisimasi inavyosherehewa leo sivyo ilivyokuwa ikisherehekewa miaka ya kati ya1960 na1990.

Leo hii natazama namna krisimasi ilivyosherekewa miaka ya 1980 ambapo mimi na wazazi wangu tulitoka kijijini cha Mkelezange Mkoa wa Pwani na kwenda kwenye sikukuu hiyo Mbagala Dar es Salaam.

Tulifika Mbagala Mbuyuni siku ya jumamosi Dar es Salaam nyumbani kwa Bibi yangu mzaa baba. Bibi huyu tulimkuta akitwanga unga wa kutengenezea tongwa katika kinu chake na sie wageni kutoka mashambani ndiyo tumeingia mijini. Tongwa likatengezwa vizuri huku wakiutangwa ulevi/mtama ambao ulichekechwa katika chekeche la mbao na kutoa unga

Baada ya kupatikana unga huo uliwekwa katika maji na kuwekwa mekoni kwa muda na baadaye kupoa na kuhifadhiwa bila ya kuwekea hamira huku ikiwekwa sukari kiasi, na ulipopoa uliwekwa pahala ambapo palikuwa salama jirani na mtungi wa maji.

Kwa kando akinamama walikuwa wakimenya viungo vya pilau na kuvitwanga katika kinu kikubwa ambacho hicho ndicho kilichotumika kutwangia unga wa tongwa. Jua lilipozama yalianza maandalizi ya kwenda kanisani huku waliobakia hapo nyumbani wakikanda unga wa maandazi ambayo yalitakiwa kuumuka ili kukicha asubuhi waweze kuchomwa vizuri kwa ajili ya chai ya asubuhi siku ya Krisimasi.

Ilipofika saa mbili tulianza safari ya kwenda kanisani tukiongozwa na shangazi zangu wengi ambapo nyumbani kwetu tulijaliwa sana kuwa mashangazi wengi warembo. Naposema warembo sitanii walikuwa kweli warembo maana shangazi ni baba na shangazi huwa hataniwi. Tulipofika kanisani tuliingia katka kanisa moja dogo hivi ambapo watoto wadogo wote tulikalishwa mbele huku tukioneshwa sinema ya Yesu ambayo ilinipa taswira namna Yesu alivyozaliwa.Hii ilikuwa ni sinema yangu ya kwanza kuiona tangu nizaliwe.Nilitambua kumbe Yesu alizaliwa vile, huku akili yangu iikiingiza kitu kipya kabisa.

Tuliitazama picha hiyo na baada ya muda sasa tulienda katika kanisa kubwa kwa ajili ya misa ya krisimasi, kanisa hilo kubwa lilikuwepo katika nyumba ya makazi ya Shirika la Watawa wa Wadada wa Wadogo leo hii, kanisa hilo kubwa nadhani lilibomolewa na kujengwa nyumba hiyo ya watawa hawa wa kike.Tulisali usiku huo huku zikiimbwa nyimbo nyingi za wakati huo, kwa kuwa nilikuwa napenda kuimba kiasi niliupenda wimbo huu.

Mtoto amezaliwa kwa ajili yetu sisi, Tumepewa mtoto mwanaumee, Mwenye ufalme mabegani mwake Malaika wa shauri wa kuu.

Kwa kuwa tulikwa wadogo ili kutopotea tulishikwa mikono usiku huu na kurudi nyumbani kulala. Kulipokucha watu wazima walishaamka alfajiri na kuchoma maandazi ya kunyea chai ya maziwa na maandazi. Wengine kuelekea kanisani kusali huku tukiambiwa kuwa wale waliosali usiku, mchana wasiende kusali ili kubakia nyumbani kufanya maandalizi ya chakula. Hilo liliwagusa wakubwa hasa kina shangazi lakini mie halikunigusa bali nilienda kusali ili kumuona huyo mtoto Yesu aliyezaliwa usiku.

Tulitoka Mbagala Mbuyuni hadi Mbagala Magegeni, Hapa tulikutana watoto wadogo wakitutania na hasa mimi kwani nilivaa suruali yangu ambayo ilikuwa  haigusi viatu huku soksi zangu zikionekana, watoto hawa waliigiza milio wa njiwa, huku wakitumwagia michanga, kana kwamba mie ni njiwa. Wakimaanisha kuwa nimevaa suruali ya njiwa.

Nikiwa na ndugu zangu niliwatazama tu hawa jamaa maana nilisema kuwa sasa siyo wakati wa ndundi (wakati wa ugomvi) bali wakati wa kumuona Yesu huyu aliyezaliwa. Hapa tukavuka barabara tukaenda kwa mguu hadi Mbagala Msalabani moja kwa moja hadi Mbagala Misheni kanisani kusali. Kanisani kwa mbele kulikuwa na mfano wa mwanasesere aliyebebwa kama mtoto na wazazi wake, akifanana na ile picha  ambayo tulionesha usiku uliotangulia, tukamaliza kusali.

Tuliporudi nyumbani, tulikuta tayari mandhari ya nyumbani imeshaonesha dalili kuwa ni sikukuu, pilau likinukia kweli kweli. Tuliyotoka kanisali tulipewa chai ya maziwa maandazi tukanywa vizuri. Maana kwa mara ya mwisho maziwa niliyanywa nikiwa Mpwapwa wakati huko Mkuranga ilikuwa ni nadra sana hata kuona ng’ombe na hata kunywa maziwa na sikuwahi kumuona ngombe kwa kipindi chote nilichokuwa huko zaidi ya ng’ombe niliyemuona katika vitabu vya shule tu. Kwa hiyo hapo krisimasi ya Mbagala ilinoga mno.

Tukiwa tunakunywa chai hiyo nilisikia majina yakitajwa, wali huu peleka kwa mama Faida, Wali ule peleka kwa mama Hadija, Wali huu peleka kwa akina Hadija Adidas, Wali huu peleka kwa Bi Mminge, Sufuria kubwa peleka kwa Hadija Mpare, wali huu peleka kwa Hadija Kitotola. Hao waliokuwa wakipelekewa wali huo walikuwa ni majirani na marafiki wa nyumbani kwetu ambao walikuwa waisilamu. Nakumbuka hata wao wakati wa Iddi walikuwa wakileta kila aina za pilau na wali. Nakumbuka hapo nyumbani kuna sikukuu moja ya Iddi pilau za familia fulani zilikuwa tamu sana.

“Mama Faida anajua sana kupika pilau, yale ni mapishi ya Kilwa.”

Niliwahi kuwasikia hata baba zangu wadogo wakisifia mabinti wa mama huyu kuwa ahhh wale wanajua sana kupika, itabidi tuoe kwao. Wakati hii leo hao baba zangu wadogo wala hawakuwaoa mabinti wa mama huyu. Nadhani ilikuwa kilemba cha ukoka? Swali je pilau letu lilikuwa tamu kwa majirani hao? Hilo silifahamu.

Kweli safari ya kupeleka pilau hizo majumbani ilifanyika. Nikiwa pale mezani nakunywa chai nilitamani kazi ya kupeleka hizo pilau majumbani mwa majirani kwani unapata wasaa wa kudokoa kidogo, kwa hakika utoto umejawa na umelo wa kulakula lakini siku hiyo sikupata nafasi ya kuitwa kuipeleka pilau kwa majirani hao. Nilitamani mno kuipeleka pilau hiyo kwa akina Hadija Adidas, maana huyu alikuwa binti tuliyekuwa tunalingana rika kwani hata ile michezo ya Kombolela, Baba na Mama wanavuta sigara sports na Kula mbakishie baba nilikuwa nacheza naye.

Sasa ukawa wasaa na sie kula pilau hilo hapo nyumbani ambapo tuliyatupa mawe pangoni vilivyo baada ya kumaliza siye wadogo tulikikabidhiwa tongwa katika kikombe cha bati na kuanza kunywa kidogo kidogo.

Tongwa hilo lililowekwa katika mtungi maalumu lilikuwa limepoa mithili ya soda iliyozamishwa katika jokofu. Baada ya muda iliagizwa kuchukuliwa Redio Kaseti kutoka kwa mjomba wangu mmoja Ndugu Tanu Mswago aliyekuwa mwanajeshi wakati huo ambaye alishiriki vita vya Kagera alikuja na redio Kaseti yake. Ilichukuliwa redio kaseti hiyo huku ikiwa imefunikwa kitambaa chenye maandishi ya kufumwa Mery X Mass zikaanza kupigwa nyimbo kadhaa kupamba sikukuu hii.

Watoto wote mawazo yetu yalikuwa katika tongwa ambalo lilikuwa mtungini.Wengine wakisherekea sikukuu hiyo sisi tulikuwa tunatafuta upenyo tunaenda kuchota tongwa mtungini na kunywa. Wakubwa wakilisakata rumba la kuzaliwa kwa Bwana Yesu sie tuliendelea kugida tongwa taratibu nalo jua likizama kwa spidi mithili ya gari linaloshiriki mashindano ya fomula one.

Siku ya Krisimasi ilipita na siku iliyofuata togwa letu lilikuwa bado limebaki katika mtungi kwa hiyo siye watoto tuliendelea kunywa tongwa hilo, unapiga chai kikombe imoja na tongwa vikombe viwili.

Sasa tongwa hilo tulilifakamia mno na mara tukashangaa tunaanza kupepesuka, jamani nyie watoto vipi? Swali hilo liliulizwa, hao wanafanya utani tu, watu wengine walisema, wanatutania tu. Nina binamu yangu mmoja yeye alitia fora zaidi kwani sasa alikuwa amelewa chakali, kumbe tongwa letu limebadilika na kuwa pombe. Binamu huyu usingizi ulimpitia na kulala, uzingizi mzito. Baadaye mkubwa mmoja ndipo alibaini kuwa lile tongwa lilishachachuka, msiwape watoto, wanalewa! hilo sasa ni tongwa la wakubwa .

Ilipofika saa saba mchana na mie nikawa nimelewa chakari tongwa ya krisimasi hapo tena ninasimuliwa kuwa mara baada ya kulewa ilibidi nitafutiwe pahala pa kulala na kulazwa kwenye mkeke wa bibi. Maana ulevi wa tongwa ulikuja na usingizi mzito nikiota ndoto ya picha ya Yesu namna Mama Jusi wa Mashariki ya Mbali walivyokuwa wakiifuata nyota na kumtafuta kumuona mfalme aliyezaliwa. Nililala muda mrefu, niliamka saa 12 jioni, nilidhani kuwa hiyo ni siku nyengine huku nikitaka tena kuukimbilia mtungi wa tongwa ambapo sasa wakubwa walishaumaliza.

Kweli tulikaa Mbagala kwa juma moja zaidi na baadaye kurudi kijijini Mkelezange kuendelea na maisha yetu ya kijijini nyumbani kwa Profesa Kighoma Malima.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.